The House of Favourite Newspapers

Faida za kupata matatizo katika maisha

0

Stressed_Man_page-bg_14653WAKATI mwingine matatizo huwafanya watu wahisi mwisho wa maisha umewadia! Hushindwa kabisa kukabiliana na changamoto zinazotokana na matatizo hayo na badala yake hubaki wakilaumu wasijue cha kufanya.

Hilo ni kosa kubwa maishani. Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa matatizo ndiyo nguzo muhimu  katika safari ya kusaka  mafanikio. Bila matatizo na changamoto, si rahisi mtu kunyanyuka na kuanza kufanya kazi.

Matatizo humfanya mtu akue kifikra na kumjengea mbinu mbadala za kutafuta njia za kupata maisha bora. Tafiti mbalimbali za kisaikolojia, zinaonesha asilimia 85 ya waliofanikiwa maishani wengi wao walipitia maisha magumu yaliyowalazimu watumie akili kutatua jambo lililokuwa msukumo wa wao kufanikiwa.

Mwanasaikolojia maarufu duniani, Johhan Wolfgang Van Goethe aliwahi kuandika kwenye moja ya vitabu vyake kuwa “Problems and challenges are important because they always leave us with a great lesson in life” (Matatizo na changamoto ni za muhimu sana, kwa sababu hutuachia somo kubwa maishani).

Kwa maana nyingine ni kwamba, matatizo huchangia ukomavu wa akili katika kukabiliana na maisha kwani hapo ndipo akili huhitajika kutumika kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko kipindi chochote.

Kabla sijasonga mbele, ngoja nitoe mfano mmoja. Jamaa alikuwa akipitapita mitaa ya karibu na nyumbani kwao akamuona mzee mmoja akiwa ameketi huku akisoma gazeti na kunywa kahawa.

Pembeni yake kulikuwa na mbwa aliyeketi huku akibweka kwa maumivu makali, lakini yule mzee hakuonesha kujali hata kidogo.

Yule mpita njia, akamuuliza yule mzee kulikoni yule mbwa abweke kwa maumivu na huyo mzee asimjali?

Katika hali ya kushangaza, yule mzee alijibu kuwa mbwa alikuwa amekalia msumari lakini haukuwa umemuingia sawasawa na kudai kuwa ukimuingia yeye mwenyewe atanyanyuka!

Somo kubwa katika mfano huu ni kuwa, ukiona mtu yuko matatizoni lakini amekaa na kulalamika bila kutafuta suluhu ya tatizo hilo, ni dhahiri kuwa halijambana ipasavyo.

Uwezo uliomo ndani ya mwanadamu timamu ni mkubwa kuliko matatizo. Historia inaonyesha kuwa Mungu hakuumba matatizo kabla ya mwanadamu;  tafsiri rahisi ni kuwa, changamoto zitokanazo na maisha ya watu ni rahisi kuzikabili na zinapokabiliwa hukuza ufahamu na kuleta maendeleo.

Jambo kubwa linalowakwamisha watu wengi ni kulalamika kama mfano wa mbwa, hawachukui hatua za kutafuta suluhu. Ukipita katika mitaa na vitongoji utawakuta watu wakilalamika kuwa hawana fedha, lakini cha kushangaza hawataki kufanya kazi, hawazitafuti; sijui wanategemea fedha zitajileta zenyewe?

Imani ya wanasaikolojia wengi ni kwamba, matatizo ni chachu ya utafutaji; wamehakikisha katika tafiti zao kuwa nguvu ya akili na mwili inatokana na msukumo wa changamoto. Ukimfunga mtu kwenye mti na akawa na maumivu makali hawezi kulia tu, atajitutumua kujinasua, atafikiri cha kufanya ili tu ajikomboe.

Wengi wetu tunapokuwa na shida tunafikiria zaidi matatizo kuliko utatuzi wake. Ukimuuliza mtu unafikiria nini kujikomboa na hali hii duni, atakuambia “sina cha kufikiri nimekwama”,  jambo ambalo ni kosa kubwa. Suluhu ya changamoto za maisha si kubweka mithili ya yule mbwa; ni kuwaza na kutenda namna ya kujinasua.

Mwisho; kwa namna yoyote tusikubali matatizo yetu yatukatishe tamaa ya kufanikiwa, imani ya washindi wa maisha ni KUFANIKIWA, shida ni njia ya kuelekea kwenye neema na si kikwazo cha mafanikio.

Kadiri unavyozitafsiri shida na kuzipatia ufumbuzi ndivyo unavyojiletea maendeleo na kujijengea uwezo wa kushinda shida moja hadi nyingine. Ukiacha shida moja bila kuitafutia ufumbuzi si ajabu ikakutesa hiyo mpaka itakuingiza kaburini. Mwaka 2016, hebu tubadili mtazamo wetu; TUJIAMINI NA KUTENDA – TUTAFANIKIWA!

Leave A Reply