The House of Favourite Newspapers

Afya ya Harmo, Hofu Yatanda

0

Hofu inazidi kutanda juu ya afya ya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambayo inaelezwa kuwa, yupo hatarini kukumbwa na magonjwa ya hatari, yanayoongoza kwa vifo vya binadamu duniani.

 

TUJIUNGE HAVOC, MASAKI

Hivi karibuni, ndani ya ‘club’ ya starehe ya usiku ya Havoc iliyopo Masaki jijini Dar, Harmonize au Harmo, alikuwa na jambo lake na wasanii wake, ambapo walikuwa wakizindua EP (Extended Play au albam fupi) ya msanii Country Wizzy.

 

Kwenye ‘iventi’ hiyo, ambayo gazeti hili lilihudhuria, Harmo alishuhudiwa akiwa na furaha iliyopitiliza. Furaha hiyo haikupita hivihivi, kwani alionekana akifakamia pombe kali na baadaye alianza kuvuta sigara kama kawaida yake kama gari-moshi, kiasi cha kufunikwa na moshi wa sigara.

 

HABARI HII ILIPOZALIWA

Mmoja wa watu wa karibu wa Harmo aliyeomba hifadhi ya jina gazetini, alizungumza jambo zito juu ya afya ya msanii huyo na hapo ndipo habari hii ilipozaliwa. “Huyu Konde Boy (Harmo) yupo vizuri sana, tena sana…ila kadiri siku zinavyosonga, anazidi kuhatarisha afya yake.

 

“Jamaa amekuwa mvutaji wa sigara sana. Pia amekuwa ni mtumiaji mzuri sana wa pombe, hasa pombe kali. “Na siyo mimi tu ninayeona hatari, lakini watu wake wote wa karibu wanasema moshi (wa sigara) unahatarisha mno afya yake kwa sababu kila siku inaelezwa na mamlaka tofautitofauti ndani na nje ya nchi kwamba, uvutaji wa sigara uliopitiliza, una madhara makubwa kiafya.

HATARI KUBWA

“Lakini hatari kubwa ni kwamba, huu uvutaji wake wa sigara na unywaji wa pombe, vinaweza kumsababisha safari nyingine ya kula unga (madawa ya kulevya). “Kikubwa ninachokiona, ni watu kama ninyi (waandishi) kutumia taaluma yenu kumwambia jamaa, aachane na matumizi ya sigara, kwani siyo sifa kama baadhi ya watu wanavyodhani.

 

“Uvutaji wa sigara siyo suala la kumsingizia, wewe (mwandishi) mwenyewe umemuona anavuta, lakini pia hebu ingia hapo kwenye page (ukurasa) yake ya Instagram, utaona picha zake akivuta sigara na kunywa pombe… “Na mimi nikwambie siri ambayo wengi hawaijui, miongoni mwa mambo yaliyomfanya ajitoe Wasafi, hilo la kuvuta ni mojawapo.

 

MAJIBIZANO NA SALLAM

“Kama utakumbuka kuna kipindi alijibizana na Sallam SK (mmoja wa mameneja wa Lebo ya Wasafi Classic Baby -WCB) juu ya masuala ya kuvuta sigara kubwa (bangi). “Kama viongozi wa Wasafi wakiamua kusema ukweli, basi wanaijua vizuri ishu ya Konde Boy (Harmo) kuwa mvutaji mzuri.

 

USHAURI KWA BASATA

“Mimi nilikuwa ninashauri, hata Basata (Baraza la Sanaa la Taifa), ndiyo wakati wao wa kumsaidia msanii kama huyu kabla hajapata madhara makubwa ya kiafya na siyo kufungia nyimbo zao tu.

 

“Kiukweli inaumiza sana kuona mtu kama Konde Boy (Harmo) anahatarisha afya yake kwa kuvuta kitu kimeandikwa ni hatari kwa afya yake. “Najua ni balozi wa brandi ya sigara, lakini siyo kuzitundika hadi apate madhara ya kiafya,” alimalizia kufunguka mtu huyo wa karibu na lebo ya Harmo ya Konde Gang Music Worldwide.

DAKTARI AMUONYA

Mmoja wa madaktari maarufu jijini Dar, Dk Godfrey Charles ‘Dk Chale’ aliyezungumza na gazeti hili juu ya madhara ya uvutaji wa sigara wa kupitiliza kama unaofanywa na Harmo, alikuwa na haya ya kusema, huku akimuonya staa huyo;

“Uvutaji wa sigara wa kupitiliza kama huo, hudhoofisha kinga ya mwili, hivyo kuwa rahisi mno kushambuliwa na magonjwa hasa ya mfumo wa upumuaji.

 

“Moshi wa sigara huwasha macho na pili kemikali zilizo ndani ya sigara, hupita kwenye mishipa, damu na hatimaye kudhuru macho. Sigara pia husababisha kudhoofika kwa sehemu ya kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona vizuri na hata kutofautisha rangi.

 

“Kemikali zinazopatikana ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha, hivyo basi inaanza kuzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika. Mvutaji wa sigara huonekana mkongwe au aliyezeeka zaidi kuliko umri wake.

 

“Uvutaji wa sigara unasababisha saratani ya ngozi. Kemikali za sigara, husababisha vidonda kwenye ngozi na ambavyo haviponi kwa urahisi. Baada ya muda, hugeuka saratani (kansa).

 

“Sigara hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye meno, hivyo kusababisha kuoza kwa meno, harufu mbaya mdomoni na uchafu wa meno. “Sigara pia hutatiza kupona kwa vidonda, hasa baada ya kung’olewa kwa jino. “Uvutaji wa sigara, ndiyo sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu.

 

Pia husababisha kupasuka kwa vibofu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya mwilini. Wavutaji pia hupata saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa, hivyo inabidi kutobolewa kwa kishimo kwenye shingo, ili kuwezesha mwathiriwa kupumua.

 

“Sigara pia inasababisha mifupa kuwa mepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kuwa kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu.

 

“Sigara hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini vinavyosababisha vidonda tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula. Vidonda vya mvutaji, huwa ni vigumu kutibika na mara nyingi hutokea tena baada ya kupona.

 

”Kutu ya sigara hukusanyika na kuganda kwenye kucha na baina ya vidole vya mvutaji. Kisha hubadilisha rangi ya vidole na kucha kuwa za manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole pia hukauka na kuwa ngumu kwa sababu ya joto na kemikali za sigara.

USHAURI WA BURE

Kwa mtu yeyote ambaye amekuwa mtumwa wa kuvuta sigara, ninamtia moyo kuwa bado hujachelewa sana kuchukua uamuzi wa kuacha kuvuta sigara, kwani atapata manufaa makubwa sana.

 

“Kuacha kuvuta sigara, ni hatua ya mwanzo. Kinachofuata ni kutafuta mtu anayeweza kukusaidia katika kampeni hii binafsi ya kuacha kuvuta sigara, ambaye atakusaidia zaidi kukushauri. “Siku hizi kuna maelfu ya huduma za kusaidia kuacha uvutaji wa sigara. Wahudumu wa afya kwa ujumla, pia tupo mstari wa mbele katika hilo.

 

“Tunakupatia tiba na ushauri pia. Tunaanza kufuatilia hali ya tabia yako ya uvutaji, ndipo tunajua tiba sahihi itakayokufaa, lakini ni baada ya kukufanyia vipimo kujua ni kwa kiasi gani tatizo limekuathiri kimwili na kiakili, kisha mtu anaanza matibabu kwa sababu ni tatizo linalotibika.”

 

HARMO NA UVUTAJI SIGARA

Katika utetezi wake juu ya uvutaji wa bangi, miezi kadhaa iliyopita, Harmo alikanusha jambo hilo huku akikiri na kusisitiza kuwa yeye ni mvutaji mzuri wa sigara, kiasi cha kupewa ubalozi wa sigara juzikati.

“Wakati mwingine tuacheni utani, tuweni serious, mimi nilijiposti na mimoshi ya sigara, tena sigara embassy, hiyo bangi yenyewe naisikia kwenye bomba,” anasema Harmo ambaye ni C.E.O wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide.

Stori Sifael Paul, Risasi

Leave A Reply