The House of Favourite Newspapers

Hata Uwe Bilionea, Bila Mambo Haya Hujafanikiwa!

Amancio Ortega raia wa Spain

Na AMRANI KAIMA| GAZETI LA IJUMAA| SAIKOLOJIA, MAISHA NA WEWE

Huko mtaani kuna dhana ambayo imejengeka katika baadhi ya vichwa vya watu kwamba, kuwa na mabilioni ya pesa ni kufanikiwa. Kwa kuzingatia dhana hii, baadhi ya watu hufikia hatua ya kutafuta pesa kwa udi na uvumba lakini wanapozipata hawazifanyii kitu na kuamua  kuzilimbikiza kwenye akaunti zao, lengo ni ili wawe mabilionea.

Sawa! Kuwa bilionea ni sifa katika jamii, lakini ubilionea huo bila kufanya mambo yanayoonekana na kuifanya hata jamii inayokuzunguka kufaidika na fedha zako utakusaidia nini katika maisha yako?

Nasema hivyo kwa sababu wapo watu huko mitaani wanazo fedha nyingi tu, lakini ukiambiwa wana pesa huwezi kuamini kutokana na jinsi walivyo. Ni wabahili, wagumu wa kusaidia jamii na wagumu pia wa kufanya mambo ya kimaendeleo.

Niseme tu kwamba, pesa ni muhimu sana katika maisha ya binadamu, ukiwa na pesa unao uwezo wa kufanya lolote ambalo utalipanga katika akili yako, liwe zuri ama baya.

Si hivyo tu, pia ukiwa na pesa utaheshimika kwa watu wengi, lakini kama tu utakuwa mtu wa kuwajali, kuwaheshimu na kuwapenda wengine ambao wako chini yako.

Huwezi kuheshimika kama utakuwa na pesa kisha ukawa na tabia ya kujiona, kudharau watu wenye hali duni. Ukifanya hivyo ni dhahiri watu hao watakuchukia na mwishowe hutaona raha ya kuwa na pesa.

Carlos Slim Helu – Bilionea raia wa Mexico

Tunapozungumzia mafanikio, hatuna budi kufahamu kuwa ni neno pana kidogo. Ni sawa kwamba kuwa na pesa ni sehemu ya kufanikiwa katika maisha ila sasa, ukiwa na pesa nyingi ukashindwa kuzifanyia kitu cha maana huwezi kuwekwa katika kundi la watu waliofanikiwa.

Kila mtu ana malengo katika maisha. Kuna ambaye atakuambia; ‘Leo hii nikipata shilingi milioni mia moja nitajenga nyumba na kununua magari’. Lakini kuwa na magari ya kifahari, nyumba, mke ama mume mzuri ni kufanikiwa?

Jibu kwa walio wengi ni kwamba kuwa na magari, nyumba ya kifahari, mke ama mume mzuri pamoja na watoto ni kufanikiwa, lakini ukweli wenyewe ni kwamba kufanikiwa ni zaidi ya kuwa na vitu hivyo.

Kisaikolojia kuwa na vitu hivyo ni sehemu ya mafanikio tu kwani kuna vitu vingine vya msingi sana kwa binadamu ili aweze kuwa katika mafanikio kamili. Maisha ya binadamu bila kutawaliwa na furaha, upendo kutoka kwa watu wanaomzunguka pamoja na amani ya moyoni hawezi kuchukuliwa kama aliyefanikiwa.

Ukichunguza kwa undani utakuta baadhi ya watu wenye fedha na mali nyingi hawana furaha katika maisha yao kama wanavyotaka wao. Wanakosa furaha kwa sababu muda mwingi wanakuwa na hofu na wasiwasi juu ya mali zao.

Kutokana na baadhi ya watu kuamini kwamba kuwa na pesa ni kufanikiwa, hulazimika kufanya kadiri wawezavyo ili waweze kuzipata. Watadhulumu, wataua na kuiba ili wafanikishe azma yao ya kufanikiwa, bila kujua kwamba kwa kufanya hivyo ni sawa na kujiibia, kujidhulumu na hata kujiua. Kamwe wanaofanya hivyo hawawezi kuwa na maisha ya furaha.

Kwa kuthibitisha hili, jaribu kuchunguza maisha ya watu ambao hujipatia pesa kwa njia haramu, wengi wao maisha yao yamejawa na hofu na mabalaa ya hapa na pale lakini wanakuwa wavumilivu na walio nje hawawezi kujua hayo.

Maisha yao yanakuwa ya wasiwasi kwa sababu wanajua kwamba siku yoyote mambo yanaweza kugeuka na kuwa mabaya bila kutarajia. Waliojipatia pesa kwa njia ambazo siyo halali ni vigumu kuwakuta wakiwa na maisha ya furaha ndani ya nyumba.

Utawakuta wakikorofishana na wake ama waume zao kila siku, hali ambayo huwafanya wakose upendo maishani mwao, kukosa amani katika mioyo yao pamoja na kupungukiwa na furaha kiasi cha kuwafanya wasiwe katika kundi la waliofanikiwa.

Tufahamu kwamba hatuwezi kusema tumefanikiwa katika maisha yetu kama hatutakuwa tumejihakikishia furaha, upendo na amani katika mioyo yetu.

Unapokuwa na pesa nyingi na mali ya kutosha, utakuwa umekuwa tajiri ambapo kwa tafsiri ya haraka waliotajirika ndiyo waliofanikiwa, lakini ukweli ni kwamba ukiwa tajiri bado hujafanikiwa na ili uweze kufanikiwa jitafutie mambo hayo matatu ambayo ni amani, upendo na furaha, hapo ndipo unaweza kusema una mafanikio makubwa

Comments are closed.