The House of Favourite Newspapers

Flora imarisha ndoa yako, injili itanoga kweli!

0

mbashaaaaBWANA Yesu asifiwe dada yangu! Habari za siku nyingi na pole na mishemishe zako za kila siku, Mungu ni mwema, natumai anazidi kukubariki na unazidi kupambana na maisha.

Binafsi namshukuru Mungu, sijambo naendelea na shughuli zangu kama kawaida. Hofu na mashaka ni kwako wewe uliye mbali na mboni za macho yangu.

Dhumuni la barua hii ni kutaka kuzungumza na wewe juu ya mustakabali wa muziki wako wa Injili ambao mimi pamoja na Watanzania wengi tumekujua kupitia kazi hiyo ya kumtumikia Mungu.

Mchango wako ni mkubwa sana dada yangu, kupitia muziki wako watu wamepata kubadilika. Wamepata uponyaji na kimsingi nyimbo zako zimekuwa faraja kwa wengi kwa nyakati tofauti. Wapo waliokuwa na majonzi, wamebarikiwa kwa kusikiliza nyimbo zako.

Umekuwa mfano wa kuigwa katika jamii. Umekuwa kiongozi wa kiroho kupitia nyimbo zako. Lakini yote hayo yalikuwa yakienda kwenye mstari kwani pia ulikuwa umeyatendea haki maandiko matakatifu, Mwanzo sura ya pili, mstari wa 18 yasemayo: “Si vema huyo mwanamume aendelee kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi, awe kikamilisho chake.”

Wewe ulikuwa msaidizi wa mumeo kipenzi, Emmanuel Mbasha. Ukawa kikamilisho cha Emma. Mlikuwa mkifanya kazi ya Mungu pamoja. Watu walizidi kubarikiwa kwa kusikiliza nyimbo zenu lakini pia walibarikiwa kuona ndoa yenu inasimama na nyinyi kutimiza maandiko.

Mlionesha kwa vitendo maandiko katika kitabu cha Mwanzo sura ya pili, mstari wa 24 usemao: “Hiyo ndiyo sababu mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake nao watakuwa mwili mmoja.”

Lakini baada ya ndoa yako kupata ‘ajali’, mambo hayaendi kama zamani. Uzuri wa Injili yako kidogo unakosa ile ladha ya awali. Watu walizoea kuwaona mkiwa pamoja na mumeo jukwaani. Mkiimba na kucheza nyimbo zenu kwa staili ya kuvutia.

Waliozoea ‘kapo’ yenu wanaimisi kwelikweli. Wanatamani  hata leo mmalize tofauti zenu na muishi kama zamani. Muziki wenu utakuwa na maana kubwa sana. Tumefundishwa kusamehe saba, mara sabini kwani kwenu nini inashindikana kusameheana?

Bila kutafuta nani aliyekosa, mnaweza kuudhihirishia umma kwamba Mungu ni mwema na hakuna linaloshindikana chini ya jua. Kwamba mmepitia katika kipindi kigumu cha majaribu lakini mmeyashinda. Uzuri kupitia kazi yangu ya uandishi nimepata kuzungumza nanyi nyote wawili.

Wote mnaonesha mpo tayari kusameheana isipokuwa kila mmoja anajutia ‘sarakasi’ mlizopitia na kwamba nani atakubali kuonekana mkosaji kwa wakati huu. Biblia inasema mwanamke mpumbafu huivunja ndoa yake kwa mikono yake, wewe usikubali kuwa mpumbavu.

Bila kuangalia mlipojikwaa, mnaweza kuanza upya na Mungu akawaongoza mkaishi vizuri na muziki wenu ukawabariki wengi zaidi. Mungu akuongoze dada yangu!

Ni mimi kaka yako,

Erick Evarist

Leave A Reply