Absa MobiTap inawezesha wauzaji kupokea malipo ya kadi za benki kutoka kwa wateja kwa kutumia simu janja kama mashine ya kuchanjia kadi.
Benki ya Absa Tanzania imezindua Absa Mobi Tap – ambayo ni suluhisho la kwanza la aina yake nchini Tanzania ambalo linawawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati (SMMEs) kutumia simu zao kwa ajili ya kuchakata miamala ya kadi za benki na kuondoa hitaji la mashine za kuchanjia kadi, yaani POS.
Absa MobiTap inatarajiwa kuharakisha mchakato wa ulipiaji wa bidhaa kwa wanunuzi na wauzaji kwa kutumia simu janja kama mashine ya kuchanjia kadi. Wateja wanaweza tu kugusa kadi zao za benki kwenye simu ya muuzaji ya Android au kompyuta kibao ili kufanya malipo.
Kwa upande wa wafanyabiashara, wanachohitaji kufanya ni kupakua programu ya Absa Mobi Tap kutoka Play Store kwenye simu zao janja. Baada ya hapo wataweka taarifa zao na kuunganishwa na kuwa tayari kupokea malipo ya kadi za benki. Ili kuchakata malipo, mfanyabiashara ataingiza kiasi cha manunuzi kwenye program ya Absa MobiTap, kisha mteja atagusisha kadi yake nyuma ya simu hiyo na kuingiza PIN yake ikiwa inahitajika na kukamilisha malipo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ndabu Swere, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, alisema kuanzishwa kwa Absa Mobi Tap ni ushahidi wa mkakati wa benki hiyo kuendelea kujikita katika kujenga kampuni ya kisasa ya kidijitali ambayo inaenda na nyakati na mahitaji ya wateja.
“Kama benki inayoongozwa kidijitali, tumejitolea kuongoza njia katika uvumbuzi wa kidijitali na tutaendelea kuzindua suluhisho nyingi za kidigitali za ubunifu wa hali ya juu ambazo zinakidhi mahitaji ya wateja wetu ya sasa na ya baadae, na kuhakikisha kuwa bidhaa zetu zimeundwa kushughulikia changamoto ambazo wateja wetu wanakabiliwa nazo.
Absa MobiTap ni suluhisho la kwanza la aina yake hapa nchini na tunajivunia kuwa benki ya kwanza kuwaletea Watanzania suluhisho la malipo ya kidigitali la ubunifu huu wa kipekee.
Tunaamini suluhisho hili litaleta mapinduzi katika namna ambayo wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati nchini yanavyoendesha biashara zao, kwani itaondoa vizuizi na kupanua chaguzi katika upatikanaji wa huduma za malipo ya kidijitali.
Biashara nyingi ndogo ndogo hazikuweza kupata mashine za POS kwa sababu ya uwekezaji mzito unaohitajika kwaajili ya hizo mashine. Lakini Absa MobiTap amekuja kuleta ufumbuzi kwenye hili.
Sasa hata dereva wa Uber / Bolt anaweza kupokea malipo ya kadi kupitia simu yake ya mkononi ambayo ni njia salama, ya haraka, na rahisi kwa wote – wanunuzi na wauzaji. Dhama hii ya kuwezesha wafanyabiashara wa aina zote inaenda sambamba na kusudi letu la ‘Kuwezesha Afrika ya kesho, pamoja, …hatua moja baada ya nyingine’.”
Kwa upande wake, Aron Luhanga, Mkuu wa Kitengo Mawasiliano, Masoko na Mahusiano, alisema suluhisho hili la Absa MobiTap ni moja ya mengi ambayo benki itaendelea kutoa katika ufumbuzi wa malipo ya kidijitali wakati Absa inaendelea kuimarisha nafasi yake kama kinara katika nyanja hiyo hapa nchini.
Alisema, “MobiTap inaruhusu wauzaji kutumia teknolojia ambayo tayari wanayo – simu janja, karibuni kila mfanyabiashara siku hizi ana simu janja. Hata hivyo, mtej wetu akiwa hana simu janja, na anahitaji kujiunga na Absa MobiTap, tutampatia simu bure ili kumfanikisha.”
Kwa mujibu wa Aron, suluhisho hili kimsingi linalenga wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), hasa wale ambao hapo awali walitegemea malipo kwa fedha taslimu au uhamishaji wa kielektroniki (EFT). Wafanyabiashara mbalimbali, kama vile madereva wa Uber/Bolt, migahawa, saluni, maduka ya vifaa, wakulima, wote wanaweza kutumia fursa hii ya uvumbuzi kuwasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Katika hotuba yake ya kuhitimisha, Ndabu, alitoa wito kwa wafanyabiashara wote – wafanyabiashara wa ukubwa wote (wadogo na wa kati) kutumia fursa ya Absa MobiTap kuwezesha biashara zao kupokea malipo ya kadi za benki kwa njia ya haraka, rahisi, na salama zaidi, ili kuwezesha kukuza jamii ya kidijitali, isiyotembea na pesa taslimu kwa faida ya wote.