The House of Favourite Newspapers

CAG Abaini Madudu CUF, CCM, Amkabidhi JPM – Video

0

 

CHAMA cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), vinatajwa kwa matumizi mabaya ya fedha katika Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika Mwaka wa Fedha 2018/19.

 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere,  ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Machi 2020, jijini Dodoma, wakati akimkabidhi Rais John Magufuli ripoti hiyo.

 

Kichere amesema, ukaguzi huo umebaini kwamba CUF ilihamisha fedha za ruzuku kiasi cha Sh. 300 milioni kati ya Sh. 366.38 milioni, kutoka kwenye akaunti yake ya benki kwenda katika akaunti binafsi ya mwanachama wa chama hicho, kinyume cha sheria.

 

Pia, amesema CUF haikuwasilisha nyaraka za matumizi za fedha hizo kwake, kwa ajili ya kuzifanyia ukaguzi.

 

“Ukaguzi wa vyama vya siasa, nilibaini CUF kilipokea ruzuku kutoka serikalini kiasi cha Mil. 366.38 lakini chama hicho kilihamisha mil 300 kutoka akaunti ya chama na kwenda katika akaunti binafsi ya mwanachama.

 

“Mil 66 zilitolewa kama fedha tasilimu, hata hivyo nyaraka za matumizi za fedha hizo hazikuwasilishwa kwangu kwa ajili ya ukaguzi. Pia, nilibaini mil 47 zilitolewa katika akaunti ya benki ya chama, pasipo idhini ya katibu mkuu wa chama, “ameeleza Kichere.

 

Pia ameeleza, CCM kupitia jumuiya yake ya wazazi ilifanya matumizi yasiyokuwa na tija kwa kumfidia mpangaji hasara ya kiasi cha Sh. 60 milioni, baada ya kukiuka masharti ya mkataba wa upangishaji.

 

“Matumizi yasiyokuwa na tija ya kumfidia mpangaji pasipo kufuata taratibu, kiasi cha Sh. mil 60 jumuiya ya wazazi ilitoa baada ya kumuondoa mpangaji bila kufuata utaratibu na mpangaji kuonyesha nia ya kufungua kesi ya madai. Jumuiya hiyo ililazimika kulipa fidia ya hasara baada ya mazungumzo nje ya mahakama,” amesema Kichere.

 

Katika hatua nyingine, Kichere amesema ukaguzi wake, alibaini vyama vya siasa vinne vilipata hati isiyoridhisha na 11 vilipata hati mbaya.

 

Leave A Reply