The House of Favourite Newspapers

Jide Amekuwa Mlezi wa Wana!

0

JUDITH Wambura Mbibo almaarufu Lady Jaydee au Jide, ni mwanamuziki mkongwe kwenye gemu la Bongo Fleva.

Kipaji chake kiligundulika akiwa na umri wa miaka saba tu!

Ni Binti Komando anayestahili kupewa sifa ya kuwa Malkia wa Nguvu.

Historia yake kwenye muziki huu, inamfanya kuwa mwanamuziki wa kike wa Bongo Fleva ambaye hajaondoka kwenye ramani na ana ushawishi mkubwa.

Jide amekuwa ni mwanamuziki wa kike wa kwanza kufanya RnB kwa lugha ya Kiswahili.

Miaka 18 iliyopita (2002), alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike wa Bongo Fleva kushinda Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike wa Tanzania na kutumbuiza kwenye tuzo kubwa Afrika, Kora.

Amebeba tuzo kibao. Mwaka 2004 alishinda Tuzo ya Albam Bora ya RnB kwenye tuzo za muziki Bongo. Mwaka uliofuata alishinda Tuzo ya Video Bora Kusini mwa Afrika.

Mwaka 2014, alishinda Tuzo za AFRIMMA zilizotolewa Texas, Marekani akiibuka Mwanamuziki Bora wa Kike Afrika Mashariki.

Jide ndiye mwanamuziki wa kike wa Bongo Fleva mwenye ngoma (hits) nyingi na Albam 7 nzito sokoni zilizofanya vizuri kila kipindi alichozitoa.

Albam zake ambazo alitamba nazo na kufanya vizuri ni Machozi ya mwaka 2000, Binti ya mwaka 2003, Moto ya mwaka 2005, Shukrani ya mwaka 2007, The Best of Lady Jaydee ya mwaka 2012, Nothing But The Truth ya mwaka 2013, Woman ya mwaka 2017 na habari njema ni kwamba, anakuja na albam yake ya nane itakayokwenda kwa jina la 20 akiwa ametimiza miaka 20 kwenye gemu.

Kuonesha kwamba Jide ni mwamba, platform (jukwaa) kubwa inayojihusisha na biashara ya muziki, iliainisha mambo kumi ya Jide ambayo watu hawayajui;

Hadi sasa Jide amefanikiwa kurekodi nyimbo takriban 170 huku kolabo zikiwa ni 97 hadi 100.

Tangu aanze muziki, Jide ameshinda jumla ya tuzo 35 kutoka Tanzania na kimataifa.

Albam mbili za mwanzo za Jide; Machozi na Binti, alizirekodi akiwa anasimamiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Media Group, marehemu Ruge Mutahaba.

Jide huwa hapendi kusaini mikataba ya kusimamiwa kimuziki, huu ni ushauri aliopewa na gwiji wa muziki Afrika, marehemu Oliver Mtukudzi.

Albam ya kwanza ya Jide ya Machozi, yote ilirekodiwa MJ Records na Producer Master J.

Kwa mara ya kwanza, Jide alikutana na Will Smith jijini London, Uingereza kwenye birthday ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela. Hiyo ndiyo sababu Will Smith alipokuja Tanzania, alimtaja Jide kama mwanamuziki pekee anayemfahamu.

Jide ana mchango mkubwa kwa Malkia Karen (mtoto wa aliyekuwa mumewe, Gardner G Habbash) kuingia kwenye muziki kwa kuwa aliishi naye na aligundua anapenda muziki alipokuwa na umri wa miaka 7.

Kabla ya kuingia kwenye muziki, Jide alikuwa akifanya kazi Zanzibar, Tembo Hotel na Kiwanda cha Sigara (TCC).

Taaluma pekee ya Jide aliyosomea kwenye maisha yake, ni Uandishi wa Habari kwenye Chuo cha Times School of Journalism (TSJ) cha jijini Dar.

Akiwa bado mtangazaji wa Clouds FM, Jide ni miongoni mwa wanamuziki walioshiriki kwenye wimbo wa maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

KOLABO

Imezoeleka kumuona Jide akifanya kolabo kali na wakongwe wenzake kwenye muziki. Lakini hivi karibuni zimeibuka kolabo kali ambazo Jide amefanya na wasanii wa umri mdogo kiasi cha kupewa jina la mlezi wa wana;

WIFE-HARMONIZE FT LADY JAYDEE

Wife ni ngoma ya mwanamuziki na bosi wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide, Rajab Abdul ‘Harmonize’, ambayo iliachiwa rasmi Juni 17, mwaka huu kwenye Mtandao wa YouTube na kufanya poa kwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 2 kwa mwezi mmoja.

Kolabo hiyo ilitengeneza bonge moja la kemistri, kwani Jide alionesha ukongwe wake unavyozidi kuwika kwa kufanya kazi na Harmonize au Harmo ambaye yuko kileleni kwa sasa.

Ubunifu uliofanyika ndani ya video hiyo, umemfanya Jide kuendelea kubaki kileleni kama mwanamuziki anayeheshimiwa, maana Harmo hakuonesha yale madoido yake ya kumbambia dada yake huyo!

AMEN-RAPCHA FT LADY JAYDEE

Amen ni ngoma ya rapa mkali aliye chini ya Lebo ya Bongo Records akiwa amemshirikisha Jide. Ngoma hiyo iliachiwa Julai 18, mwaka huu na kufanya poa kwa kutazamwa mara zaidi ya laki mbili kwenye YouTube hadi sasa.

Kwenye ngoma hiyo, Jide amefanya poa kinoma kuonesha uwezo wake wa kuchana, kwani aliwahi kusema kuwa ni kitu alichokuwa akikifanya mwanzo kabla ya kuwa muimbaji.

Ndani ya ngoma hiyo, Jide ameonesha ubunifu wa hali ya juu kuanzia melodi hadi video, kwani sini zote ameonesha kufanya poa sana.

ASANTE -DOGO JANJA FT LADY JAYDEE

Asante ni ngoma mpya kutoka kwa mwanamuziki Abdul Chende ‘Dogo Janja’ ambayo amemshirikisha dada mkuu, Jide.

Ngoma hiyo imetoka hivi karibuni na imekuwa moto, kwani inakimbiza kwenye trending za YouTube na kushika namba kumi na moja ikiwa imetazamwa zaidi ya mara laki moja na arobaini hadi juzi, kwa kuwa kimefanyika kitu cha tofauti hasa kwenye mashairi yenyewe.

Mashairi ya ngoma ya Asante yamekuwa ni makali, hii yote ni kutokana na uwepo wa mkongwe huyo wa muziki kiasi cha kutengeneza bonge moja la kolabo nyingine kali kwenye Bongo Fleva.

Ngoma hiyo imepita kwenye mikono ya MJ Records chini ya Producer Daxo Chali. Inazungumzia shukrani na jinsi neno Asante lilivyo na ukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ubunifu mkubwa umefanyika kuanzia melodi hadi video ambayo imefanyika kwa Director Msafiri wa Kwetu Studios.

Mbali na hilo, Dogo Janja amekuwa ni msanii anayetoa hit kali, kwani mbali na Jide, tayari amefanya kolabo na mkongwe kama Hamad Ally ‘Madee’ na wengine.

SHOO NA ZUCHU

Julai 18, mwaka huu, Jide alifanya bonge moja la shoo akiwa na msanii mpya wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Othman ‘Zuchu’.

Zuchu alifanya shughuli kubwa kwenye Ukumbi wa Mlimani City akiwa anawashukuru mashabiki wake kwa kumpokea vizuri na EP yake ya I AM ZUCHU, alimpa heshima Jide kama dada yake aliyemzidi umri na muziki pia.

Wawili hao walipoungana, waliacha mvumo mkali kwa wapenda burudani, kwani ilikuwa ni bonge moja la shoo.

Habari ni kwamba, wawili hao wanatarajia kuachia bonge moja la ngoma.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply