The House of Favourite Newspapers

Watu Kibao Kutekwa 2017, Hatari Zaidi kwa Wasanii Wapewa Mwongozo

0
Nay wa Mitego (kulia) akiwa na Roma.

Na GLADNESS MALLYA| RISASI MCHANGANYIKO| HABARI

HALI ni tete! Kutokana na matukio ya utekaji yanayoendelea nchini, hali bado ni mbaya kwani habari zinaeleza kwamba bado matukio hayo yataendelea kwa wingi mwaka huu wa 2017, Risasi lina habari kamili.

Ili kujua kinachoendelea katika upande wa unajimu kuhusu mambo yanayotokea Tanzania kwa sasa ya mauaji pamoja na utekaji yataisha lini, Risasi Mchanganyiko lilifunga safari mpaka ofisini kwa mtabiri maarufu, Hassan Yahya Hussein ‘Maalim Hassan’ , Magomeni Mwembechai, Dar ambaye alieleza siri nzito.

Ben Saanane.

Maalim Hassan alieleza kuwa matukio ya utekaji kwa mwaka huu wa 2017 yataendelea kuwa mengi sana pia mauaji kwa kutumia risasi yataendelea kwa sababu mwaka huu ulianza siku ya Jumapili ambapo sayari inayotawala siku hiyo ni jua pia nyota inayotawala ni Simba ambayo asili yake ni moto.

“Yaani sayari ya jua inakuwa na mambo kama vile kiburi kwa hiyo watu watakuwa na kiburi sana, kutumia nguvu, ufahari, kuona haya, vyombo vya moto kama bastola hivyo masuala ya kupigwa risasi yatakuwa ya kawaida maana mwaka huu ni wa moto.

“Mwaka 2017 ni mbaya sana, watakaokuwa na nguvu kwa jambo wanalotaka lifanyike na litafanyika hata kwa nguvu ni wanasiasa na viongozi wa dini lakini watu wengine wanatakiwa kuwa makini sana wasiwe watu wa kuingilia sekta hizo maana watajikuta kwenye matatizo makubwa.

“Watu wanatakiwa kuwa na tahadhari kwa sababu huu ni mwaka wa viongozi wa kisiasa na kidini, nguvu itatumika hata sehemu ambayo haihiitaji nguvu,” alisema mtabiri huyo.

HATARI KWA WASANII

Mtabiri huyo aliendelea kusema kuwa hatari kubwa iko kwa wasanii endapo wataingia kwenye mambo ya kidini na kisiasa hivyo wanatakiwa kuwa makini katika hilo.

AWAPA MWONGOZO

Kufuatia mwaka huu nguvu kubwa kuwa kwa wanasiasa na viongozi wa kidini, Maalim Hassan aliwataka wasanii kusimama kwenye fani yao na wasiingilie mambo mengine ambayo hayahusiani na kazi yao.

“Kama wewe ni msanii wa muziki usiingilie mambo ya kisiasa wala kuimba, bora uimbe mambo yanayohusiana na jamii au mapenzi vinginevyo wakiingia huko itawapa matatizo watajikuta wakitekwa au kuingia kwenye matatizo mengine makubwa, nawasihi waachane na siasa kabisa iwe ni kwa wasanii wa muziki au filamu,” alisema Maalim Hassan.

Hata hivyo, aliwashauri raia wote wa Tanzania kuachana na kuingilia mambo ya kisiasa au ya kidini na wajihusishe na kazi zinazowahusu kwani mwaka huu siyo mzuri kwa mtu anayejiingiza kwenye kazi hizo ambazo hazimuhusu au kushabikia.

Katika mahubiri yake ya Ijumaa Kuu wiki iliyopita, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Bukoba,  Methedius Kilaini, alisema vitendo vya utekaji vinavyotikisa nchi kwa sasa, havimuachi salama mtu yeyote, kwani hata viongozi wa dini nao wanaweza kutekwa wakati wowote.

Alizitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa raia, kuwa makini zaidi kwani hofu iliyoligubika taifa kwa sasa ni kubwa.

Hivi karibuni msanii wa Muziki wa Hip Hop, Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ (pichani) na wenzake watatu walitekwa na watu wasiojulikana  wakiwa studio na kurudi siku tatu baadaye wakiwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Mwingine aliyewahi kutekwa ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane, hajapatikana mpaka sasa tangu alipotoweka Novemba mwaka jana.

 

Leave A Reply