The House of Favourite Newspapers

Exclusive… Siri Nzito Yafichuka Magari Wasafi

0

DAR: Hii ni exclusive! Mpya kutoka kwenye makaratasi yake, Gazeti la IJUMAA linakuletea nyuma ya pazia kuhusu muonekano mzuri wa magari wanayoyatumia mastaa wa kruu inayosumbua anga la Bongo Fleva, Wasafi Classic Baby (WCB), karibu.

 

MIJADALA YA MITANDAONI

Kwenye mitandao ya kijamii, hususan Instagram, kumekuwa na mijadala ambayo imekuwa ikiibuka na kutikisa kuhusu magari wanayotumia mastaa hao.

 

Kuna ambao wanaonesha shaka yao kwa kutoamini kama kweli, mastaa hayo wanazo pesa za kununua magari hayo ambayo yanaonekana yameundwa miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo ni vigumu mno kulimudu.

 

“Wewe unataka kuniambia Mondi hili Toyota Land Cruiser V8 lake anaweza kuwa amelinunua la mwaka 2018 au 2020? Haiwezekani bwana, tuweni wa kweli,” ni miongoni mwa hoja zilizogonga kwenye vichwa vya wengi mitandaoni.

 

MADAI YA KUYAKODISHA…

Kuna wengine walikwenda mbali kwa kudai kuwa wasanii hao wamekuwa wakisema kwamba magari hayo wanayakodi na kufanyia show-off (kujionesha), halafu wanayarudisha ‘show-room’.

 

“Hivi wewe unadhani kununua magari kama yale ya bei ghali kiasi kile ni mchezo, habari ni kwamba hayo magari kuna mahali wanayachukua, wanatamba nayo mjini, halafu wakimaliza wanayarudisha.

 

“Hivi wewe hushangai unaweza ukamuona Diamond na gari fulani, halafu wiki ijayo unamuona na lingine. Kuna kamchezo tu wanacheza hana uwezo wa kununua magari yote haya,” alichangia mdau mwingine.

 

KUHUSU MBOSSO

Kama ilivyokuwa kwa Mondi, wananzengo wamemchachamalia Yusuf Mbwana ‘Mbosso’ kwamba, gari analotamba nalo aina ya Toyota Land Cruiser Prado si mali yake, bali amepewa na bosi wake, Mondi na ni lile alilokuwa amemzawadia aliyekuwa mpenzi wake, Tanasha Donna.

 

Mbali na hayo, ‘vurugu-mechi’ hiyo iliyagusa pia magari mengine likiwemo la Zuhura Othuman ‘Zuchu’, la Tanasha Donna na lile la Mama wa Mondi, Sanura Kassim ‘Sandra’.

 

IJUMAA KAZINI

Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa mengi bila kuwa na ukweli wa mambo, Gazeti la IJUMAA lilifanya uchunguzi wake na kumpata mtu ambaye huwa anayabadilisha muonekano magari hayo na kuonekana ya kisasa.

 

Mtu huyo si mwingine bali ni jamaa mmoja aitwaye Ismail ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Rider ambaye anatoa ufafanuzi wa kina kuhusu magari hayo.

 

AANZA NA MONDI

“Labda niwatoe hofu tu kuhusiana na magari ya Diamond, ukweli ni kwamba magari yote wanayoyaona ni ya kwake kabisa wala hana ambalo halimiliki yeye, maana mimi ndiye ninayeyafanya service (matengenezo) ya magari yao kila mara ofisini kwangu.

 

ANA ZAIDI YA SITA…

“Diamond ana magari zaidi ya sita. Miongoni mwa magari yake ni BMW X6 na lile Toyota Land Cruiser V8, ninakuhakikishia yangekuwa siyo ya kwake ningejua kila kitu,” alisema Rider.

 

PRADO LA MBOSSO, TANASHA…

Alipoulizwa kuhusu Toyota Prado V8 za Mbosso na Tanasha, Rider anafunguka;

“Zile gari (la Mboss na Tanasha) ni magari mawili, lakini ni model moja ila kuna utofauti kwenye vifaa, watu wamekuwa wakiyafananisha ila kwa mtu anayeyajua magari, ukiangalia utaona kwamba yale ni magari mawili tofauti.

 

“Mimi ambaye nimeyaboresha miundo yake hata ukiniamsha usingizini lazima nitayajua utofauti wake na mimi nilijua nikiyaacha yafanane yangeweza kuleta maneno mengi kama yalivyokuwa sasa ndiyo maana nikaamua kuyatofautisha baadhi ya sehemu ila kwa mtu wa kawaida kugundua inakuwa shughuli.

 

“Kwenye rimu nimeweza kuzitofautisha, ya Tanasha nimeweka ndogo na lila la Mbosso nimeweka kubwa hata maua yana utofauti, hata show ya mbele nimeweka model tofauti.”

 

LA ZUCHU SASA…

Alipoulizwa kuhusiana na gari la Zuchu aina ya Toyota Vanguard ambalo alipewa na Mondi na kwa sasa lina muonekano wa tofauti, Rider anasisitiza;

 

“Kuna vifaa ambavyo huwa tunatumia, unajua sisi tunaweza kutoa gari kutoka kwenye mwaka 2008 hadi 2020 kabisa na gari ikaonekana kuwa kwenye chati, hakuna mtu ambaye hapendi gari lake liwe kwenye trending.”

 

LA MAMA DANGOTE

Ride alifafanua pia lile Toyota Land Cruiser V8 ambalo Mondi alimzawadia mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ wakati akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

 

“Ni kweli alimpa na hilo gari hadi leo lipo na mimi ndiye ninalifanyia service (matengenezo) kila mara kwenye kulipaka rangi na mambo mengine na hata lile jina kwenye plate namba niliweka mimi, kwa hiyo hakuna wa kunidanganya kuhusiana na magari ya Wasafi yote,” alisema.

Stori: Khadija Bakari

Leave A Reply