The House of Favourite Newspapers

Country Boy Amefuata Nyayo za Rich Mavoko

0

WATU huigana, ndivyo unavyoweza kusema. Msanii wa Bongo Fleva kutoka Konde Music Worldwide ya Rajabu Abdul Kahali almaarufu Harmonize katika harakati za kuhakikisha lebo yake hiyo inakua na kuleta ushindani wenye tija katika tasnia ya muziki, Septemba, 2020 alimsaini Country Boy akamuingiza Konde Gang.

Wakati inamsainisha Country Boy, lebo hiyo ilikuwa tayari ina wasanii wengine machachari kama Ibraah, Angella, Cheed na Killy waliotoka Kings Music ya King Kiba na Young Skales msanii wa Nigeria.

Hata hivyo, Januari, 2021, Konde Music wakatangaza kuachana na Country Boy kwa madai mkataba wake umemalizika na wamefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kutoendelea kufanya kazi.

Ukweli ni kwamba Country Boy alisaini Konde Music tayari akiwa msanii mkubwa ambaye amekuwepo kwenye muziki muda mrefu kabla ya hata ya Harmonize hajatoka kimuziki.

Msanii Country Boy amesema msanii ni lazima ajitengezee mazingira ya upekee kwa sababu hiyo ndio biashara yake.

Rapa huyo anasema kitu hicho kimemfanya baadhi ya wasanii kuogopa kufanya naye ngoma kutokana na kiwango ambacho amekiweka katika muziki wake.

“Ukiwa msanii ni lazima uwe na value yako, usiwe tu wa kawaida, hiyo ndiyo biashara siku zote. Ninavyojiweka na mazingira ambayo nimetengeneza ni mazuri na kunifanya niweze kuogopeka hata ukija unakuja na kazi bora.

“Hata muziki wangu nauchukulia serious zaidi, kila ninachokifanya lazima niw kiogope na nikiheshimu, sijichukulii poa,” anasisitiza jamaa huyo.

Country Boy kwa sasa anafanya vizuri na ngoma kadhaa ikiwemo ya Mwaaa aliyoshirikiana na Moni ambapo kwa pamoja sasa wanaunda Kundi la MoCo.

Tukio hilo linafafanishwa na la lile la Diamond pale alipomsaini Rich Mavoko ndani ya WCB Wasafi Juni, 2016 akiungana na wasanii wengine wa lebo hiyo kwa wakati huo kama Harmonize, Rayvanny na Queen Darleen.

Julai, 2018, Rich Mavoko aliamua kuondoka katika lebo hiyo kwa mvutano mkali na mabosi wake hao hadi kufikishana Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa ajili ya usuluhishi.

Katika historia, Mavoko ni msanii wa kwanza kuondoka katika lebo hiyo kama ilivyo kwa Country Boy alivyoondoka kwenye Lebo ya Konde Music.

Rich Mavoko kabla ya kusaini WCB tayari alikuwa ni msanii mkubwa hadi kufikia hatua ya kushindanishwa na Diamond.

Rich Mavoko ambaye alijiunga na WCB mwaka 2016 akiwa msanii wa tatu kusaini na lebo hiyo baada ya Harmonize na Rayvanny, ngoma zake sasa zinavuma kinoma na huko kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati Richard Martin almaarufu Rich Mavoko akijiunga na WCB ambako amefanya kazi kibao zikiwemo kolabo matata kama ya Zilipendwa ambayo ilibamba kinoma, mashabiki wengi walipigwa butwaa na wengine wakihoji uamuzi wake huo, wakisema amebugi kinoma.

Hata hivyo, wengine walipongeza wakisema kuwa amekwenda kujiunga na lebo yenye wasanii wanaojitambua na wanaoamini katika kufanya kazi, hata hivyo staili yake ya uimbaji ilielezwa kuwa ni tatizo kwani inafanana kabisa na ya Diamond (bosi wa WCB) na hata Harmonize kwa mbali. Hata unaposikiliza ngoma ya Show Me ambayo ni kolabo yake na Harmonize ni ngumu kuwatofautisha sauti zao.

Wasanii wa WCB wamekuwa na kawaida ya kushirikiana kama siafu pindi wanapokuwa na jambo lao ambapo wamekuwa wakivamia kwenye mitandao ya kijamii kutangaza kazi za msanii mwenzao, jambo ambalo limekuwa likiwapa mafanikio makubwa.

Baada ya kuhama alitengeneza ngoma iitwayo Happy ambayo ulifanyiwa kazi studio za S2Kizzy na siyo Wasafi Records.

Kabla ya kuanzisha Konde Music, Harmonize alikuwa chini ya WCB ya Diamond iliyomtoa kimuziki mwaka 2015 akiwa ni msanii wa kwanza kusainiwa.

Baada ya kuondoka WCB, Oktoba 2019 ndipo Harmonize alipotangaza kuzaliwa kwa Konde Music huku Ibraah akiwa msanii wa kwanza kumsaini pamoja na kuachia EP yake, Steps yenye nyimbo tano.

Kwa hali hiyo basi utagundua kuwa Diamond na Harmonize wameshindwa kudumu na wasanii waliowasaini katika lebo zao ambao tayari walikuwa wametoka kimuziki.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Leave A Reply