Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-13

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:

Siku za baba Shua kukaa Arusha zilibaki mbili, lakini akarudi nyumbani kwake Dar bila kuzimaliza. Alifika saa kumi na mbili na nusu jioni na kukuta mkewe yuko bafuni anaoga, akachukua simu yake na kukaa sebuleni akaanza kupekua meseji moja baada ya nyingine.

SHUKA NAYO SASA…

Meseji ya kwanza ilikuwa ya mama Shua kwenda kwa Musa, iliandikwa hivi…

“Vipi leo, nahisi kama kuna ulazima. Au wewe unasemaje? Nakusikiliza.”

Akafungua majibu ya Musa huku moyoni akisema…

”Huyu Musa huyu…si ndiyo huyu kijana mgeni aliyehamia humu ndani?”

Mara, mkewe akatokea. Alipomwona mumewe ameshika simu yake na anajua mna meseji za Musa, mwanamke huyo huku akiwa amejifunga kanga moja tu, aliruka kama chui na kufika kwenye mwili wa mume wake…

“Baba Shua nini bwana unasoma meseji zangu?” alisema mama Shua lakini aliikosa simu yake kwani baba Shua aliinua mkono juu zaidi na kumfanya mkewe huyo kuangukia mapajani mwake…

“Una siri gani humu kwenye simu mpaka unanikataza kuangalia? Kwanza umeanza lini?”

Mama Shua alikosa jibu, lakini akabaki hapohapo kwenye mapaja ya mumewe akizuia mumewe asisome meseji zake…

“Sasa nahisi unataka kupigwa ndiyo unijue mimi ni nani!” alisema baba Shua, mama Shua akaogopa lakini hakumruhusu mumewe kusoma meseji zake.

Kitendo hicho kilimfanya baba Shua kuzidi kuhisi vibaya kwani kama kweli mkewe angekuwa mwema kwenye simu hiyo asingetumia nguvu vile kumzuia asisome meseji…

“Na kwa taarifa yako nimeshaona meseji ya Musa,” alisema mwanaume huyo.

Mama Shua akazidi kuogopa, akaweweseka ile mbaya huku akisema…

“Mimi sina uhusiano naye mbaya. Labda mawazo yako tu.”

“Kama mawazo yangu acha nione meseji nyingine…”

“Sitaki na simu yangu, kwani mi nimesoma meseji zako?”

Ilibidi baba Shua atumie nguvu ya ziada kumchomoa mkewe kwenye mapaja yake, akaanguka chini lakini na  yeye simu ikaanguka chini, mkewe akaidaka na kukimbilia chumbani.

Kule chumbani, mama Shua alizifuta meseji zote kisha akamtumia meseji moja Musa…

“Kimenuka, usitume meseji wala kupiga simu mpaka nitakapoanza mimi.”

Akaifuta meseji hiyo na kutoka na simu…

“Eee, simu hiyo angalia kama kuna kitu,” mama Shua alimwambia mume wake…

“Hivi wewe kumbe siku zote ulijua unaishi na mwanaume asiyekuwa na akili siyo? Unaweza kunichezea akili mimi?”

Mama Shua alimwona mume wake amabadilika rangi, akatambua upuuzi wake.

Baba Shua alisimama, akaenda kumgongea mlango Musa…

“Dogo!”

“Naam.”

“Toka nje.”

“Mh! Kweli kimenuka,” alisema moyoni Musa huku akitoka. Moyo ulikuwa ukimdunda sana…

“Oya! We unachati na mke wangu siyo?”

“Mimi bro?”

“Si ndiye ninayeongea naye hapa. Sasa unaniulizaje mimi bro?”

“Mwite athibitishe.”

Mama Shua aliposikia Musa anaruka kimanga na anataka aitwe athibitishe, aliifuta namba ya Musa kwenye simu kisha akaibadili namba ya mfanyakazi mwenzake anayeitwa Xsaver kuwa Musa.

Alitoka mwenyewe bila kuitwa…

“Baba Shua si nimekukatalia pale kwamba sina uhusiano na huyu kijana. Mbona unanilazimisha?”

“Unataka kuniambia huna namba yake ya simu?”

“Sina.”

“Lete simu yako.”

Baba Shua alisachi jina la Musa kwenye simu, likatokea, akaipiga ile namba akiwa ameiweka simu sikioni. Iliita lakini si ya Musa yule japo yeye aliishika simu yake…

“Niambie dada angu?” upande wa pili wa simu ulisikika ukisema, baba Shua akakata simu na kumrudishia mke wake…

“Sawa, lakini nitaendelea kuchunguza,” alisema akirudi ndani. Mama Shua naye akarudi ndani, pia Musa.

Sasa ikawa, Musa ana namba ya mama Shua lakini mama Shua hana.

Siku hiyo ilipita, ikafuata siku nyingine. Asubuhi Musa alikwenda kuoga, akamkuta mama Shua na msichana wake wa kazi wako uani. Alisalimia, akaingia bafuni kuoga. Alipotoka, alimkuta baba Shua na mtoto Shua nao wapo uani. Musa akamsalimia baba Shua kisha akamwinamia Shua…

“Mchumba…mchumba…hujambo?”

“Mwambie sijambo,” alisema mama Shua akimfundisha mtoto wake…

“Sijambo…”

“Sasa leo vipi, tutakutana saa ngapi tukale raha mchumba?” alisema Musa akiwa bado amemwinamia Shua…

“Mwambie wewe tu ukitoka kazini unitafute.”

“Tafute mimi,” alisema Shua akiwa amekosea lakini ujumbe ulifika…

“Sasa tatizo wewe mchumba huna simu…”

“Mwambie wewe si unayo unipigie ukitoka kazini.”

Muda wote huo, baba Shua yeye alikuwa akicheka jinsi mwanaye anavyojibu…

“Piga wewe… kazini,” alisema Shua kwa kukatakata maneno.

“Haya nitakupigia ujiandae.”

“Mwambie usiwe na wasiwasi mchumba.”

“Wasiwasi …chumba,” alisema Shua akiuma kidole kimoja cha mkono.

Musa alijiandaa akaondoka zake. Mama Shua naye alijiandaa akaondoka zake. Lakini alijitahidi sana kutafuta namna ya kuwasiliana na Musa mchana akashindwa. Musa naye alihisi kumtafuta mwanamke huyo kwa simu kunaweza kuleta kizaazaa baadaye kwa mume wake. Akaogopa.

***

Giza likiwa limeshaingia, Musa anarudi sasa, akakutana na

mama Shua njiani…

“Musa vipi? We unajua namba yako sina, kwa nini usinitafute wakati we unayo? Kwani ule ujumbe wangu asubuhi kupitia kwa mtoto hukuulewa?”

Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG


Loading...

Toa comment