The House of Favourite Newspapers

Mastaa: We Gonna Miss You Nape

Nape kulia akisalimina na mashabiki wa soka nchini juzi uwanja wa Taifa.

Na GLADNESS MALLYA| IJUMAA WIKIENDA| HABARI

WE GONNA miss you! Ndivyo baadhi ya mastaa walivyosikika wakisema mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ kufanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kumteua Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Nape Moses Nnauye.

Kama msemo usemao ‘mazoea yana tabu’ hiyo imewatokea baadhi ya mastaa hao kwa kile walichodai kwamba walimzoea Nape na walifurahia kufanya naye kazi kwa ukaribu lakini ndiyo hivyo ‘watammis’ na kuendelea kufanya kazi na Mwakyembe. Katika makala haya, baadhi ya mastaa waliozungumza na Over Ze Weekend na kueleza ya moyoni mwao juu ya kiongozi huyo ambaye ni Mbunge wa Mtama (CCM);

BABY MADAHA:

“Nape ni waziri pekee aliyekuwa wa tofauti na waliomtangulia, alikuwa karibu na wasanii na ni mtu mwelewa na alikuwa free sana kuongea na mtu ndiyo maana hatua hiyo wasanii na wanahabari wengi wamejikuta wakihuzunika, tumuombee tu huyu aliyeteuliwa aweze naye kuhudhuria matamasha yetu ya usiku au mchana.”

SHILOLE

“Kiukweli siwezi kuongea hapa nalia na kuhuzunika tu.”

JIMMY MAFUFU

“Kuondoka kwa Nape ni pigo kubwa, nitoe tamko kama Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) kuwa Nape alifanya vizuri na kushirikiana nasi kama familia lakini ndiyo hivyo imetokea, tutaungana na Mwakyembe.”

KULWA KIKUMBA ‘DUDE’

“Kifupi nimeumia nimehuzunika, Nape alitutengenezea mazingira mazuri sana sisi na hata wanahabari, wanamichezo na wengine, amekuwa akishiriki matukio mengi sana yaliyo chini ya wizara yake, kiukweli tutammiss.”

KOLETHA RAYMOND

“Wizara ilimfiti kitaaluma, pia ni kijana mwenzetu aliyekuwa anaweza kuhimili mikiki ya wizara husika. “Utendaji kazi wake hasa kwenye upande wa sanaa tulianza kuuona na tulitegemea bado tutakuwa naye katika vita kwa sababu mikakati ilikuwa mingi ili kuiokoa tasnia ya filamu Tanzania!”

MICHAEL SANGU ‘MIKE’

“Kiukweli taarifa ya Nape ilinishtua sana. Lakini hakuna namna ndiyo utaratibu wa kazi, tulimzoea mno kwa kuwa tumefanya naye kazi tangu CCM (Chama Cha Mapinduzi) hadi leo.”

ISABELA MPANDA

“Nape alikuwa poa sana kwetu, tutammis kiukweli lakini hatuna budi kukubaliana na uamuzi wa rais.”

ESTER KIAMA

“Tulimzoea Nape na tunamuahidi kuyafanya yale yote aliyokuwa akituelekeza.”

MUHSEIN AWADH ‘DK. CHENI’

“Kwangu napokea kama mabadiliko mengine maana aliyemteua ndiye aliyembadilisha ni sawa na Mungu amekuumba ipo siku atakuchukua kwa wakati wake, uwezo wa kazi yake anayeujua aliyemteua na labda aliyemteua ameona hapo alipomuweka kumbadilisha ni yeye, sioni kama kuna lawama.”

Comments are closed.