The House of Favourite Newspapers

ALIYEIBA MAHINDI YAKANG’ANG’ANIA MABEGANI, ZIPU YAMUOKOA

PWANI: Frank Joseph (23) mkazi wa Dar es Salaam ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kuiba kilo 20 za mahindi, jana aliwaambia waandishi wa habari jinsi kitendo cha kufunguliwa zipu ya suruali yake kilivyomtua mzigo ambao ulimganda kichwani kwa saa kadhaa baada ya kuuiba mkoani kwa mama mmoja maeneo ya Mlandizi.

 

Kwa mujibu wa mtuhumiwa huyo, mzigo huo wa mahindi yaliyokuwa kwenye kiroba aliuiba Mtaa wa Nyambwiro, Mlandizi wilayani Kibaha majira ya saa 7.00 usiku wa kuamkia jana na kwamba haukumtoka kichwani mpaka saa 12 asubuhi ya jana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kasema kuwa taarifa walizipata kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa  Nyambwiro, Ally Mwabilo, kabla ya kufika eneo la tukio na kumuokoa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa hatarini kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali.

 

Shana alisema askari wake walimchukua mtuhumiwa ambaye aliwaonyesha alikochukua mzigo huo, lakini mwenye nyumba, ambaye jina lake hakutaka kulitaja, hakuwapo muda huo. Mtuhumiwa alipelekwa kituoni akiwa na mzigo kichwani wakati harakati za kumpata mwenye mali zikiendelea.

Mmiliki wa mzigo huo alipofika kituo cha polisi Mlandizi alionana na mtuhumiwa huyo na kumfungua zipu ya suruali na kuongea maeneo fulani (ambayo hata polisi hawakuyaelewa) kisha mtuhumiwa alipoambiwa ashushe mzigo, ulitoka kichwani.

 

Aidha, Kamanda huyo aliwaonya vijana kuacha kuvuna vitu ambavyo hawakupanda na badala yake wajishughulishe kupata mali kwa jasho lao.

VIDEO: Aiba Mahindi, Gunia Laganda Mabegani!

 

Joseph alikiri mbele ya waandishi wa habari kuiba mzigo huo na kwamba uligoma kutoka kichwani hadi mwenye mali alipofungua zipu ya suruali yake na kupata wepesi wa kuushusha mzigo huo.

 

“Nilikua napita nikaona mzigo upo nje,” alisema Joseph ambaye ni mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam. “Nikaubeba. Nilivyokua naushusha haukutoka kichwani, ulivyogoma kutoka nikaamua kurudi kwa mwenyewe (lakini) sikumkuta hadi nilipomuona kituo cha polisi. Alivyofungua zipu ya suruali yangu na kuongea maneno yake, (ghalfa) nikaweza kuushusha mzigo,” alisema Frank.

 

Frank ambaye alidai anafanya kazi ya kusukuma mkokoteni aliwashauri vijana kuacha tamaa na kufanya kazi zao kwa bidii.Aidha, alisema hawezi kurudia tena kuiba baada ya tukio hilo.

Aliyeng’ang’aniwa na Mahindi ya Wizi! RPC Kafafanua

Comments are closed.