Jini Mauti-6

ILIPOISHIA
Damu hazikukata, ziliendelea kutoka, hakuwa akisikia maumivu yoyote yale lakini damu zilitoka mfululizo hali iliyoonekana kumuongezea hofu kubwa. Hakutulia, akatoka na kuelekea katika sehemu moja iliyokuwa na baa fulani ambayo mpaka muda huo haikuwa imefungwa, akaingia na moja kwa moja kuelekea msalani. ENDELEA NAYO…

“Unakwenda wapi huko?” aliuliza msichana mmoja, alikuwa mhudumu katika baa hiyo.
“Msalani?” mama alijibu huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Wewe ni mteja?”
“Hapana.”

“Ila?”
“Nimepata tatizo! Nipo kwenye kipindi changu,” alijibu mama.
Mhudumu yule alimuelewa kwani hata na yeye alikuwa mwanamke, alichokifanya ni kumruhusu, alipofika mle ndani, akachukua maji na kujaribu kujiosha lakini kitu kilichoshangaza, damu hazikuweza kukatika, ziliendelea kutoka mfululizo kitu kilichomuongezea hofu kubwa.

“Nitafanya nini?” alijiuliza.
Baada ya dakika kadhaa, damu zile zikakata lakini tumbo likaanza kuwa kwenye maumivu makali, mama alilia huku akilishika tumbo lake lakini hali iliendelea kuwa vilevile. Hakutaka kukaa mle msalani, alichokifanya ni kutoka huku akiugulia maumivu.

Mhudumu yule alipomuona akamsogelea na kumuuliza tatizo lilikuwa nini, mama akamwambia kwamba alisikia maumivu makali ya tumbo hivyo akamchukua na kuanza kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.

Walipoanza kuondoka kuelekea huko hospitali, njiani mama alianza kuona mauzauza, kuna wakati alisikia sauti za paka wengi wakilia, tena kwa kuliita jina lake, wakati mwingine alikuwa akiwaona wakipita karibu nao na kila alipomwambia mhudumu yule kuhusu wale paka alibaki akishangaa kwani hakuwa akiwaona.

Mama aliogopa, mauzauza yale yalimfanya kugundua kwamba ulikuwa ni uchawi uliokuwa ukifanywa na bibi. Hakutaka kuzungumza kitu chochote zaidi ya kuendelea na safari. Walipofika hospitalini, kitu cha ajabu kabisa ambacho hawakujua nini kilikuwa kikiendelea, hakukuwa na mtu yeyote hospitalini hapo.

Ilikuwa ni hali ya kushangaza mno, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Hiyo ilikuwa ni hospitali ya halmashauri iliyokuwa ikifanya kazi saa ishirini na nne, sasa kwa nini isiwe na mtu ndani? Madaktari walikwenda wapi? Yaani hata wagonjwa wasiwepo? Kila walipojiuliza, walishindwa kuelewa.
“Mbona hakuna watu?” aliuliza yule mhudumu.

“Hata mimi nashangaa kwa nini.”
Walijaribu kuingia ndani ya hospitali ile, hakukuwa na mtu yeyote, waliingia ndani ya kila chumba, hakukuwa na mtu yeyote yule. Walibaki wakishangaa, hawakuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.

Wakayafuata mabenchi yaliyokuwa kwenye moja ya korido zilizokuwa mle ndani wakaketi. Bado mama aliendelea kugumia kwa maumivu makali ya tumbo, alishindwa kusimama.
Akaanza kumwaga machozi pale kwenye benchi, mhudumu yule ndiye aliyekuwa akimpoza kwa kumtaka kunyamaza.

“Wewe Stellah!” ilisikika sauti masikioni mwake, hapohapo akauinua uso wake na kuangalia mbele, bibi alisimama mbele yake huku mkononi akiwa na ule mkoba wa kichawi, mama akashtuka.
“Mama!”
“Chukua huu mkoba.”

“Mama sitaki, sitaki kuwa mchawiiii…”
“Nimesema chukuaaa…”
“Sitakiii…”

Mama alipiga kelele, hapohapo bibi akapotea na mkoba wake, kitendo cha kupotea tu, tayari yale maumivu ya tumbo aliyokuwanayo yakapotea ghafla na kuwa mzima kabisa. Mhudumu yule akabaki akimshangaa, kelele alizokuwa akizipiga alizisikia lakini suala la uchawi hakuwa akilijua.
“Vipi?”

“Abeee.”
“Umesema hutaki kuwa mchawi?”
“Ndiyo!”
“Ulikuwa unamwambia nani?”

Mama hakujibu swali hilo, alichokifanya ni kusimama na kuanza kukimbia kuelekea barabarani. Mhudumu yule alimshangaa, hakumuelewa mama, wakati mwingine alionekana kama chizi. Hakutaka kujali sana, kwa kuwa hakuwa akimfahamu, akaamua kumuacha.

Mama alikimbia mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na giza, pembeni kulikuwa na miti mingi, alipofika hapo, akaufuata mti mmoja na kukaa chini yake. Alibaki akilia tu, hakuamini kama kweli mama yake alikuwa mchawi.

Hakulala usiku kucha, alikuwa mtu wa kulia tu. Sauti za paka zilikuwa zikisikika kila kona, aliogopa sana.

na sauti hizo ndizo zilizomfanya kutokulala kabisa. Hakukuwa na siku ambayo aliishi kwa hofu kubwa kama siku hiyo.

Mpaka inafika asubuhi, alikuwa machoz, akainuka na kuanza kuondoka mahali hapo. Lengo lake siku hiyo lilikuwa ni kwenda Dar es Salaam, hakutaka kuendelea kubaki Lushoto kwa kuamini kwamba kadiri ambavyo angeendelea kubaki huko basi bado angeendelea kufuatwafuatwa na bibi.


Loading...

Toa comment