The House of Favourite Newspapers

Huyu ndiye Mopao Mokonzi? Je, atapona? Tusubiri!

0

JINA lake halisi ni Antoine Christophe Agbepa Mumba lakini wengi tunamjua kwa jina la Koffi Olomide au Le Grand Mopao Mokonzi.

Ni maestoro wa muziki wa Rhumba barani Afrika akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Nchini Tanzania Koffi anafahamika tangu enzi zile za Effrakata kisha Ekotite na Papa Ngwasuma. Mara ya mwisho kuonekana Bongo ni siku ile ya Kilele cha Wiki ya Wananchi (Yanga), Agosti 29, 2021 alipopiga shoo ya kukata na shoka kwenye Dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar.

 

Kwa sasa ana makazi nchini Ufaransa; koloni la Kongo. Mopao ni miongoni mwa wanamuziki wa Afrika matajiri waliouza albam nyingi zaidi Ulaya na anaendelea kuwavutia wengi kwenye kumbi za burudani.

 

Lakini katika siku za hivi karibuni amerejea kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kwa namna hasi ambayo haina afya kwenye muziki wake akiandamwa na majanga juu ya majanga.

 

Kubwa ni kesi yake nzito iliyopewa jina la Le Grand Mopao ambapo wanenguaji wa kike wanne wa zamani wamemshitaki.

 

Koffi mwenye umri wa miaka 65 anashtakiwa kwa kuwadhulumu kingono na kuwabaka wanenguaji wanne wa kike waliokuwa wakicheza dansi wakati walipofanya naye kazi kwenye tamasha nchini Ufaransa.

 

Mwaka 2009, Koffi alikimbia Ufaransa na kurejea Kongo, lakini aliahidi kujitetea dhidi ya madai hayo.

 

Mwaka 2012, alihojiwa kuhusu tuhuma za ubakaji wa wanenguaji hao wanne, hakufungwa, lakini baadaye mahakama ya Paris, Ufaransa ilimhukumu kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumnyanyasa kingono mtoto wa miaka 15 kama ilivyo kwa mwanamuziki mkubwa duniani R Kelly wa Marekani ambaye anasota rumande na huwenda akaenda na maji kwenye hukumu ya kesi hiyo.

 

Koffi aliamriwa kulipa faini ya Euro 5,000 na riba kwa mmoja wa wanenguaji wake. Mahakama ya Nanterre nchini Ufaransa pia ilimuamuru kulipa faini sawa na hiyo kwa kuwasaidia wanawake watatu kuingia Ufaransa kinyume cha sheria.

 

Wizara ya Utawala ambayo ilikuwa imeomba afungwe kwa miaka saba, ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

 

Koffi ambaye mara kadhaa amekuwa akisema hadharani kuwa ananyanyaswa, anaendelea kukanusha tuhuma za ubakaji.

 

Mwaka 2019, aliiambia TV5 Monde kuwa; “Ilimradi nikumbuke kuwa nimekosea na ninatumai kuwa siku moja wanawake hawa watakuja na kusema kwamba wamedanganya kuhusu madai hayo.”

 

Mashtaka dhidi yake yanawezekana kuwa yalifanyika wakati wa matamasha nchini Ufaransa kati ya mwaka 2002 na 2006.

 

Wanawake hao wanamshutumu kwa kuwapa hifadhi katika nyumba iliyo karibu na Paris na kuwalazimisha kufanya naye mapenzi, ili baadhi yao waweze kudumu kukaa hapo.

 

Mbele ya majaji, Koffi alikanusha mashtaka hayo, akidai kuwa wanawake hao ‘walisafiri kwenda na kutoka Champs-Elysees na wakati mwingine ‘walidai wasindikizwe’.

 

Waendesha mashtaka wanasema walisindikizwa kwa nguvu. Koffi alithibitisha kuwa ana haki ya kuwasimamia walipoondoka ili kuhakikisha kuwa hawatoroki Ufaransa kutokana na kazi waliyokuwanayo.

 

Anasema madai hayo yametungwa na wanawake hao wanne wanaotafuta namna ya kuendelea kuishi Ufaransa.

 

Kuhusu jinsi wanawake waliotoroka kutoka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi na kwenda kuandamana, mwimbaji huyo alijibu; “Hiyo ni sinema tu…muda wao wa kurudi Kongo ulikuwa karibu, walijua kabisa kwamba wanarudi Kongo. Kwa hivyo walitaka kukaa Ufaransa kwa gharama yoyote,” anasema Mokonzi.

 

Wanawake hao wanasema hawajaweza kurejea Kongo kwa kuhofia kulipizwa kisasi kwani mwanamuziki huyo anafahamika kwa ubabe.

 

Koffi pia alikanusha madai ya ubakaji. Wanawake hao wanasema wakati f’lani aliwaalika hotelini, wakati mwingine katika studio ya muziki na kuwalazimisha kufanya naye mapenzi.

 

Koffi alikana kwa kusema; “Hapana, sijawahi kuwa peke yangu na hawa wasichana, unawezaje kufanya mapenzi studio? Siwezi kuwafikia!

 

“Hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai yaliyotolewa na washtaki hawa.”

 

Mahakama ilisema itatangaza uamuzi wake Desemba 13, mwaka huu; hofu kubwa ikiwa ni huwenda msala huo mzito ukamtumbukiza kwenye yanayomkuta R Kelly.

 

Sheria inasemaje unyanyasaji wa kijinsia kwa mtoto wa miaka 15 nchini Ufaransa?

 

Chini ya sheria ya makosa ya jinai nchini Ufaransa, ni kosa kwa mtu mzima, kutumia au kufanya ngono na mtoto wa miaka 15 hata kama hukutumia nguvu yeyote.

 

Endapo akipatikana na anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela na faini ya Euro 100,000.

 

Tayari Koffi ametoa wimbo mpya kuwaomba msamaha akina mama barani Afrika. GETTY IMAGES

 

Mbali na kesi hiyo Koffi ana kesi nyingine zinazomkabili nchini Ufaransa ambapo mwaka 2012 alifungwa gerezani kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kushtakiwa kumpiga na kumuumiza mtayarishaji wa muziki.

 

Kwa upande wake, Koffi anasema madai yote ni uzushi; “Sijawahi kumpiga mtu au kumbaka mtu au kubaka watu.”

 

Kesi yake ambayo itasikilizwa Desemba 13,mwaka huu inaweza kuathiri kazi yake ya muziki kama atapatikana na hatia. KOFFI

 

Mwaka 2018 nchini Zambia, Koffi alishtakiwa kwa kumuacha mpigapicha wake.

 

Mwaka 2016 alikamatwa jijini Nairobi, Kenya na kurudishwa kwao baada ya kumpiga mateke mnenguaji wake wakati anawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

 

Mwaka 2008 Kofi alituhumiwa kwa kumpiga mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha RTGA cha nchini Kongo na kuharibu kamera yake, lakini baadaye walipatana nje ya mahakama.

 

Makala; Elvan Stambuli, Bongo

Leave A Reply