The House of Favourite Newspapers

Tanzania Hatuna Ugomvi na Kenya, ni Kanuni za Diplomasia – Video

0

SERIKALI imesema kuwa haina mgogoro wowote wala ugomvi na nchi ya Kenya na kwamba Serikali hizi zinashirikiana kwa mambo mengi mpaka sasa, lakini suala la kufunga mipaka na anga yalikuwa ni maamuzi ya nchi moja moja kuchukua tahadhari kuhusu kusambaa kwa gonjwa hatari la Covid-19.

 

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Agosti 11, 2020, na Dkt. Hassan Abbas, Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akifanyiwa mahojiano na front Page ya +255 Global Radio.

 

“Suala la diplomasia ni pana sana, unaposema ushirikiano wetu na nchi za nje unashuka una maanisha nini? Kumbuka mpaka sasa Rais wetu ni Mwenyekiti wa SADC (Kumuia ya  Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) na hivi karibuni atakabidhi kwa nchi nyingine, ungekuwa na uhusiano mbaya ungepewa uenyekiti wa SADC?

 

“Mhe. Rais anapokea mabalozi kila siku, anaapisha mabalozi kila mara na kuwapeleka nchi nyingine, kama huna mahusiano nao utapelekaje balozi? Bado sisi ni wanachama wa UN pia tuna miradi mingi ambayo tunafanya pamoja na benki kubwa ikiwemo ya AfDB na WB.

 

“Tuna mahusiano mazuri na Kenya, hili suala la corona lilikuwa ni dharura, kila nchi ilichukua tahadhari zake, wengine walifunga mipaka wakiamini corona wataidhibiti, mfano Kenya, China, Zambia, Marekani, Uingereza, lakini mpaka sasa corona bado ipo, sisi tulifunga michezo.  Je, tulikuwa na ugomvi na wanamichezo?  Haya mambo kila mmoja alikuwa na mbinu zake za kupambana na gonjwa hilo, lakini tunashirikiana vizuri.

 

“Diplomasia inaongozwa na Kanuni inaitwa “reciprocity”, Tanzania haikutajwa katika nchi zilizoruhusiwa kuingiza ndege zao Kenya, kwa hiyo sisi tuliheshimu maoni ya jirani yetu ambae tuna uhusiano wa damu na kindugu, hivyo tukasema kama hatujaruhusiwa basi kwa kipindi hiki na wao wapumzike kuja. Kwahiyo sio ugomvi bali ni kanuni ya kidiplomasia.

 

“Hakuna kilichokwama kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta la Hoima, ni mradi ambao Tanzania tumenunua hisa, unatumia wabia ambao ni Total na wengine.  Hawa watekelezaji ulifika wakati wakatofautiana, lakini hiyo changamoto imekwisha, Agosti hii kazi inakwenda kuanza.

“Si kwamba kwa sababu ya uchaguzi sheria haifanyi kazi hapana, suala la CHADEMA kuongeza ubeti wao katika wimbo wa Taifa tumewaachia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wafate taratibu na sheria zao, kila chombo kina mamlaka inayokisimamia, hatujui huko kama wameomba radhi au vipi, wanatutoa relini, sisi tunajenga SGR (reli ya kisasa).

 

Dkt. Abbas amesema  Serikali imetekeleza miradi mingi katika sekta ya elimu na inaendelea kuboresha sekta hiyo ikiwemo kutumia zaidi ya TZS Trilioni 1 kugharamia elimu bila malipo katika miaka mitano iliyopita.

 

“Tunaposema elimu bure si kwamba ada tu, tumepeleka vifaa vingi vya shule, maabara, chaki, tumeajiri walimu, wataalam wa maabara wa fizikia na kemia, vitabu, madawati, tumejenga madarasa na majengo mengine tunakarabati.

 

“Uchumi wa kati maana yake umetoka kwenye uchumi wa kimaskini unakwenda kwenye uchumi wa kitajiri, tatizo watu wanachanganya mambo hapa.  Kuna vipimo kama GDP per capital (uchumi wa ndani wa nchi), GNI (mapato kutoka nje, inapimwa na Benki ya Dunia) kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo yanasababisha uchumi wako upande, sisi tumepita vigezo hivyo, tunapambana kwenda mbele zaidi.

 

“Nasisitiza tu kwamba tumeingia kwenye uchumi wa kati, maana yake ni kubadilika, uwe mtu wa tabasamu na ujiamini, zaidi nchi yetu ina amani tuendelee kuilinda, tunakwenda kwenye uchaguzi tubishane kwa hoja mwisho wa siku tuwe wamoja,” amesema Dkt. Abbas.

Leave A Reply