The House of Favourite Newspapers

Harmo Asibezwe, ni Fundisho Tosha

0

MSANII wetu hapa Tanzania, Harmonize au Konde Boy Mjeshi au Harmo amekuwa akibezwa na baadhi ya watu, hasa baada ya hivi karibuni kufanya ziara nchini Marekani na shoo kufanyika jijini Columbus, Ohio na kwa video tulizoziona ni kweli kabisa shoo ilikuwa na watu wachache na kuzua minong’ono mingi, wengine wakiponda shoo zake.

Mara baada ya ziara hiyo, sasa Diamond Platnumz ameaza ziara hukohuko Marekani kuanzia Oktoba 8, 2021 kisha atakwenda Ulaya kwa ajili ya shoo ambapo tunaweza kusema anapishana na msanii mwenzake, Harmonize.

Jambo muhimu ambalo hakika hawaelewi wapinzani wa Harmonize ni kwamba, Harmo ni bonge la msanii hapa nchini na mimi nampa namba tatu kama siyo namba mbili kwa ukubwa hapa Bongo ukiachana na Diamond na King Kiba anayefuatia ni yeye.

Sasa kama msanii wetu mkubwa namna hiyo anakwenda nje kufanya shoo wanajitokeza watu na kumponda, hiyo inasaidia nini kwa wasanii wetu?

Katika soka, Harmo tunaweza kumfananisha na timu kama Simba au Yanga au Azam, sitasema Mondi ni timu gani au King Kiba ni timu gani, lakini hizo ni timu tatu kubwa zaidi Bongo kwa mfano zinaenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika halafu ziishie hatua ya mtoano; yaani hata raundi ya makundi zisifike hiyo inatoa picha gani kwa soka la Bongo? Na je, inakuwa ni aibu ya nani? Timu peke yake au Taifa?

Wapinzani wa Harmonize hawachukulii uzito ziara yake Marekani. Wanaona ni suala la Konde Boy tu na Konde Gang yake, lakini kiukweli ziara ile tuhusishe suala zima na tasnia nzima ya muziki wa Bongo Fleva.

Matukio kama hayo ya kukosa watazamaji kwenye shoo inatakiwa yawashtue wapenzi wote wa muziki wa Kizazi Kipya nchini.

Ni kama taarifa isiyo rasmi kwamba kwa mambo kumbe ni tofauti na tunavyodanganyana hapa nyumbani na views na trends za YouTube.

Mambo ni tofauti kwa sababu watu tunaotamani wawe wapinzani wetu; yaani wasanii wa muziki kutoka Nigeria wameshavuka hatua hizo kabisa.

Wakati hivi karibuni Hamronize anapiga shoo yake huko Marekani, wiki moja nyuma, Burna Boy alijaza Ukumbi wa O2 Arena jijini London, Uingereza.

Uwanja huo unasemekana unaochukua zaidi ya watu 20,000 na wote hao walilipa viingilio kuangalia shoo hiyo.

Burna Boy mwenyewe alikuwa anatamba kwenye ukurasa wake wa Instagram kwani alidai; “Nimejaza O2 Arena peke yangu, kwa bei ninayoitaka mimi.”

Siyo Burna Boy, Msanii mwingine Wizkid pia atapiga shoo hapohapo O2 Arena Novemba 18, mwaka huu na mpaka hivi tunavyozungumza tiketi zote za shoo hiyo inasemekana zimeshauzwa.

Na si kuuzwa, ziliuzwa na kuisha ndani ya siku mbili! Na kumbuka hiyo ni shoo inayofanyika nje ya Nigeria na ni mbali kabisa na nyumbani kwao.

Hapa nyumbani kwa wanamuziki wana upinzani na upinzani ni mzuri. Kwa sababu upinzani unasaidia kunogesha gemu na kukuza muziki, lakini tukiwa na upinzani usio na macho, kwamba hata kwenye mambo ya kujenga tunaleta mambo ya uko timu gani unadhani tutafika tunakokusudia?

Ndiyo matokeo yake tutakuwa tunaitana wasanii wakubwa humu ndani halafu tukitoka nje, tukienda kwenye maeneo ya watu tunaonekana si lolote kwenye tasnia hiyo.

Ni kama vile mwanafunzi darasani ambaye huwa ni mbumbumbu anayeshika namba moja kwenye darasa lenye mambumbu wengi. Ni namba moja sawa lakini ni mbumbumbu, ila akiwa na mambumbu wenzake yeye mwamba! Lakini akitoa mguu nje ya darasa tu, ni mwanafunzi zero.

Shoo ya Harmonize iwe funzo. Na kama tutajitia upofu wa kuona kila kitu kipo sawa tutegemee kuona muziki umeganda hapahapa tulipo sasa hivi au ukaporomoka zaidi.

Ni lazima wanamuziki na timu zao wafanye wawezalo ili muziki wetu upenye hadi huko kwa wenzetu.

Tusiue muziki wetu sisi wenyewe, lazima tujiulize sababu za watu kutojaa kule Marekani. Je, kwa nini Uarabuni watu wanajaa kwenye shoo za wanamuziki kutoka hapa nyumbani.

Kwa vyovyote kuna kazi ya kufanya ili muziki na wasanii wetu waweze kupaa juu zaidi.

Mwaka huu wimbo wa Harmonize uendao kwa jina la Attitude ndani yake ukiwa amewashirikisha mwanamuziki kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Awilo Longomba na msanii H Baba wa Tanzania ameonesha njia mpya. Awilo siyo mtu wa kubeza na naamini hiyo itasaidia Harmo kuwa wa kimataifa zaidi.

Wasanii wa Nigeria mbali ya kufanya muziki mzuri pia wamekuwa wakifanya vizuri katika anga za kimataifa ikiwemo kuongoza kuzoa tuzo kwa nchi za Afrika zikiwemo zile za Grammy walizopata hivi karibuni kwa wanamuziki wao Wizkid, Davido na Burna Boy. Tunataka Harmo naye afike huko na siyo yeye tu, bali tuone wengine wengi.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Leave A Reply