The House of Favourite Newspapers

DAKTARI ATEKWA KAMA ROMA

0
DAKTARI
Daktari anayedaiwa kutekwa

 

DAR ES SALAAM: Ikiwa ni siku chache tu tangu msanii mkali wa Hip Hop, Roma Mkatoliki atoe kibao chake kipya kiitwacho Zimbabwe, kinachozungumzia pamoja na mambo mengine, juu ya tukio la kutekwa kwake, Jumapili iliyopita, daktari mmoja wa dawa za asili, Mubaraka Daruweshi ‘Muba’ naye alitekwa mithili ya ilivyomtokea mwanamuziki huyo.

 

TUANZE NA CHANZO

Chanzo chetu makini kililidokeza Risasi Mchanganyiko kwamba wakati wakiwa mazoezini uwanjani karibu na nyumba ya daktari huyo, walishangaa kuliona gari aina ya Toyota Prado likiondoka kwa kasi na baadaye kufuatiwa na kelele kutoka kwa mke wa jamaa huyo akiomba msaada akidai mumewe ametekwa.

 

“Huyu jamaa licha ya kuwa ni daktari wa tiba asili, pia ni kiongozi wetu hapa msikitini, tunasali naye na mara nyingi zikiwepo kesi kwenye Baraza la Kiislamu, huwa anatumika kusuluhisha, sasa asubuhi tukashuhudia gari likiondoka kwa kasi nyumbani kwake huku mkewe na dada yake wakipiga kelele za kuomba msaada.

ROMA Mkatoliki.

“Watu walijitokeza na bodaboda na kuanza kulifukuzia lile gari, lakini walipoona wananchi wanawakaribia, wakatoa silaha na kuwatisha, wakafanikiwa kumchukua kijana mmoja ambaye alikuwa na pikipiki yake, ambaye alikuwa amelikaribia gari lao, wakampandisha garini na kuondoka naye. “Purukushani zilipozidi, gari lao likaelekezwa Kituo cha Polisi Chang’ombe, wakaliacha nje, watu wachache wakashuka na kuingia kituoni, sijui kama walifanya chochote humo ndani, mara wakatoka na kuondoka tena kwa kasi,” kilizidi kusema chanzo hicho.

 

MKEWE ASIMULIA ILIVYOKUWA

Risasi Mchanganyiko lilikata mitaa hadi Temeke maeneo ya Chang’ombe na kufanikiwa
kukutana na mke wa daktari huyo, huku likishuhudia pia watu wengi ndani ya nyumba yake, waliokwenda kumpa pole kwa tukio hilo lililoteka hisia za watu wengi.

 

 

Mke huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Fatuma, huku akibubujikwa na machozi, alisema; “Nilikuwa nje nafua asubuhi ya saa nne, mume wangu alikuwa anakunywa chai ndani, akaja kijana mmoja na mama mtu mzima, wakaniuliza kama wamemkuta mume wangu, nikawaambia ndiyo, wakaingia ndani.

 

“Yule kijana akaomba aende msalani, akaenda, yule mama akabaki anamweleza mume wangu anavyoumwa presha, maana ni mtaalamu wa tiba za asili, mume akaniambia nikachukue kipimo cha kupimia presha, nikaenda, ile natoka chumbani kuja sebuleni, nakuta watu wawili zaidi wakiwa na bastola, wakatuambia tukae chini, tupo chini ya ulinzi.

 

“Nikakaa chini na mume wangu akawa anawaomba akavae nguo maana alikuwa amejifunga msuli tu, wakakataa, wakanichukua tukaingia chumbani kutafuta nguo, wakakuta nguo yangu wakaichukua wakamfunga usoni, wakamchukua na kuondoka naye. “Wakaniambia nisitoke nje mpaka wao waondoke, walivyoondoka ndiyo nikatoka na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada, gari lao liliondoka kwa kasi, watu wakawa wanalifukuzia huku sisi tukienda kuripoti polisi ambapo walisema tusubiri baada ya saa 24 ndiyo tutaenda kufunguliwa jalada la kesi,” alisema Fatuma. Fatuma alisema huko nje majirani walimwambia waliwaona watu wengine wawili wakiwa na bunduki ambao waliungana na watekaji kuondoka na mumewe.

IGP Sirro.

NYUMBANI KWAKE KAMA MSIBA

Nyumbani kwa daktari Muba, Risasi Mchanganyiko lilishuhudia hali ya simanzi, mithili ya eneo la msiba, watu wengi, wake kwa waume, baadhi yao wakiangua kilio. Familia hiyo na majirani waliokuwa wamekusanyika nyumbani hapo, waliiomba serikali na wanaharakati mbalimbali kuwasaidia ili ndugu yao huyo apatikane.

 

“Tunaiomba serikali itusaidie jamani, maana hapa tuko njia panda kwani hata kituoni tulipoenda hatujapata msaada wa kujua ndugu yetu yuko wapi badala yake tumeambiwa tusubiri saa 24, tunaumia sana kwa kweli maana wangekuwa ni watu wazuri waliomchukua wangeonyesha hata vitambulisho, lakini unaambiwa tangu saa tisa usiku hilo gari lilikuwa likizunguka mitaa hii tu,” alisema mmoja wa majirani.

 

MWENYEKITI WA MTAA ATHIBITISHA

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Mwenyekiti wa Mtaa wa Temeke, Bakili Mohamed alikiri kusikia taarifa hizo na kufika kwenye familia ya Muba ambapo alisimuliwa tukio lilivyokuwa na kuahidi kuendelea kufuatilia zaidi kwa viongozi wa polisi.

 

“Jumapili sikuwepo, lakini nilisikia taarifa hizo ambapo leo (Jumatatu) nilifika nyumbani kwa mwananchi huyo na kukutana na familia ambayo imenielezea tukio lilivyokuwa ila naamini dola inajua maana kama gari ilienda mpaka kituo cha polisi sasa tusemeje, ila ninaendelea kulifuatilia zaidi,” alisema mwenyekiti.

 

MSIKIE KAMANDA MUROTO WA TEMEKE

Ili kuujua ukweli, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi, Temeke, Gilles Muroto na kumuuliza kuhusu kukamatwa kwa mtu huyo nyumbani kwake na watu wasiojulikana ambapo alijibu kwa kifupi kuwa hakuwa na taarifa hizo. Aprili 4, mwaka huu, msanii Roma Mkatoliki, akiwa na wenzake wawili katika studio za Tongwe Records, Masaki jijini Dar es Salaam, alitekwa na watu wasiojulikana na kupatikana siku nne baadaye akiwa na majeraha katika maeneo mbalimbali ya mwili wake. Hakuwahi kusema alitekwa na nani!

 

NA: GLADNESS MALLYA NA ALLY KATALAMBULA

Leave A Reply