The House of Favourite Newspapers

Harusi ya Nandy, Billnass Usipime!

0

MAMBO ni moto! Ndiyo maneno yanayotamkwa mtaani kwa sasa kutokana na habari kueleza kuwa, harusi ya mastaa wa Bongo Fleva; William Lyimo ‘Billnass’ na mchumba wake, Faustina Charles ‘Nandy’ itakuwa ya aina yake, Risasi Jumamosi limedokezwa.

 

Harusi hiyo ambayo mipango yake kabambe inaendelea, inaelezwa kuwa itakuwa ya kipekee kwani imeshaanza kuvuta hisia za Watanzania wengi na wadau wa tasnia ya burudani hasa baada ya Billnass kumvalisha Nandy pete ya uchumba hivi karibuni.

 

Habari kutoka kwa chanzo kilicho ndani ya familia, zinaeleza kuwa maandalizi ya ndoa yake ni ya kukata na shoka maana bajeti yake ni kubwa na inatarajiwa kuhudhuriwa na watu maarufu kutoka ndani na nje nchi.

 

“Yaani ndoa ya Nandy na Billnass usipime, kwani imeandaliwa mikakati kabambe kwa lengo la kuifanya kuwa ya kihistoria na ya kipekee.

 

“Wawili hawa wameipanga harusi yao kitambo kabisa yaani waliiandaa kuwa harusi kubwa na wala wasingechukua muda hata kidogo baada tu ya kuvalishana pete, lakini huu ugonjwa wa Corona ndiyo umetibua kila kitu,” kilisema chanzo hicho.

 

Kwa upande mwingine, chanzo kilizidi kutiririka kuwa, wawili hao kutokana na kila mmoja kuwa na mapenzi ya dhati kwa mwenziye, wamepanga harusi hiyo kuwa ya tofauti kabisa na mastaa wengine waliowahi kufunga ndoa.

 

“Wametenga bajeti ya zaidi ya milioni 100 ambayo itatosha kuhakikisha watu wanakula na kusaza, wanakunywa, lakini pia wamepanga kuifanya harusi yao katika hoteli moja kubwa hapa nchini yenye hadhi ya nyota tano, kwa sababu wamenishirikisha kila kitu kuhusu mipango hiyo,” kilisema chanzo.

 

Ili kuleta utamu wa habari, Risasi Jumamosi lilimtafuta Nandy na kumuuliza kuhusiana na maandalizi ya ndoa yao hiyo ambapo alisema, wanatamani harusi yao kuwa ya tofauti na nzuri kabisa ambayo itaweka historia ndani na nje ya nchi.

 

“Mungu ni mwema, natamani ndoa yetu iwe ya tofauti kabisa na ninamshukuru sana Mungu kwa sababu jambo la kwanza limetimia na hili la ndoa naamini atatuwezesha litimie. Harusi yetu itakuwa ya tofauti kabisa,” alisema Nandy.

STORI: KHADIJA BAKARI, RISASI

Leave A Reply