The House of Favourite Newspapers

Harmonize: Msipoteze Bando Lenu Kunipigia Kura

0

 

STAA wa muziki wa kizazi kipya nchini Rajab Kahali maarufu Harmonize ametangaza rasmi kutozitambua tuzo zinazoendelea hususani African Entertainment Awards USA (AEAUSA) alizotajwa kama mmoja wa wasanii wanaowania tuzo hizo mwaka huu.

 

Harmonize ameutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kuandika ujumbe kupitia Insta story yake, unaomaanisha kuwa kwa sasa hayuko tayari kuwasumbua mashabiki wake kuhangaika kumpigia kura kwa kuwa yeye mwenyewe hayuko tayari kushiriki kwenye tuzo hizo.

 

“Sijateuliwa kuwania tuzo yeyote kwa hivyo tafadhali usipoteze kifurushi chako cha Internet kunipigia kura, hii ni kwa wanachama wa Konde Gang pekee” ameandika Harmonize.

 

Msanii huyo ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani kwa ziara yake ya kikazi ameyasema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa kwa majina ya wasanii walioteuliwa kuwania tuzo za African Entertainment Awards USA ambazo msanii huyo ameteuliwa kwenye vipengele kadhaa ikiwamo cha msanii bora wa kiume. Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (Best Male Artist – East/South/North Africa).

 

Kitendo hicho kimeibua sintofahamu kwa mashabiki wa Harmonize kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakijadili kuwa pengine kujiengua kwa msanii huyo kumekuja kufuatia kutopangwa kwake kwenye vipengele kama msanii bora wa kiume, msanii bora wa mwaka nk.

 

Vipengele hivyo vimeshikiliwa na wasanii kama Burna Boy, Davido, Wizkid, Facolistic, Shatta Wale, Stonebwoy, Diamond Platnumz na wengine kadhaa ambao wanatajwa kuwa pengine wana hadhi moja na msanii huyo.

Leave A Reply