The House of Favourite Newspapers

Athari za Chakula Alacho Mjamzito kwa Mtoto

0

WATAALAMU wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitaji ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, mwili wako unahitaji virutubisho ili kusaidia ukuaji wa mwili, kama ni kijana mwili wako una mahitaji maalumu unayoyahitaji kudhamini makuzi ya kiafya ya mwili wako wakati wa utu uzima na wakati unapokuwa mtu mzima unahitaji kuwa na uzito uliolingana na mwili wa wastani.

Tukiangalia katika upande wa wajawazito na wale wanaonyonyesha nao pia wana vyakula vyao maalumu wanavyohitajia tofauti kabisa na wanawake wengine. Uchunguzi wa kitiba uliofanywa unaonyesha kuwa, hali ya kiafya ya mama mjamzito huwa na athari mbalimbali kwa mtoto atakayezaliwa.

Vilevile kuna ushahidi mkubwa kuwa magonjwa sugu ya watu wazima huanzia wakati mtoto bado akiwa tumboni mwa mama yake akiwa katika hali ya kiluilui au (foetus). Kwa hivyo akina mama wajawazito wanashauriwa kuzingatia vyakula wanavyokula kabla na baada ya kushika mimba.

Tuangalie athari za chakula kwa afya ya mtoto na virutubisho vinavyopaswa kujumuishwa katika mlo wa mama mjamzito. Chakula cha mjamzito kinaweza kuwa na athari kubwa muhimu kwa afya ya watoto kwa miaka mingi baada ya kuzaliwa.

Miaka kadhaa ya hivi karibuni, Jarida la Masuala ya Lishe la Uingereza la Prestigious lilichapisha makala

 tatu kuhusu athari za lishe ya mama mjamzito kwa afya na ukuaji wa kiakili wa mtoto ambaye bado hajazaliwa.

Wengi wanafahamu kuwa akina mama wajawazito wanapaswa kula chakula chenye virutubisho vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha kuwa watoto wao watakaowazaa wamerutubika vya kutosha wakati wakiwa kwenye mfuko wa uzazi. Hata hivyo, kile ambacho hatukubaliani nacho hivi sasa ni kwamba chakula cha mama mwenye mimba kinaweza kuwa na taathira chanya kwa afya ya watoto kwa muda wa miaka mingi, baada ya kuzaliwa.

Hivi sasa imethibitika kuwa kile kinacholiwa na akina mama wakati wa ujauzito, chakula ambacho kitakuwa kimejumuisha virutubisho vyote vinavyotakiwa, kinaweza kuwafanya watoto wao watakaozaliwa kuwa werevu zaidi. Kwani wataalamu wa afya wanasema kuwa hivi sasa wanaweza kuandaa kizazi kipya cha watoto werevu kwa kula chakula kinachotakikana wakati wa ujauzito.

Akina mama wajawazito ambao katika kipindi cha ujauzito hawakupata lishe bora isiyo na mada za protini, nishati, madini na

 vitamini kwa jumla huzaa watoto walio na uzito wa chini. Aidha, watoto hao huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na magonjwa ya kisukari katika kipindi cha utu uzima.

Baada ya kufahamu umuhimu wa kula lishe bora kwa mama mjamzito na athari zake chanya kwa mtoto atakayezaliwa, sasa tuangalie hatari ya unywaji pombe kwa akina mama wajawazito. Watu wengi wanafahamu madhara yanayotokana na utumiaji wa madawa ya kulevya na ya kawaida pamoja na uvutaji sigara wakati wa ujauzito, lakini wanawake wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu madhara yanayosababishwa na unywaji pombe wakati wa ujauzito.

Utasikia mume au ndugu, jamaa na marafiki wakimshawishi mama mjamzito kwa maneno kama vile” hebu pata pombe chupa moja, itakuburidisha, kunywa mvinyo kidogo tusherehekee mimba yako. Chupa moja haiwezi kukuathiri bali itakusisimua tu,” n.k.

Nadhani wengi tumewahi kusikia maneno kama haya na ushauri usiofaa ambao hauna faida yoyote bali huleta madhara kwa mtoto atakayezaliwa.

Unywaji pombe wa aina zozote wakati mama akiwa na mimba huwa na madhara tofauti kwa mtoto aliye tumboni mwake, kuanzia zile za wastani hadi kubwa. Kumbuka kuwa mama anapokunywa pombe mtoto naye hunywa pia.

Kuna madhara makuu matatu yanayoweza kumsibu mtoto ambaye bado hajazaliwa iwapo mama yake alikuwa akinywa pombe wakati wa ujauzito. Mosi, ni kuweko hatari kubwa ya kutoka mimba au kuzaliwa mtoto kabla ya miezi tisa, pili, chembe za mwili za mtoto aliye tumboni zinaweza kuathiriwa au anaweza kuwa na uzito mdogo na kuzaliwa akiwa na ulemavu zaidi ya mmoja, tatu, chembe za ubongo wa mtoto huyo zinaweza kuharibiwa na pombe na mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ambayo kitaalamu hujulikana kama Foetal Alcohol Syndrome.

Miongoni mwa madhara yanayoweza kumpata mtoto ni kama vile kuzaliwa akiwa na ulemavu wa kimwili na kiakili. Kwa upande wa kimwili, mtoto huweza kuathiriwa na mtindio wa ubongo (au brain retardation), mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo sana na uso wake kuwa na mwanya mkubwa baina ya pua na mdomo. Kwa upande wa macho, wengine huzaliwa wakiwa na matatizo ya kuona, masikio hushambuliwa na baadhi ya magonjwa, n.k.

Kwa hiyo ni jambo lenye umuhimu kwa akina mama kuwaandalia watoto wetu mwanzo mzuri wa makuzi bora tangu wakiwa tumboni.  

MAKALA KUTOKA GAZETI LA UWAZI

(Jinsi ulivyo inatokana na unachokula)

www.globalpublishers.co.tz

+255 768 215 956

 

Darassa Afanya Makamuzi Ya Kihistoria Dar Live (Pichaz na Video)

Leave A Reply