The House of Favourite Newspapers

Ahukumiwa Jela kwa Kuishi Nchini Bila Kibali

0

RAIA wa Nchini Yemen, Edhah Nahdy (34) amehukumiwa kulipa faini ya Sh 1,400,000 au kwenda jela mwaka mmoja na miezi nane baada ya kutiwa hatiani kwa makosa manne likiwemo la kuishi nchini bila kibali.

 

Hukumu hiyo ilitolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar-es-saalam na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi mbele ya Wakili wa Serikali, Shija Sitta.

 

Mshitakiwa huyo amehukumiwa baada ya kukiri kutenda makosa manne ambayo ni kumdanganya Ofisa wa Uhamiaji kwa kujifanya yeye ni raia wa Tanzania, kutoa nyaraka za uongo kwa maana ya kitambulisho cha uraia cha Tanzania (kitambulisho cha NIDA), kukutwa ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na cheti cha kuzaliwa ili aweze kujipatia cheti cha kusafiria.

 

Wakili Sitta amedai, mshitakiwa huyo alitenda kosa la kukutwa ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Januari 19, 2021 katika ofisi za makao makuu jijini Dar-es-Saalam.

 

“kwakuwa mtuhumiwa amekubali mashtaka yake, Mahakama inamuhukumu kulipa faini ya laki Tano kwa kila kosa (la Kwanza na la nne )au kwenda jela mwaka mmoja lakini pia kwa kosa (la pili na la tatu )atalipa faini ya laki mbili kwa kila kosa au jela miezi 8” amedai Hakimu Shaidi.

 

Mshitakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini hivyo kuepuka kwenda Segerea kwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi nane.

Leave A Reply