The House of Favourite Newspapers

Kocha: Huyu Chama Balaa!

STAA wa zamani wa Simba, Talib Hilal ameikubali kombinesheni ya mastraika watatu wa timu hiyo kuwa inatisha na kueleza ina ubavu wa kurudia maajabu ya mwaka 2003 kwa kutinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba imevuka hatua ya awali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa jumla ya ma­bao 8-1 juzi Jumanne.

Simba itacheza na mshindi wa jana jioni kati ya Nkana Red Devils ya Zambia na UD Songo ya Msumbiji ambazo zilikuwa zinarudiana.

 

Simba ipo njia moja kusaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyofanya mwaka 2003 ilipoitoa Zamalek kwenye raundi ya tatu ya mtoano ambapo kipindi hicho ikinolewa na Talib aliyeshirikiana na mkenya James Siang’a.

Staa wa zamani wa Simba, Talib Hilal.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, Talib, ambaye alifanya makubwa Simba akiwa mchezaji na kocha kwa vipindi tofauti, aliifagilia timu hiyo kuwa ina mas­traika wa hatari Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco.

 

Talib, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Oman, pia amemvulia kofia kiungo mshambuliaji Clatous Chama, ambaye anaamini ameongeza makali ya makucha ya Simba.

“Washambuliaji wa Simba wanatisha kwanza hata kwa maumbo yao halafu pia ni wafungaji wazuri, sioni sababu wasifike mbali kwenye mashindano ya Afrika.

 

“Unajua Simba iliweka historia katika mashindano ya kimataifa miaka ya nyuma kwa kuwa walikuwa na mas­traika wakali, kama unawakumbuka kina Abdalla Kibadeni, Zamoyoni Mogela, Malota Soma na wengineo,” alisema Talib, ambaye alicheza kama sentahafu wakati Simba ilipoifunga Al-Ahly ya Misri mabao 2-1 jijini Mwanza mwaka 1985.

 

“Huyu Mzambia anajua mpira aisee, yaani kwanza ana sifa kuu mbili moja ya kuwa na kipaji cha kuufanya mpira anavyotaka pamoja na kuwachezesha wenzake halafu na pili ni balaa katika kufunga,” aliongeza.

Mchambuzi mahiri wa soka nchini, Mwalimu Kashasha alisema; “Chama ni mchezaji ambaye anastahili kuja kwenye Ligi yetu kama mchezaji wa kulipwa,ana akili ya ziada ya mpira. Akiugu­sa mpira ana­kuwa tayari ameshafanya maamuzi zaidi ya matatu apige pasi nyuma, mbele au aukokote.”

 

“Ni mchezaji mwepesi kucheza na wenzake, anachezea miguu yote miwili na anacheza anavyotaka na ana jicho la kuona mbali…pasi zake ni hatari sana na anafanya maamuzi haraka sana, ni mgumu sana kukabika,” alisisitiza Kasha­sha. Katika mabao mawili ya juzi, Chama alilisifia la kwanza.

CHAMA AFUNGUKA

“Siwezi kuacha kulitazama hili bao asante Mungu kwa kunipa nafasi ya kufunga na kuifanya Simba iweze ku­fanikiwa kwenda hatua nyingine katika michuano hii ya Caf mimi pamoja na wachezaji wenzagu,” alisema Chama.

“Hivyo, basi ninataka kuona timu yangu inafika katika hatua nzuri ya michuano hii mikubwa Afrika na hilo linawezekana kabisa kwa kushirikiana na wen­zangu,” alisema Chama.

 

Jana katika mitandao mbalimbali za Zambia gumzo ilikuwa ni Chama huku Nkana wakionywa kuwa nae makini.

Chama tayari ana mabao matatu kwenye Ligi ya Mab­ingwa Afrika huku Bocco na Kagere kila mmoja akiwa na mabao mawili.

 

Talib aliongeza kuwa: “Hizi mechi za nyumbani na ugenini ni muhimu sana kufunga mabao mengi na ku­timiza hilo ni lazima uwe na mastraika wazuri.” aliongeza Talib, ambaye aliinoa Simba pia mwaka 2007.

KAGERE ANENA

“Siyo kwa sababu tume­waondoa Mbabane ndiyo tuone tayari tumemaliza, bado tuna kibarua kigumu mbele tunapoelekea katika michuano hii ambayo ni migumu inakutanisha timu bingwa ya ligi.

 

“Hivyo, basi tumeanza vizuri michuano hii kwa kuwaondoa Mbabane na malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri na mwisho wa siku tufanikishe malengo yetu hilo ndilo jambo la msingi.”

SIMBA WAREJEA

Wakati huohuo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea leo Alhamisi saa 9 alasiri kiki­tokea Afrika Kusini kilipoun­ganisha ndege kutokea Eswatini kilipoenda kucheza na Mbabane.

SAMSON MFALILA,

Dar es Salaam

 

Comments are closed.