The House of Favourite Newspapers

Esma, Petit Gari Limewaka

0

GARI limeweka! Ndiyo sentensi inayotumika kwa watalaka, Esma Khan na Hamad Manungwi ‘Petit Man’. Hii ni kufuatia penzi lao kusemekana limerejea kwa kasi ya kimbunga huku wakidaiwa kupika na kupakua kama zamani.

 

Esma ambaye ni dada wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anadaiwa kurejesha majeshi kwa Petit baada ya kumwagana na mumewe, Yahaya Msizwa; yule tajiri aliyefunga naye ndoa iliyogharimu mamilioni, lakini haikudumu hata kwa miezi mitatu.

 

Wapashaji na wafuatiliaji wa mambo ya watu wanadai kuwa, mara tu baada ya Msizwa kurejea nchini Afrika Kusini, mahali ambapo alikuwa akiishi siku zote na mkewe mkubwa aitwaye Mama Melo ndipo Esma akaona isiwe tabu, naye akarejea kwa Petit ambaye ni meneja wa wasanii wa Bongo Fleva.

 

“Ukweli ni kwamba, tangu huko nyuma, mapenzi ya dhati ya Esma yapo kwa mtalaka wake Petit Man na ilikuwa ngumu mno zile siku alizokuwa akiishi kwa Msizwa maana hakuwa ana furaha ya kweli.

 

“Watu tu walikuwa hawajui ukweli halisi uliokuwepo na ndiyo maana sasa hivi wameamua kurudiana,” anasema mpashaji huyo ambaye ni mtu wa karibu wa Esma na Petit.

 

Chanzo hicho kilizidi kuweka wazi kwamba, hata Petit alipofiwa na mama yake mzazi hivi karibuni, Esma ndiye alikuwa mfariji wake mkubwa na mara nyingi walionekana wakiwa bega kwa bega.

 

“Ukisikia gari limewaka kwa mara nyingine, basi ndiyo hivyo. Mapenzi ya kweli kati ya Esma na Petit ndiyo habari ya mjini kwa sababu wameshaachana kibao, lakini wanarudiana na hivyo ni ngumu kabisa wale kutengena na mtoto wao, Taraj ndiye anawafanya waendelee kuwa pamoja,” anasema ‘kikulacho’ huyo.

 

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na Esma ambaye alisema kuwa, kama mtu hawezi kusoma, basi atazame picha kwani ataelewa hivyo hawezi kuzungumza zaidi kuhusiana na hilo kwa sababu kila kitu kiko wazi au kinajieleza.

 

“Jamani mtu anaposhindwa kusoma kilichoandikwa basi hata picha tu inamuongoza kujua chochote,” anasema Esma. Alipotafutwa Petit, simu yake iliita bila kupokelewa.

STORI: IMELDA MTEMA, DA

Leave A Reply