The House of Favourite Newspapers

Denti darasa la kwanza ajinyonga

0

Stephano Mango, SONGEA

MAJANGA! Mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Skill Path mjini Songea Mkoa wa Ruvuma, Fatuma Ally (7) amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya manila ambayo ilikuwa ikitumika kuanikia nguo nje ya nyumba ya wazazi wake.

Akizungumza na gazeti hili juzi ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Mihayo Msikhela alisema tukio hilo lilitokea Desemba 12, mwaka huu saa 5 asubuhi katika Mtaa wa Making’inda Kata ya Msamala mjini hapa.

Kamanda Msikhela alisema siku ya tukio, baada ya askari kupata taarifa walifika eneo husika na kumkuta Fatuma ameshafariki dunia akiwa kwenye mti na shingoni akiwa na kamba ya manila.

Alisema kabla ya siku hiyo, Fatuma alikuwa na tabia ya kucheza kwenye kamba hiyo lakini siku ya tukio ilimfanya ajining’inize na kusababisha kifo chake ambacho kimezua mshangao mkubwa.

Alisema wakati tukio hilo linatokea, baba yake mzazi, Ally Omar ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) K-ambi ya Chandamari, alikuwa akinywa chai ndani.

“Baba baada ya kumaliza chai, alitoka nje na kumkuta binti yake akiwa ananing’inia kwenye kamba hiyo ya kuanikia nguo huku ulimi wake ukiwa nje na ameshakata roho,” alisema kamanda huyo.

Kamanda Msikhela alisema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi na kwamba upelelezi wa tukio hilo unaendelea.

Leave A Reply