The House of Favourite Newspapers

AVEVA, KABURU WAREJESHWA RUMANDE HADI JULAI 20

0
Evans Aveva (mwenye miwani kulia) na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wakipandishwa kortini leo.
Inaonekana bado mambo ni magumu kwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ katika kesi inayowakabili.
Leo wamepandishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar na kurudishwa rumande mpaka Julai 20, mwaka huu.
Awali viongozi hao walipandishwa mahakamani hapo Juni 29, na kusomewa mashitaka hayo wakidaiwa kughushi nyaraka zinazodaiwa walijilipa madeni kiasi cha dola 300,000.
Katika kesi hiyo namba 214 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, Aveva alikutwa na kosa la kutoa nyaraka za uongo kwenye Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam, Machi 10, 2016.
Kosa la tatu ni la kutakatisha fedha kinyume cha sheria ambapo inadaiwa Aveva na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo ikiwa ni kinyume cha sheria.
Katika kosa la nne, Kaburu alikutwa na shtaka la kutakatisha fedha na kuziweka kwenye Benki ya Barclays Tawi la Mikocheni jijini Dar es Salaam, huku kosa la tano la kutakatisha fedha hizo likimhusu Kaburu kutokana na kumsaidia Aveva kutakatisha fedha katika Benki ya Barclays kwa kughushi nyaraka.
Aveva na Kaburu walirudishwa rumande baada ya upande wa mashtaka ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kudai haujakamilisha ushahidi wake katika kesi yenye mashtaka matano inayowakabili watuhumiwa hao yakiwemo ya utakatishaji fedha.
Leave A Reply