The House of Favourite Newspapers

Kalete utumbo wa mbu mjamzito!

0

Kuna kitu kimethibitishwa kisayansi wiki hii, kuwa Wabongo ndiyo namba wani kwa ushirikina Afrika nzima. Yaani hata Wanaijeria na muvi zao tunazoziona kumbe hakuna kitu, sisi ndiyo mabingwa.

Mi sibishi, kwani wiki iliyopita tu nililazimika kutumia mbinu hizo kumpata mdada mmoja ambaye alikuwa akihangaisha akili yangu sana tangu aanze kazi ofisini kwetu. Siku hiyo bosi kafungua mlango wa chumba cha ofisi yetu, akaingia na binti kaumbika hana hata kosa moja, bosi akatuambia kifupi tu, ‘Huyu ni mwenzetu mpya tutakuwa naye, mtafutieni sehemu ya kukaa’.

Kiukweli nilikuwa nimeduwaa tu naangalia alivyo bomba, alichosema bosi wala sikukisikia vizuri. Yaani mtoto mzuri, kavaa vizuri, pafyumu yake nzuri. Nilichanganyikiwa kabisaa ndugu zangu. Nilijitahidi kila njia anione kuwa nimemzimia, wimbo wa Ben Pol ulikuwa kinywani mwangu kila dakika, Nakuzimia Vibaya Vibaya, mara mbili nilimkaribisha lanchi lakini akaniambia hali mchana anaogopa kunenepa.

Ki ukweli mbinu zote nimetumia lakini binti anaonekana hana habari na mimi. Tuko ofisi moja lakini hakieleweki. Hatimae nikaona nitumie mbinu ambayo hata dunia nzima inaelewa sisi ndiyo mabingwa Afrika. Nikaona nimuendee huyu mtoto kwa mtaalam.

Sikupata tabu sana nilipomuuliza jamaa yangu mmoja kuwa nahitaji kukutana na mtaalam, akanitajia wataalam kama kumi hivi. Lakini kuna mmoja ndiyo akanihakikishia kuwa anafaa maana huyo jamaa ni mtaalam ambaye mafanikio yake yako wazi, ana mjumba wa ghorofa, magari ya kifahari, na hufuatwa kila anapokwenda na vimwana vya nguvu.

Nilikwenda kumuona, jamaa yuko kisasa sana ukifika unamkuta sekretari, unamlipa alfu kumi ya kujiandikisha kisha ndiyo anampigia simu Mzee, unakaribishwa kwenye chumba kilichopambwa kwa taa za rangi mbalimbali, Mzee mwenyewe alikuwa kakaa kwenye kiti cha mfalme.

Nikajieleza kuwa kuna binti ananisumbua akili, ningependa nipate kitu awe ananifuata kila mahala. Mtaalam akacheka sana na kunihakikishia kuwa atanipa dawa huyo binti atanifuata kila mahala. Kisha akaniambia cha kufanya ni mimi kumtumia bando ya intaneti kwenye simu yake, jina langu likionekana tu kwenye simu yake ningojee matokeo.

Haraka sana nikatuma kabando kanguvu kwenye simu ya mtaalam na kusubiri. Kesho yake nikashangaa, binti kanifolo kwenye Twitter, Facebook, WhatsApp, Imo, Instagram, telegram. Nikajua mambo sasa yameiva, lakini bado binti akawa haongei na mimi wala hataki ofa zangu. Nikamrudia mtaalam kumuuliza kulikoni.

Dah mtaalam akanijia juu, ‘We vipi? Si nilikwambia atakufwata kila mahala? Kakufwata  Instagram, Facebook, WhatsApp na kwingine unalalamika nini?’ Nikabaki mimacho kodo.

‘Mi nilitaka anifwate nyumbani kwangu’. Mtaalam akacheka, ‘Sasa mbona hukusema mwanzo? Haya kalete utumbo wa mbu mjamzito, na kucha za nzi mtoto nikufungie kazi’.

Leave A Reply