The House of Favourite Newspapers

Rais wa China Aifagilia TZ, Korosho, Tanzanite Vyamkuna

MAONESHO ya pili ya kimataifa ya bidhaa zinazoagizwa China yamefunguliwa leo mjini Shanghai, China. Rais Xi Jinping wa China amehutubia ufunguzi huo.

 

Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya “zama mpya, kunufaika kwa pamoja na mustakabali wa pamoja” yameshirikisha zaidi ya makampuni 3,000 kutoka nchi na sehemu 150 za mabara matano duniani.

Katika hafla hiyo viongozi wa Mataifa 64 walihudhuria akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mawaziri Wakuu wa Jamaica; Serbia na Greece huku ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa. ‪

 

Aidha baada ya kufungua maonesho hayo Rais wa China ametembelea Mabanda ya nchi (5) yakiwemo mabanda ya Ufaransa; Ugiriki; Serbia; Jamaica na Tanzania.

 

Katika ziara ya kutembelea Banda la Tanzania Rais Xi Jinping alifuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Greece na Serbia na kupokelewa na Waziri Bashungwa.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, alitoa maelezo juu ya bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii. Aidha, Balozi Kairuki aliwasilisha salaam za Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli kwa Rais wa China.

Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaam za pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China.

 

Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China.

Comments are closed.