The House of Favourite Newspapers

Makambo: Msikonde, Hasira Zote Ligi Kuu

Heritier Makambo

BAADA ya kuondolewa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Mkongomani, Heritier Makambo amewatuliza mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia watulie, wanarudisha hasira zao zote kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Kauli hiyo aliitoa baada ya timu hiyo kufungwa na Rayon Sports katika mchezo wa mwisho wa kukamilisha ratiba ya makundi katika michuano hiyo ambayo Yanga ilifungwa bao 1-0.

 

Katika mchezo huo, Makambo alitoka katika dakika ya 69 na nafasi yake kuchukuliwa na Yusuph Mhilu baada ya kupata majeraha katika mchezo huo uliojaa upinzani mkubwa.

 

“Tunajua mashabiki wetu wanataka ushindi katika kila mechi, hivyo hilo tunalifanyia kazi kuhakikisha tunawapa furaha ili waendelee kutusapoti katika ligi ambayo tumepanga kufanya vizuri msimu huu,” alisema Makambo.

Aidha, Kocha Mkuu wa Yanga, Zahera Mwinyi alisema majeraha ya Makambo hayana madhara makubwa.

 

“Aliumia kwa sababu ya uwanja haukuwa mzuri kutokana na mvua ambayo ilianza kunyesha tangu tunaanza mechi, ataendelea na mazoezi ambayo nimemuachia programu Kocha Noel Mwandila ambaye yeye ndiye atawasimamia wachezaji wote kwa kipindi hiki ambacho mimi sitakuwa na timu,” alisema Zahera ambaye ameelekea nchini DR Congo kwa majukumu ya timu ya taifa hilo.

Comments are closed.