The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-26

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Alifika nyumbani akiwa amechoka sana kiakili na mwili. Aliwaza namna ya kuwasiliana na mama yake na kumweleza matatizo yake lakini moyo ulisita. Alijua ataamsha hasira za mama huyo.Alimwangalia mtoto wake, Shua. Akamhurumia sana huku akitingisha kichwa.
***
Saa sita mchana, Musa alimtumia meseji mama Shua…
“Upo?”JIACHIE MWENYEWE SASA…

Mama Shua alipoisoma meseji hiyo alisonya kwa nguvu kiasi kwamba, kama nyumba ya tatu kulikuwa na mtu muda huo angesikia…
“Huyu kijana mjinga sana. Yaani anadhani mimi niko poa? Kwani ye hajaona yaliyotokea?” alijiuliza moyoni mama Shua.

Musa alipoona meseji haijajibiwa, aliamua kupiga. Simu yake iliita mpaka ikakatika…
“Khaa! Huyu mbona hapokei simu?” alijiuliza Musa, akapiga tena. Safari hii, mama Shua aliamua kupokea huku uso ameukunja vibaya sana…
“Haloo…”

“Baby, mbona hupokei simu yangu jamani? Unajua nimekuandalia zawadi gani lakini?”
Uso wa mama Shua ulianza kukunjuka kwa mbali sana…
“Ah! Samahani sana jamani baby, nilikuwa mbali na simu…enhe! Zawadi gani hiyo my darling?”
“Ni ‘sapraizi’…”

“Jamani baby wa mimi si uniambie tu…”
“Tukikutana nitakuonesha achilia mbali kukwambia…”
“Da! Lini sasa tutakutana..?”
“Wewe tu…”
“Basi iwe leo jioni…”
“Wapi?”

“Panga wewe ila isiwe kule kwa siku zote maana kuna mzee mmoja wa kijijini ni mnoko vibaya sana…”
“Nyumbani kwako lakini kukoje?”
“Wapi?”

“Kwa wewe na mume wako…hajamaindi ile ishu?”
“Wee hayo yaache Musa bwana…nitakwambia kitu siku nyingine lakini… ila hali si nzuri kivile.”
Walizungumza, wakapanga kukutana maeneo mengine jioni ya siku hiyo ambapo mama Shua angetokea nyumbani na si kazini kwani hakwenda kazini.
***
Maua, muda mwingi aliutumia kuchati na baba Shua kwa kumtumia meseji mbalimbali za mahaba na kumpa pole kwa kazi. Pia kumsifia kwamba yeye ni mchapakazi hodari.
Ilipofika mchana wa saa saba, Maua alimtumia meseji baba Shua ya kumuulizia kuhusu chakula…
“Baby lanchi.”
Kwa baba Shua lilikuwa jambo geni na jipya pia. Hakuwahi kuwaza kwamba, Maua anaweza kurejesha mapenzi ya dhati kiasi hicho. Alijisikia furaha moyoni, ilimsaidia pia kumsahau mama Shua na tabia zake.
***
Saa kumi na moja, baba Shua alikuwa ndani ya gari akielekea Kinondoni kwa rafiki yake anayeitwa Jome.
Alipofika kwa Jome, akashtuka sana Jome…
“Ee bwana vipi?” aliuliza Jome.
“Poa, vipi kwani?”

“Mbona nimemwona shem mahali…”
“Wapi?”
“Pale Hoteli ya Bwawani One…”
“Na nani?”

“Ah! Sina hakika lakini wewe ni mwanaume utakuwa unajua namaanisha nini!”
“We niambie tu, umemwona na nani?”
“Na dogo mmoja hivi…”
“Namjua…”

“Ah! Kwa hiyo unajua kila kitu kuhusu shemeji?”
“Najua.”
“He! Ee bwana…kwani kuna nini?”
“Kaka…mama Shua si yule tena…mama Shua kadanganyika na huyo dogo uliyemwona naye…nilitaka kuchukua hatua kali, lakini nimeona nimwache yeye na maisha hayo na mimi niwe na maisha mengine, naamini itanisaidia…”

“Da! Kwani yule dogo unamjua?”
“Nini kumjua Jome, naishi naye nyumba moja. Nikienda chooni napita mlangoni kwake.”
“We Benny…kweli?”
“Kweli Jome…”
“Ah! Ina maana nafuu na Maua?”
“Ndiyo niko naye sasa…”
“Ha! Kweli kaka?”

“Kweli Jome.”
Basi, baada ya hapo walizungumza mambo mengi mpaka ikafika hatua wakaagana. Jome alimsindikiza baba Shua nje mpaka kwenye gari…
“Ha! Benny, una usafiri mara hii?”
“Wa Maua…”

“Heee! Maua huyuhuyu Maua shemeji yangu wa kitambo?”
“Huyohuyo bwana…amekuja kwa kasi sana.”
“Safi sana…safi sana…sasa Maua ndiye mke,” alisema Jome…

“Kaka ni kweli. Nimekwenda hadi kwake. Kaniingiza ndani kasema hakuna mwanaume aliyewahi kuingia. kanitambulisha mpaka kwa majirani zake kwamba mimi ndiye mchumba wake nilikuwa nje ya nchi kimasomo.”
Hapo, baba Shua na Jome walisimama nje kwenye gari wakizungumza…
“Inaelekea wapi sasa?” aliuliza Jome…

“Home kwanza, halafu Kimara kurudisha gari la Maua…”
“Nipe lifti, niache hapo mbele tu,” alisema Jome, wakaingia garini wote.
Baba Shua alipita barabara ileile yenye Hoteli ya Bwawani One, akaliona gari la Musa…
***
“Yaani baby nimeshukuru sana kwa zawadi. Bonge la gauni, kama ulinipima vile,” alisema mama Shua akimwambia Musa huku wakiwa wamekaa kwenye baa ya Hoteli ya Bwawani One wakinywa juisi kwanza kabla ya kuzama chumbani kwa ajili ya majomboz…
***
“Jome ndiyo hoteli hii ulipomwona mama Shua?” aliuliza baba Shua…
“Hapahapa…tena wale pale wamekaa. Hebu ingia na sisi tukakae tuone,” alishauri Jome, baba Shua akaingiza gari kwenye maegesho ya hoteli hiyo na kupaki sanjari na gari la Musa, wakashuka wote.

Itaendelea kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.

Leave A Reply