The House of Favourite Newspapers

Bongo Fleva ni Utambulisho wa Utamaduni wa Tanzania

0

MJADALA mkali unaendelea. Ni juu ya ama wasanii wa Tanzania waendelee kuiga midundo ya muziki wa nje kama walivyofanya kwa Amapiano au wabaki kwenye muziki wao mtambo wa Bongo Fleva.

Kila mmoja ana mtazamo wake, lakini hebu niwakumbushe msingi wa Bongo Fleva ambao unachukuliwa kuwa na asili ya Tanzania.

Tunakumbuka Bendi ya Mawingu miaka ya 90 na wengine kama Mr II au Sugu, Kwanza Unit, Hard Blasters na Profesa J, Wagumu Weusi, Sostenes Amabakisye au Sos B na wengine wengi wanachukuliwa kuwa waanzilishi wa Bongo Fleva.

Muziki huu haukupokelewa kwa shangwe na Watanzania hasa wazee; ulionekana kuwa ni kihuni.

Haikutegemewa kuwa Bongo Fleva ingeishi kwa muda mrefu, lakini kwa sasa imekua na kila mtu anaweza kuona. Imepitia katika hatua kadhaa za mabadiliko na sasa ina wapenzi wengi tena wa rika zote wakiwemo hata wazee.

Bongo Fleva inapendwa na watu hata nje ya mipaka ya Tanzania. Kenya, Burundi, Rwanda na hata Marekani na Uingereza. Hii ni fursa ya kujitangaza na kuutangaza utamaduni wa Tanzania na Afrika.

Serikali kupitia wizara husika iweke mikakati katika kukuza na kuendeleza Bongo Fleva kwa kuweka mazingira mazuri kwa vijana kujiajiri na kupata maendeleo binafsi na kwa Taifa kwa jumla.

Serikali kupitia vyombo vyake kama Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuweza kusimamia haki za wasanii.

Pia kuwekwa masharti katika utengenezaji wa nyimbo kama vile kutotumia lugha za matusi na kutumia Kiswahili ambacho ni fasaha. Kwani hii ni fursa ya kukuza utamaduni kupitia lugha ya Kiswahili.

Diamond Platnumz ni mmoja wa wasanii wa Bongo Fleva anayejulikana zaidi hadi nje ya mipaka ya Tanzania akitumia slogan yake ya Swahili Nation.

Kiba ana kipaji kikubwa cha kuimba na amechangia kuendeleza Bongo Fleva. Ameshirikishwa na wasanii wakubwa wa nje.

Muziki huu uweke vitu kadhaa ambavyo vitabeba utambulisho wa kitaifa na Serikali pamoja na kusimamia haki zao, lakini wahakikishe kuna wasanii wanafuata taratibu za msingi katika kuandaa nyimbo zao.

Japo ala za Bongo Fleva nyingi zinatengenezwa katika kompyuta na siyo upigaji wa vyombo moja kwa moja, lakini iwekwe midundo ya Kitanzania kama marimba ya Kimakonde na filimbi. Midundo ya ngoma kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania isikike kwenye Bongo Fleva.

Kuwekwe vibwagizo vya sauti za kiasili, hata ikiwa sehemu ndogo tu ya muziki huo.

Kumbuka mwanamuziki maarufu wa Pop duniani, marehemu Michael Jackson aliimba kwa Kiswahili japo sentensi moja tu kwenye wimbo wake wa Liberian Girl yakisikika maneno kama ‘nakupenda pia, nakutaka pia..’ japo wimbo huo ulikuwa wa Kingereza. Vibwagizo vya aina hii vinaweza vikachanganywa katika muziki wa Bongo Fleva.

Nyimbo nyingi sasa hivi zinaendana na utengenezaji wa video hivyo mandhari ya kutengeneza video hizo yaakisi utamaduni wa Kitanzania. Mavazi ni kitu muhimu kwani ni mojawapo ya nguzo kuu ya kutambulisha utamaduni.

Ni vyema kufahamu kuwa wasanii wanapokwenda kuimba nje kama Ulaya na Marekani, watu wa kule wanapenda kuona Afrika au Tanzania inafanana vipi? Hivyo uvaaji wao na lugha ni vitu muhimu kuzingatiwa.

Kazi za wasanii wetu zifuate kanuni za muziki, uumbaji wa maneno na mashairi yake. Vina na mizani ni mojawapo katika vitu vya kuzingatiwa ili kutengeneza kazi yenye ufanisi wa kisanaa.

Ujumbe katika nyimbo pia uzingatiwe ili kuweza kuvutia watu wa rika zote na wenye mitazamo tofauti juu ya maisha.

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO

Leave A Reply