The House of Favourite Newspapers

Fahamu Taratibu za Kubadilisha Umiliki wa Gari – Video

0

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya baadhi ya watu wanakuwa wamesajili vyombo vya moto lakini usajili wao ni batili, hawajasajiliwa na TRA ambapo magari yao yanakuwa yameliingiza nchini kimagendo, jambo linalopelekea magari zaidi ya moja yote yanakuwa na namba moja ya gari.

 

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Oktoba 8, 2021 na Mercy Macha ambaye ni Afisa Msimamizi wa Kodi TRA wakati akitolea ufafanuzi katika kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio huku akiwahimiza wananchi kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo kubadili umiliki wa vyombo vya moto ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwakumba.

 

“Jukumu la TRA sio kukusanya kodi tu, hata kuelimisha pia. Kabla hujanunua gari lazima au chombo chochote cha moto, fika TRA ujue kama chombo hicho ni cha halali, hakidaiwi kodi, fuata taratibu wa kubadilisha umiliki kuja kwako.

 

“TRA tumekuja na utaratibu mpya, unapokuja kubadilisha umiliki wa chombo lazima mmiliki wa mwanzo awepo, mmiliki mpya (aliyeuziwa) awepo na atuonyeshe kitambulisho chake, chombo lazima kiwepo maofisa wetu wakikague kuanzia Chassis Number. Unapobadilisha umiliki wa chombo lazima zile kodi za uhamishaji wa chombo zichukuliwe, TRA tukusanye mapato.

 

“Gharama ya kuhamisha umiliki wa chombo cha moto ni Tsh 100,000 jumlisha asilimia 1 ya gharama ya ununuzi iliyoandikwa kwenye kwenye mkataba, na huu mkataba lazima uwe legal, usainiwe na mwanasheria na aweke risiti ya huduma aliyotoa.

 

“Kuna wanaopewa bajaji za mkataba, anaendesha akimaliza mkataba anakabidhiwa inakuwa ya kwake lakini hawaji kubadilisha umiliki, hawa nao tunawahimiza kuja TRA kubadilisha umiliki wa vyombo vyao.

 

“Kwa magari ambayo yameingizwa nchini yakiwa na msamaha wa kodi, wakati yanauzwa kuna utaratibu wa kufuatwa kuhakikisha msamaha hauhami kwenda kwa mtu mwingine, mhusika arudi TRA kufuata taratibu hizo. Usiuze chombo chako cha moto bila kuhakikisha umebadilisha umiliki, unayenunua hakikisha nawe unakuwa mmiliki halali wa chombo chako,” Mercy Macha, Afisa Msimamizi wa Kodi TRA.

 

Leave A Reply