The House of Favourite Newspapers

Unaposhindwa kuishi vizuri na watu, unajiamini kwa lipi?-2

0

Wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia umuhimu wa kila mmoja wetu kujitahidi kuishi vizuri na watu wanaomzunguka. Kwamba kama uko ofisini, ishi vizuri na wafanyakazi wenzako. Kama ni nyumbani, ishi vizuri na wapangaji na majirani zako, kama uko chuoni pia ishi vizuri na wanafunzi wenzako.

Nalazimika kusema hayo kwa kuwa najua faida za kuishi vizuri na watu wanaokuzunguka hasa linapokuja suala la kwamba upo kwenye wakati mgumu na unahitaji msaada.

Unachotakiwa kujua ni kwamba, maisha yanabadilika sana! Unaweza kulala tajiri na ukaamka maskini, au kinyume chake. Lakini pia kaa ukijua kwamba, uwezo wa mali na fedha haviwezi kukufanya ukawa na furaha iliyokamilika kama hutakuwa unapata upendo kutoka kwa watu wanaokuzunguka.

Ndiyo maana inashauriwa kwamba, kwa hali yoyote uliyonayo jaribu kuwapenda watu ambao wako karibu yako. Usijisikie na kujiona wewe ndiyo wewe eti kwa sababu huna shida ndogondogo leo.

Mpenzi msomaji wangu, huko mtaani wapo watu ambao hujisahau pale wanapokuwa na vijisenti. Maringo, dharau na tabia nyingine zinazochukiza inakuwa sehemu ya maisha yao bila kujua kuna uwezekano pesa hizo zikayeyuka.
Lakini mtu huyohuyo ambaye leo anajiona kakamilika siku ikitokea kaishiwa utamuonea huruma, si ajabu hata akapatwa na homa kutokana na hofu ya kwamba hatapata mtu wa kumsaidia kwani hana uhusiano mzuri na wengine.

Kwa maana hiyo usipojitahidi kuishi vizuri na watu, utakuja kupata wakati mgumu sana siku utakapokuwa umechalala.
Sasa ufanyeje pale unapokuwa umeishiwa? Unapokuwa kwenye hali hiyo kwanza chukulia ni hali ya kawaida na amini unaweza kuendelea kuishi.
Usilalamike sana hadi kumfanya kila mtu akajua kwamba umeishiwa. Nasema hivyo kwa sababu wapo baadhi ya watu wakiwa wameishiwa utawajua tu. Wengine hujikuta wenye huzuni na kupoteza furaha waliyokuwa nayo.

Cha kufanya ukiwa katika hali hiyo ni kuwa muwazi kwa watu wako wa karibu. Kama umeishiwa, huna hata nauli, usitembee kwa miguu wakati yupo mtu ambaye anaweza kukusaidia katika hilo. Kama huna pesa ya kula wala usishinde njaa, mshirikishe mtu wako wa karibu, naamini atakutatulia tatizo.

Hata hivyo, msaada huo utaupata tu ikiwa umejijengea sifa nzuri kwa watu wanaokuzunguka. Ukiona mtu ana shida lakini kila anayemkimbilia anagonga mwamba, huyo siyo mtu wa watu! Wewe jitahidi kuwa mtu wa watu.

Leave A Reply