The House of Favourite Newspapers

WAINGEREZA WAMEAMUA…ARSENAL vs CHELSEA FAINALI EUROPA

BAADA ya kuona njia ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kupitia Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ ikiwa ngumu, sasa kasi ya Arsenal imekuwa kubwa upande wa pili, hiyo ni baada ya kufanikiwa kuingia Hatua ya Fainali ya Europa League, jana usiku.

Licha ya kuwa ugenini, Arsenal imefanya hivyo baada ya kuifunga Valencia kwa mabao 4-2 katika mchezo wa pili wa nusu fainali ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Mestalla.

 

Kwa matokeo hayo Arsenal imeingia fainali kwa jumla ya mabao 7-3 kwa kuwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa ndani ya Uwanja wa Emirates ulimalizika kwa wenyeji kushinda kwa mabao 3-1.

Wakicheza kwa taharadhi huku wakionekana kuwa makini Arsenal walianza kuruhusu bao katika dakika ya 11 kupitia kwa Kevin Gameiro lakini Pierre-Emerick Aubameyang ambaye amekuwa katika ubora wa juu msimu huu, alisawazisha dakika ya 17.

 

Wenyeji waliendelea kupambana lakini wakajikuta wakiongezwa la pili dakika ya 50 kupitia kwa Alexandre Lacazette, dakika nane baadaye Valencia wakapata bao la kusawazisha mfungaji akiwa ni Kevin Gameiro.

Kwa mara nyingine, dakika ya 69, Aubameyang akawatungua wenyeji wao bao la tatu kisha akaongeza la nne na dakika 88 na kumfanya awe amepiga hat trick katika mchezo huo.

 

CHELSEA WAWAFUATA FAINALI

Chelsea nao wamewafuata Arsenal katika fainali baada ya kuwafunga Eintracht Frankfurt wa Ujerumani kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 120. Chelsea wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 28 mfungaji akiwa ni Ruben LoftusCheek, lakini wageni walisawazisha kupitia kwa Luka Jovic katika dakika ya 49.

Hadi zinakamilika dakika 90 matokeo yalikuwa bao 1-1 huku ushindani ukiwa mkali. Zikaongezwa dakika 30 ambazo nazo hazikuwa na mbabe.

Waliopiga penalti kwa upande wa Chelsea ni: Ross Barkley, Cesar Azpilicueta (alikosa), Jorginho, Davide Zappacosta na Eden Hazard. Upande Frankfurt wapiga penalti Sebastien Haller, Luka Jovic, Jonathan de Guzmanm, Martin Hinteregger (alikosa) na Goncalo Paciencia. Finali Mchezo wa fainali unatarajiwa kupigwa Mei 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Olympic Stadium jijini Baku nchini Azerbaijan

Comments are closed.