The House of Favourite Newspapers

Hongera madam, washiriki mnaandika lakini?

0

wema (3)
KWAKO Mkurugenzi wa Benchmark Production, Rita Paulsen ‘Madam’ habari za siku dada yangu? Vipi uko poa? Pole na hongera kwa kazi nzito unayoifanya kwa ajili ya vijana wetu wa Kitanzania kupitia Shindano la Bongo Star Search (BSS). Umewapa fursa ya kuonekana, kujitangaza, hii ni zaidi ya shindano la kuonesha vipaji.

wema (1)Binafsi mimi ni mzima, namshukuru Mungu. Naendelea kupambana katika uwanja wangu wa habari na leo nimekukumbuka kupitia barua ili niweze kuzungumza na wewe pamoja na washiriki wa BSS kwa ujumla.

Dhumuni la barua hii kwanza kabisa ni kukupongeza Madam. Kwa takriban miaka nane sasa umeweza kuendesha shindano hilo ambalo binafsi siwezi kulibeza hata kidogo. Nikupongeze kwa kupata wazo la shindano hilo na kulifanyia kazi. Matunda yanaonekana.

Uzuri ni kwamba tumeona mabadiliko, kadiri miaka inavyozidi kwenda. Binafsi nimeguswa na namna ambavyo mwaka huu umejipanga! Kuanzia mnavyowaandaa washiriki na hata ukumbi, umenakshiwa vizuri, unavutia.

Natazama mashindano mbalimbali duniani ya aina yako, niwe mkweli, ukumbi wa mwaka huu ni ‘classic’. Maandalizi kwa jumla yanavutia, vijana mliowachuja ni kweli kabisa wanastahili kuwa mastaa wakali hapo baadaye.

Sanjari na pongezi zangu kwa Madam, niwageukie sasa washiriki. Niwaambie tu, nafasi adimu waliyoipata kupitia shindano hilo iwe chachu ya maendeleo yao. Iwe njia ya kufikia ndoto zao. Kwa washiriki ambao mmesalia, mnaonesha kabisa mna kitu ambacho Mungu amewapa.

Msikubali kipotee. Mara nyingi washiriki wanapotoka katika mashindano hayo huwa wanajisahau na kujikuta wamepotea. Fedha za ushindi mnazozipata zisiwazuzue, suala la msingi ni kutazama namna unavyoweza kujikwamua.

Kuonekana nchi nzima katika shindano hilo ni hatua muhimu, itumieni vizuri. Hakikisheni haipotei hivihivi. Sanaa ni ngumu. Changamoto yake ni kuhakikisha haukauki katika masikio ya watu. Kila siku unatakiwa kuwaza kitu cha kufanya katika muziki na kiwe kikali, kisikike.

Ubunifu ni sehemu ya maisha yenu. Hakikisheni mnakuwa wabunifu kila siku. Siku zote watu wasio wabunifu hugeuka kuwa walalamishi. Wanaopenda kulaumu ni wavivu. Nyinyi msiwe wavivu. Hata kama ikitokea hujashinda, ‘ujanja’ wako unaweza kukufikisha mbali.

Ukibweteka na kusema usubiri atatokea mtu wa kukubeba, imekula kwako. Fursa unatakiwa uzifuate na zikufuate wewe. Vyombo vya habari pia usiviache vikufuate, vifuate wewe na uvioneshe ulichojaaliwa.

Wadau wa muziki uwafuate, usisubiri wakufuate. Ukifanikiwa kuanza kusikika katika vituo vya redio na televisheni, usizubae, changamka. Ongeza juhudi zaidi katika ubunifu na maisha yako kila siku yatakuwa ni ya kufanya muziki mzuri utakaopata wasikilizaji kila kukicha.

Mkizingatia hayo nina imani kupitia miongoni mwenu, miaka inayokuja tutaandika historia kwa kuwa na staa mkubwa ambaye ni zao la BSS 2015, Mungu awaongoze katika kazi yenu, hakika mtafika mbali.

Ni mimi mwenzenu katika ujenzi wa taifa,

Erick Evarist

Leave A Reply