The House of Favourite Newspapers

Esma Aanika Ugomvi wa Tanasha, Mama D

0

DAR: Baada ya mambo kuzidi kutaradadi huko mitandaoni kuwa, mama mzazi wa staa mkubwa wa Bongo Fleva; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’; Sandra Kassim ‘Mama D’ ana ugomvi na mkwewe; Tanasha Donna, Esma Khan amejivika mabomu na kuanika ukweli wa anachokijua.

 

Kabla ya Esma ambaye ni dada wa Diamond au Mondi kufunguka, madai yenyewe yalisema kuwa, Mama D hataki Tanasha aimbe kwa kuhofia kumfilisi mwanaye.

 

ISHU NZIMA ILIVYO

Awali, Gazeti la IJUMAA lilipokea simu kutoka kwa mdau mmoja ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini na kusema kuwa sababu iliyofanya Mama D au Mama Dangote na mumewe, Shamte wasiposti wimbo wa mkwe wao huyo ni bifu lililopo kati yao kwamba mama huyo hataki Tanasha aimbe.

 

“Unajua mama Dangote na Tanasha hawaelewani hata kidogo na hiyo ndiyo sababu iliyosababisha wasiuposti hata wimbo wake kwenye akaunti zao.

“Kuna kipindi Mama Dangote alimwambia Tanasha aache kufanya muziki, badala yake awe anafanya biashara ya kuremba watu (make-up) kwa kuhofia atamfilisi.

 

“Mama Dangote anaamini kuwa kama Tanasha akiendelea kufanya muziki, Mondi ataingia gharama za kulipia production na vitu kama hivyo.

 

“Lakini Tanasha alimkatalia na kumwambia kuwa yeye huwa hapangiwi vitu vya kufanya. Kwa hiyo hawezi kufanya hiyo biashara ya make-up, badala yake ataendelea kufanya muziki na kila kitu atajilipia mwenyewe bila kumtegemea mtu. Ndiyo maana hawana maelewano mazuri kwa sababu mwanamama huyo amekuwa jeuri kwa Mama Dangote,” kilisema chanzo cha ndani kwenye familia ya Mondi.

 

IJUMAA NA MAMA DANGOTE

Baada ya kupata taarifa hizo, Gazeti la IJUMAA kama ilivyo desturi yake lilimtafuta Mama Dangote ili azungumzie tuhuma hizo zinazomkabili ambapo alisema kwa kifupi kwamba, Tanasha akipostiwa na watu wengine inatosha siyo mpaka na yeye amposti.

 

“Kama ninyi mmeshaposti huo wimbo kwenye akaunti zenu inatosha, siyo mpaka na mimi niposti,” alisema Mama Dangote.

 

ESMA SASA

Gazeti la IJUMAA halikuishia hapo, lilifanya jitihada za kumtafuta dada wa Mondi, Esma Khan ili azungumze chochote kuhusiana na ishu hiyo ambapo baada ya kupatikana alionesha hali ya kushtushwa na jambo hilo.

 

Esma ameliambia IJUMAA kuwa, si kweli kwamba mama yake ana bifu na Tanasha ila ni mambo ya kizushi.

“Jamani watu wanapenda kuzusha mambo! Hivi mnajua Mama Dangote anampenda sana Tanasha? Yaani anampenda hadi…(anatamka maneno makali yasiyoandikika gazeti).

 

“Halafu kuhusu hilo suala la bimkubwa (Mama Dangote) kutoposti huo wimbo kwenye akaunti yake, mimi sioni kama kuna tatizo kwa sababu huwezi kujua, pengine ameonesha sapoti yake kwa njia nyingine. Je, ninyi mtajuaje?

 

“Hebu watu waache maneno yasiyokuwa na ukweli wowote,” alisema Esma.

Leo Tanasha anatarajia kuzindua EP yake yenye nyimbo nne, zoezi ambalo litafanyika Nairobi nchini Kenya.

Stori: Memorise Richard nan Khadija Bakari, Ijumaa

Leave A Reply