The House of Favourite Newspapers

Fahamu Urafiki wa Nelson Mandela na Mwl. Nyerere

0

UKIZUNGUMZIA mashujaa wa Afrika ni lazima kutaja majina ya Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa Kongo, Benjamin Nnamdi Azikiwe na Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria, na wengine wengi, orodha inaweza kuwa ndefu lakini si ndefu kiasi hicho, na bila shaka juu ya orodha hiyo yuko Nelson Rolihlahla Mandela na Julius Kambarage Nyerere.

 

Katika orodha hiyo ndefu, dunia na hata baadhi ya Watanzania wanamjua au kumsikia zaidi Mzee Mandela au Madiba kama wanavyopenda kumuita watu wake.

 

Haitakuwa kazi rahisi kuona macho yaliyobeba uchungu wa mateso makali ya serikali ya kibaguzi lakini yanayohubiri amani na msamaha, walau kitu kimoja kiko dhahiri popote na kwa yeyote anayetaka kukiona, ni jinsi historia ilivyomuandika, maandishi yako wazi kwa kila mwenye macho ya kuona, na akili ya kuelewa, yu aelekea kuvikwa taji ya haki.

 

Ni vigumu kweli kuandika au kumzungumzia mtu wa kiwango cha Madiba, lakini inaweza kuswihi kuanza na mchapuo huu. Mapema mwaka 2005 wakati huo akiwa Seneta, Barack Obama, alipata fursa kuhudhuria kipindi cha television cha Oprah Winfrey na katika mazungumzo, Oprah alimpatia fursa Obama ya kumpa ujumbe wowote anaotaka ampelekee Mzee Nelson Mandela.

 

Obama aliingia chumba cha nyuma ya studio ya Oprah kuandika ujumbe huo kwa Mandela, ilipoonekana amechukua zaidi ya muda uliotarajiwa katika kuandika ujumbe huo, msemaji wake Roberts Gibbs alimfutata kumwangalia ni kitu gani kimemchukulia muda namna hiyo.

Akiwa bado anatafakari nini kuandika, Obama alimwambia msemaji wake; “Ni lazima mnipe muda wa kutosha, huwezi ukaandika ujumbe mwepesi mwepesi tu kwa Nelson Mandela”. Anaandika mwandishi Michael D. Shear wa New York Times, toleo la Juni 27, mwaka 2013.

 

Hakuna ubishi juu ya ushujaa wa Nelson Mandela na heshima anayopata duniani, yeye ni ishara ya amani na maridhiano, ni alama ya ushirikiano dhidi ya chuki na visasi. Ni Mwafrika pekee mwenye sanamu katika eneo maarufu jijini London la Parliament Square, sanamu yake ikiwa sambamba na sanamu za watu maarufu duniani kama Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, Waziri Mkuu Uingereza Winston Churchill.

 

Lakini huyu Mandela amefikaje hapo?

Kama Waswahili wasemavyo ukiona vyaelea ujue vimeundwa, bila shaka Nelson Mandela wa leo asingekuwa Mandela huyu tunayemfahamu bila kuwepo juhudi za watu waliokuwa na fikra na misimamo thabiti ya kupambana dhidi ya ubaguzi rangi wakati akiwa gerezani kwa miaka yote 27 na hata kabla ya hapo.

 

Miongoni mwa watu muhimu waliomfanya Mandela huyu awe hivi alivyo leo, anayeweza kuchukua nafasi ya kwanza ni Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza Tanganyika na Tanzania, msimamo wa dhati na usioyumba wa Nyerere dhidi ya aina zote za dhuluma ndiyo umejenga msingi ushujaa wa Mandela unaojulikana duniani leo.

 

Kwa maneno yake mwenyewe, Nelson Mandela, katika dhifa aliyoandaa kwa heshima ya Mwalimu Nyerere, Oktoba 17 mwaka 1997, alimwelezea Mwalimu kama mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Jumuiya ya Madola kuitenga Afrika Kusini ya kibaguzi, baada ya mauaji ya Sharpville.

“Huyu ni mpigania Uhuru ambaye aliitika wito wa Chifu Luthuli kuungana na Trevor Huddleston kuanzisha vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi nchini Uingereza mwaka 1959, kiongozi ambaye juhudi zake katika mkutano wa Jumuiya ya Madola zilisababisha Afrika Kusini ya kibaguzi kutengwa, baada ya mauaji ya Sharpville.

 

Nilipata bahati kukutana naye miaka mingi iliyopita, mwaka 1962, nilipozuru Tanzania kutafuta msaada tulipoanzisha mapambano ya silaha. Wakati huo, kama ilivyo sasa, nilishangazwa na msimamo wake, hamu yake ya kutaka haki na usawa popote, na dhamira yake kwa maslahi ya Afrika”

Wakati tukielekea kupata Uhuru, Mwalimu pamoja na kuwa kiongozi wa taifa changa hakusita kuweka wazi msimamo wake ambao bila kuwa na ujasiri wa kipekee, viongozi wachache sana wangeweza kuwa na msimamo wa namna hiyo hasa msimamo wenyewe unapowawekea wale wanaotarajiwa kuwa wahisani wako.

 

Mei mwaka 1961 kuelekea mkutano wa mawaziri wakuu wa Jumuiya ya Madola, huku Waziri Mkuu wa Afrika Kusini akitarajiwa kuhudhuria mkutano huo, Mwalimu aliandika makala kwenye gazeti la London Observer ikiweka wazi msimamo wa Tanganyika akisisitiza kuwa Tanganyika haitajiunga Jumuiya ya Madola kama Afrika Kusini wataendelea kuwa wanachama.

Makala hiyo iliyohitimishwa kwa maneno mazito yenye msisitizo; “To vote South African in, is to vote us out” kwamba kuwakubalia Afrika Kusini uanachama ni kutukataa sisi, iliamsha hamasa kubwa dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Mwandishi nguli wa masuala ya Jumuiya ya Madola ambaye pia ni mwasisi mwenza wa Umoja wa Waandishi wa Habari wa Jumuiya ya Madola (CJA), Derek Ingram, anazungumzia hatua hiyo ya Mwalimu kuwa ilisababisha shinikizo kubwa kwa Afrika Kusini mpaka ikajitoa; “His move stepped up the pressure on South Africa and led to its withdrawal a few days later.”

 

Mchango wa Mwalimu katika harakati za ubaguzi hauishii hapo, Juni 26, 1959 Kamati ya Jumuiya za Kiafrika (CAO) iliitisha kikao katika ukumbi wa Holbourne jijini London, kuwataka Waingereza wasusie bidhaa za Afrika Kusini, hasa matunda yaliyokuwa yanauzwa kwa wingi katika miji mbalimbali ya Uingereza katika vuguvugu lililoitwa Boycott Movement, Askofu Mkuu Trevor Huddleston, Mwalimu Nyerere na Kanyama Chiume wa Malawi ndiyo walikuwa wasemaji wakuu katika hadhara hiyo na waasisi wa vuguvugu hilo lililokuja kujulikana baadaye kama Ant – Apartheid Movement (AAM).

 

Tangu mwanzo wa miaka ya 1960 mchango wa AAM katika kuutokomeza ubaguzi wa rangi ulikuwa hauna kifani, lakini pia ikumbukwe kuwa vuguvugu hilo halikuwahi kuwafurahisha wakubwa kwa sababu ya maslahi yao Afrika Kusini.

 

Pamoja na Chama cha Labour cha Uingereza, kuahidi kuacha kuiuzia silaha Afrika Kusini kama kingeshinda uchaguzi lakini hata baada ya kuingia madarakani kwa Waziri Mkuu wake, Harold McMillan, ahadi hiyo ilishindwa kutekelezwa kwa vitendo.

 

Hata alipozuru Afrika Kusini na kutoa hotuba yake maarufu katika Bunge la Afrika Kusini; “The wind of change is sweeping across Africa,” pamoja na kuona huo upepo wa mabadiliko uliokuwa unalikumba Bara la Afrika wakati huo, McMillan siyo tu hakuunga mkono shughuli za AAM lakini alilaani harakati hizo.

 

Hili halishangazi kwa vile kwa mujibu wa mtandao wa South African History on line (SAHO), katika miaka hiyo ya 1950 Uingereza ilikuwa mshirika mzuri wa biashara wa Afrika Kusini, zaidi ya asilimia 30 ya bidhaa zilizoingizwa Afrika Kusini zilitoka Uingereza, asilimia 28 ya mauzo ya bidhaa za nje za Afrika Kusini ziliuzwa Uingereza. Ukiondoa uhusiano huo wa kiuchumi, kati ya mwaka 1946 na 1959 kulikuwa na Raia wa Uingereza zaidi ya 113, 000 waliokuwa wakiishi Afrika Kusini.

 

Hizi ndizo juhudi zilizoweka msingi wa mapambano ya dhati dhidi ya aina zote za dhuluma ambazo kwa hakika zisingeweza kufika mbali au kufanikiwa kwa kiwango hicho bila kuwa na nguvu ya Mwalimu Nyerere ambaye, msimamo wake dhidi ukandamizaji wa aina yoyote ile ulikuwa dhahiri hata kwa wasiokubaliana naye.

 

Kujitolea kwake kulikoifanya Tanganyika na kisha Tanzania kuwa kimbilio na ngome ya kutumainiwa na wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika katika mazingira hatari kama vita baridi vya wakati huo, kwa kiwango cha juu kabisa pamoja na mambo mengine yamechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Afrika Kusini ya Mandela na hata Madiba mwenyewe kuwa jinsi walivyo leo. Na ni uungwana tu kusema kuwa nyuma ya fahari aliyonayo Mandela leo, yuko Julius Kambarage Nyerere aliyeongoza kuwapinga makuburu si kwa sababu ya rangi yao bali matendo yao.

*********

 

MWAKA 1976, baada ya kutokea mauaji makubwa ya wanafunzi katika mji wa Soweto, yaliyotekelezwa na polisi wa makaburu, na hivyo kusababisha vijana wengi wa ANC kuikimbia Afrika Kusini na kwenda kuwa wakimbizi nje, chama hicho kiliona haja ya kuwa na shule yake nchini Tanzania ambayo ingetumiwa na vijana hao wa ANC waliokuwa wamekimbia kukwepa vipigo vya polisi.

 

Kutokana na hali hiyo, mwaka huo, ujumbe wa ANC uliwasilisha ombi kwa Mwalimu la kupatiwa ardhi ya kutosha ya kuweza kujenga shule zake, kuanzia chekechea, msingi na sekondari. Mwalimu alikubali ombi hilo la ANC na kuwakabidhi wajumbe hao kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa wakati huo, Anna Abdallah ili awatafutie ardhi ndani ya mkoa wake.

 

RC Anna Abdallah, aliwachukua viongozi hao wa ANC, akiwamo Tambo hadi katika shamba la mkonge la Mazimbu na kuwakabidhi eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Elimu cha ANC (ANC Education Facilities). Mwaka 1978 ilizinduliwa rasmi shule ya kwanza ya msingi ya ANC Mazimbu, mwalimu wake mkuu akiwa Wintshi Njobe.

 

Mwaka 1979, ANC ilipata pigo kubwa baada ya mwanaharakati wake kijana, mwanafunzi bado wa shule, ambaye alikuwa mwiba kwa serikali ya kibaguzi ya makaburu, Solomon Mahlangu kunyongwa hadi kufa baada ya Mahakama ya nchi hiyo kumtia hatiana na kutoa hukumu ya kunyongwa mwaka 1977, kwa madai ya kuendesha vitendo vya kigaidi.

 

Inasimuliwa kwamba wakati wa kutekeleza hukumu hiyo ya kunyongwa, Aprili 6, mwaka 1979, akiwa katika Gereza Kuu la Pretoria, makaburu walimwita mama yake na ndugu yake ili kushuhudia tukio hilo la kinyama.

 

Wakati Solomon akipandishwa kwenye kitanzi, kijana aliyekuwa amehitimu mafunzo ya Umkhonto wa Sizwe katika kambi za jeshi za ANC nchini Angola na Msumbiji kutokana na kukatishiwa masomo yake na Makaburu akiwa darasa la nane mwaka 1976, mama yake alianza kububujikwa machozi, lakini Solomon akamwambia mama yake kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kulia, na badala yake akamwambia mama yake maneno yafuatayo:

“Tell my people that I love them and that they must continue the struggle, my blood will nourish the tree that will bear the fruits of freedom. Aluta Continue.” (Mama ninakufa, waambie watu wangu (Wana-ANC) kwamba nawapenda na waendeleze mapambano haya, damu yangu hii itakayomwagika ndiyo itakuwa kirutubisho cha mti ambao hatimaye utatoa matunda ya uhuru. Mapambano yanaendelea).

 

Baada ya tukio hilo la kunyongwa kwa mwanafunzi Solomon aliyekuwa na miaka 23, kituo cha elimu cha ANC Mazimbu, Morogoro, kilibadilisha jina la kituo hicho kama hatua ya kumuenzi mwanaharakati huyo, na kukiita Solomon Mahlangu Freedom College (Somafco) hadi mwaka 1992 kilipofungwa baada ya utawala wa makaburu kusalimu amri dhidi ya harakati za ANC, kwa kumwachia huru Mandela kutoka kifungo cha maisha, kuruhusu shughuli za kisiasa, kisheria na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, na hivyo kutimia kwa ndoto ya Solomon Mahlangu.

 

Solomon Mahlangu Campus, SUA Kwa sasa eneo hilo la Somafco Mazimbu, linamilikiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), baada ya Serikali kulikabidhi rasmi kwa chuo hicho mwaka 1998. Uongozi wa SUA kutokana na kuenzi mchango wa kijana Solomon katika harakati za ANC kusaka ukombozi wa Afrika Kusini, umebadili jina lake kutoka Solomon Mahlangu Freedom College na kuwa Solomon Mahlangu Campus (SMC).

 

Magdalena John, ni Ofisa Utawala wa kampasi hiyo ya SUA. Katika mazungumzo na Raia Mwema chuoni hapo hivi karibuni, anasema kituo hicho cha elimu cha ANC Mazimbu, mbali na kutoa elimu ya awali hadi sekondari, wanafunzi na wanaharakati wa ANC walikuwa wanajishughulisha pia na miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kukiongezea uwezo wa kiuchumi kituo hicho.

 

Anaitaja baadhi ya miradi ya kijamii na kiuchumi iliyokuwa ikiendeshwa katika eneo hilo na wapiganaji hao wa ANC kuwa ni pamoja na hospitali iliyokuwa na hadhi ya mkoa ya daraja la pili, iliyokuwa ikiitwa kwa jina la ANC Holland Solidarity Hospital iliyozinduliwa rasmi Mei 4, 1984, na Oliver Tambo ambaye ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa ANC aliyekuwa akiishi mahali hapo hadi kinafungwa mwaka 1992.

 

Ofisa Utawala huyo anaitaja miradi ya kiuchumi kuwa ni pamoja ranchi ya mifugo iliyokuwa imesheheni ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku. Aidha, kulikuwa na mradi wa kiwanda cha ushonaji nguo na kiwanda cha kutengeneza samani (furniture) kilichokuwa kikijulikana kwa jina la Vuyisile Mini Furniture.

 

Kwa mujibu wa Magdalena, kutokana na ongezeko la wana ANC katika eneo hilo na pia kupanuka kwa mahitaji kwa jamii hiyo ya wana ANC, mwaka 1988/89 uamuzi ulifikiwa wa kukihamisha kiwanda hicho cha ushonaji wa nguo, ambazo nyingi ya hizo zilikuwa nguo za kivita kwa ajili ya wanapiganaji wa Umkhonto, na kukipeleka Dakawa ambako ANC ilikuwa imeanzisha kambi nyingine ya kutolea mafunzo ya kijeshi kama ilivyokuwa kwa Kongwa.

 

Kiwanda hicho cha nguo cha Dakawa, kilijulikana kwa jina la ANC Dakawa Arts & Craft. Mitambo ya kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wake wote vilihamishwa na ANC mwaka 1993 na kupelekwa Grahamstown, na hadi sasa shughuli hiyo ya ushonaji inaendelea chini ya jina hilo hilo la ANC Dakawa Arts & Crafts.

 

Wapiganaji hao wa ANC waliacha nini hapo Mazimbu? Yapo makaburi 97, kati ya makaburi hayo mawili yakiwa yamefukuliwa na wenye nayo na kuhama nayo kwenda Afrika kusini, yanayotokana na vifo vya watoto na watu wazima katika familia za wapiganaji wa chama hicho waliokuwa wakiishi hapo.

 

Lipo jengo moja karibu na makaburi hayo lililokuwa likitumika kama nyumba ya ibada, jingo kubwa la kiutawala na nyumba 162 za familia ambazo kwa sasa zinatumiwa na wafanyakazi wa kampasi hiyo ya SUA, madarasa 28, kumbi nne za mihadhara ya kitaaluma na ukumbi wa bwalo unaojulikana kwa jina la The Nelson Mandela Freedom Square.

 

Ipo pia mitaa kadhaa inayobeba majina ya miji ya mataifa ya nje, kama vile Copenhagen ili kuenzi michango ya hali na mali wa mataifa hayo, ikiwamo Denmark, katika harakati za ANC kutafuta ukombozi wa Afrika kusini, pamoja na mtaa wa Heroes (Mashujaa) unaoelekea kwenye makaburi ya mashujaa hao 97 waliozikwa katika makaburi hayo.

 

Nihitimishe makala haya kwa kusema juhudi za Mandela zinamwongeza mwanamapinduzi huyo katika orodha ndefu ya mashujaa wa taifa hilo la Afrika Kusini. Katika orodha hiyo, Govan Mbeki, Oliver Tambo, Solomon Mahlangu, Steven Biko, Chris Hani, Joe Slovo, Yusuf Dadoo, Walter Sisulu, Fatima Meer, Ashley Kriel, Anton Fransch, Joe Modise, Lilian Ngoyi, Tsietsi Mashirini, Helen Joseph, Ben Turok, Ambrose Makiwane, Miriam Makeba, Adelaide Tambo na wengine wengi wataendelea kuenziwa na kizazi cha sasa na kijacho cha ANC.

***********************************************

UHUSIANO baina ya Tanzania na Nelson Madela ulichochewa na mauaji ya Sharpeville yaliyotokea mwaka 1960; na ulipita katika majaribu mengi yakiwamo mkutano baina ya Madiba na Mwalimu Nyerere mwaka 1962.

 

Mapitio ya maandishi mbalimbali pamoja na mahojiano ambayo gazeti hili limefanya na watu waliofahamu uhusiano baina ya Mandela, Nyerere, nchi pamoja na vyama vyao, yameeleza mengi kuhusu uhusiano huo wa kihistoria baina ya nchi hizi.

Maandishi katika mtandao wa chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini, yanaonyesha namna uongozi wa juu wa chama hicho ulipoamua kuhamia Tanganyika baada ya serikali dhalimu ya makaburu wa Afrika Kusini kukipiga marufuku chama hicho pamoja na kile cha PAC, baada ya mauaji hayo ya Sharpeville.

 

Chama hicho kilimtuma kada wake, Frene Ginwala, kuja nchini hapa mwaka huo huo wa 1960 na yeye ndiyo hatimaye aliyepanga mipango ya kuwasafirisha kwa siri viongozi wa juu wa ANC kama vile Oliver Tambo na Yusuf Dadoo kuja Tanganyika wakati huo.

 

Baadaye, Ginwala alipewa kazi na Mwalimu Nyerere kama mhariri wa gazeti la serikali la Standard (sasa Daily News) na Baba wa Taifa ndiye aliyewapokea akina Tambo na huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wa kipekee baina ya Tanzania na wapigania uhuru wa Afrika Kusini.

 

Chama cha ANC kinasema kwamba wakati chama hicho kilipoamua kutumia nguvu kuung’oa utawala wa makaburu, kilimtuma Mandela kuja Tanganyika ili kuzungumza na Nyerere kwa ajili ya kupewa msaada wa kifedha na mafunzo.

 

“Hata hivyo, mkutano huo wa kwanza baina ya Nyerere na Mandela haukuisha vizuri kwa sababu Mwalimu aliwataka ANC kusitisha njia ya mapigano hadi kwanza utawala wa makaburu utakapomtoa gerezani mpigania uhuru mwingine wa chama cha PAC, Robert Sobukwe.

 

“Nyerere pia alikuwa na uhusiano mzuri na Sobukwe na kwa kweli Mandela hakufurahishwa sana na ushauri huo wa Nyerere. Hata hivyo, katika miaka iliyofuata uhusiano huo, Tanzania ilikuja kuwa mshirika mzuri sana wa ANC,” unasema mtandao wa www.sahistory.org.za

Taarifa rasmi zinaeleza kwamba Tanzania ndiyo yalikuwa makao makuu ya kwanza ya ANC na PAC na hadi kufikia mwaka 1965, jumla ya wapigania uhuru 800 walikuwa wanapata mafunzo katika vyuo vya Mazimbu, mkoani Morogoro na Kongwa mkoani Dodoma.

 

Mazimbu na Kongwa
Nyerere, baadeye kubali kuanzishwa kwa kambi ya kwanza ya mafunzo ya kijeshi ya wapiganaji wa kundi la Umkhonto wa Sizwe wilayani Kongwa mkoani Dodoma kati ya mwaka 1963 na 1964 na serikali ya Tanzania ilikuwa ikigharamia sare na mlo mmoja wa wapiganaji hao.

Miongoni mwa walioanzisha kambi hiyo ni Joe Modise ambaye baadaye alifikia kuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali isiyokuwa ya kibaguzi ya Afrika Kusini.

 

Kambi ya Mazimbu ndiyo ambayo baadaye ilikuja kujenga chuo cha mafunzo maarufu kwa jina la Solomon Mahlangu (SOMAFCO).

Maelezo mbalimbali yanaonyesha kwamba aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Moroagoro katika miaka ya 1970, Anna Abdallah (baadaye alikuja kuwa waziri katika wizara mbalimbali na sasa mbunge), ndiye aliyewapa eneo hilo wapiganaji hao wa ANC.

 

Nusura uhusiano uvunjike
Mwaka 1969, uhusiano baina ya ANC na Tanzania ulifikia katika hatua mbaya. Kada wa TANU, Oscar Salathiel Kambona, alidaiwa kutaka kumpindua Nyerere kwa kushirikiana na wapiganaji wa Umkhonto waliokuwa wamechoka kufanya mazoezi hapa nchini pasipo kutumwa kurudi kwao kuanzisha mapambano.

 

Maelezo kuhusu hilo yalitolewa na kada wa PAC, Potlako K. Lebalo, na serikali ya TANU iliamua kurejesha makambini wapiganaji wote wa ANC waliokuwepo ikiwa ni pamoja na kukiondoa chama hicho hapa nchini.

Hata hivyo, mwana historia wa ANC, William Gumede, anasimulia kwamba Tambo aligoma kulazimishwa kwa wapiganaji hao kufungiwa makambini; kwa maelezo kwamba wao ni “Wapigania Uhuru na si wakimbizi.”

 

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa ANC kuhamishia Lusaka makao yake makuu ambayo yalidumu hadi chama hicho kiliporuhusiwa tena kushiriki katika siasa.

Hata hivyo, serikali ya Tanzania ilikuwa na msimamo mkali pia dhidi ya wanachama wa ANC waliokuwa na mrengo wa kikomunisti. Hiyo ndiyo sababu wanachama kama Michael Harmel, Dadoo, Joe Slovo na Ruth First baadaye walipigwa marufuku kukanyaga katika ardhi ya nchi hii.

 

Hata hivyo, kutokana na mauaji ya Soweto ya mwaka 1976, ambayo pia yalisababisha utawala wa makaburu kukamata watu wengi zaidi, ndipo wananchi wengine wakakimbia Afrika Kusini na kuja Tanzania.

 

Hapo tena, Anna Abdallah, kwa maelekezo ya Nyerere, alitafuta eneo katika mkoa wake kule Dakawa ambako nako ikawa kambi ya wapiganaji.

Alipotoka jela, Mandela kwanza alitembelea Lusaka yalikokuwa makao makuu ya ANC na ndipo akafanya ziara yake ya kwanza nchini Tanzania ambapo alipokewa na Mwalimu aliyekuwa amestaafu tayari.

 

Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo na mmoja wa watoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Rashid Kawawa, anasimulia namna baba yake alivyofurahi wakati Mandela alipotoka gerezani na kutembelea Tanzania.
“Uajua Mwalimu alimpa baba (Kawawa) majukumu mazito ya kusimamia harakati za ukombozi. Mambo mengi yalikuwa yakiishia kwake kabla ya kwenda kwa Mwalimu.

 

Yeye hakuwa amewahi kumuona Mandela zaidi ya kumsikia tu na kusaidia wapiganaji wake. Sasa siku Mandela alipokuja Tanzania (Machi, 1990), baba alifurahi sana na akasema kuna kipindi walidhani hawataweza kumwona Madiba akiwa hai,”anasema Vita.

 

Akizungumza na Raia Tanzania mjini Dodoma wiki hii, Mbunge wa Rungwe Magharibi (CCM), Profesa David Mwakyusa, alisema ishara ya uhusiano mzuri baina ya Nyerere na Mandela ni mwaliko ambao Mwalimu alipewa na Madiba mwaka 1994.

 

Nakumbuka nilikuwa na Mwalimu Ulaya wakati Mandela aliposhinda Uchaguzi Mkuu wa Afrika Kusini mwaka 1994. Tukiwa huko Mwalimu alitumiwa ujumbe na Mandela wa kumtaka ahudhurie sherehe za kuapishwa kwake.

 

“Ikabidi Mwalimu atoke Ulaya na kwenda moja kwa moja Afrika Kusini pasipo kupita Dar es Salaam. Mwalimu aliuchukulia mwaliko ule kama heshima kubwa kwake na alikuwa akizungumza kwa furaha sana kuhusu kuvunjwa kwa utawala wa makaburu, alisema Mwakyusa ambaye alikuwa daktari binafsi wa Mwalimu wakati huo.

Leave A Reply