The House of Favourite Newspapers

DC aagiza Padre akamatwe kwa utapeli

0

NA STEPHANO MANGO,
RISASI mchanganyiko
RUVUMA: Mkuu wa Wilaya ya Songea, Benson Mpesya ameviagiza vyombo vya usalama kumkamata mara moja Padre mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea ili afikishwe mbele ya sheria kwa madai ya utapeli.
Mpesya alitoa maagizo hayo wakati akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Kata ya Matimila, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, baada ya kumlalamikia kutapeliwa zaidi ya shilingi milioni mbili, walizotoa ili wapatiwe mbolea.

Baadhi ya wananchi hao, Yustini Komba na Kotrida Komba walimweleza mkuu wa wilaya kuwa padre huyo aliyefahamika kwa jina moja la Xavery, alifika Matimila na kujitambulisha kwa wananchi kuwa ametokea Jimboni Songea.
Yustini akiongea kwa jazba alisema wanamfahamu Xavery kwa muda mrefu hivyo walimwamini na kuamua kuchanga fedha kwa kuwa walikuwa na shida ya mbolea na waliziingiza kwenye akaunti ya benki moja kama walivyoelekezwa.
Lakini baada ya hapo, wanasema wamemtafuta padre huyo bila mafanikio na kila walipofuatilia kwa paroko wa parokia ya Matimila aliyekuwa mwenyeji wa padre huyo, lakini naye ameshindwa kumpata.

DC Mpesya aliwaambia wananchi hao kuwa padre huyo licha ya kutapeli wao, amefanya hivyo pia sehemu zingine na taarifa hizo zipo ofisini kwake, hivyo akaagiza kukamatwa haraka iwezekanavyo.

Juhudi za kuwapata viongozi wa parokia za Matimila na Songea ziligonga mwamba baada ya kuelezwa na wasaidizi wao kuwa walikuwa bize na maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka. Gazeti hili linaendelea kufuatilia sakata hilo kwa karibu ili kujua hatima ya agizo hilo la mkuu wa wilaya.

Leave A Reply