The House of Favourite Newspapers

Hakimu Atuhumiwa Kupokea Rushwa 150,000/=

0

HAKIMU mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Magugu,  Adeltus Richard Rweyendera, amefikishwa mahakamani na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.

 

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara, Isdory Kyand,o amesema mtuhumiwa huyo alipokea rushwa hiyo kutoka kwa wazazi na ndugu wa washtakiwa wanne ambao walikuwa wanashtakiwa kwenye kesi namba 242/2020 ikiwa ni kishawishi cha kuwasaidia na kuwaachia washtakiwa hao kwenye kesi tajwa ambayo alikuwa anaisikiliza.

 

Kyando amesema awali TAKUKURU  ilipokea taarifa kutoka kwa wasiri ikifafanua kuwa hakimu aliomba kiasi hicho cha fedha akiwataka wazazi na ndugu wa washtakiwa hao wachangishane.

 

Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, walifanya uchunguzi wa kina na kubaini ni kweli kesi tajwa ilikuwepo katika mahakama ya mwanzo Magugu na kwamba kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na hakimu huyo huku kesi hiyo ikitajwa mara kadhaa bila kusikilizwa tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza tarehe 3/8/2020.

 

Uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa wananchi hao walikamatwa kwa tuhuma za uzururaji miongoni mwao wakiwa kwenye maeneo yao ya biashara. Hata hivyo, TAKUKURU walibaini kuwa hakimu huyo aliwataka washtakiwa wote wanne wachange kiasi hicho cha fedha.

 

Kyando amesema baada ya kujiridhisha na ukweli huo maafisa wa Taasisi hiyo, waliandaa mtego wa rushwa na kufanikiwa kumkamata hakimu akiwa amepokea kiasi cha shilingi 150,000 fedha ambazo aliziweka kwenye droo ya meza yake mara baada ya kuzipokea.

 

Aidha TAKUKURU imemuunganisha kwenye mashtaka  Issaya Kiluma ambaye alikubaliana na hakimu huyo kutoa rushwa hiyo akichangia jumla ya shilingi 40,000 ikiwa ni sehemu ya shilingi 150,000/= ambazo hakimu alikamatwa nazo.

 

Kyando ameongeza kuwa Kiluma alikuwa miongoni mwa ndugu wa washtakiwa ambaye alikubaliana na hakimu kutoa kiasi hicho cha fedha pasipo kutoa taarifa TAKUKURU. Amesema kuwa mwananchi huyo ataunganishwa kwenye mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa rushwa ambapo kosa hilo lina uzito sawa na kosa la kupokea rushwa.

 

Kwa upande mwingine taasisi hiyo imetoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Manyara na Watanzania kwa ujumla kuacha kuwashawishi na kutoa rushwa kwa watumishi wa idara ya mahakama na kwingineko kokote na pale wanapoombwa rushwa wasisite kutoa taarifa katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo kote nchini.

 

Aidha,  amewataka watumishi wa idara ya mahakama ambayo ni wadau wakubwa wa mapambano dhidi ya ya rushwa na ambao wanafanya kazi muhimu ya kusimamia haki za Watanzania kuhakikisha kuwa wanawasimamia ipasavyo watumishi wachache ambao siyo waadilifu na kuwachukulia hatua stahiki pale inapothibitika kuwa wamejihusisha na vitendo hivyo.

Leave A Reply