Kakolanya Afichua Kinachommaliza Kindoki

 

Beno Kakolanya.

KIPA tegemeo wa Yanga, Beno Kakolanya amewataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kumuunga mkono nyanda mkongomani, Klaus Kindoki na siyo kumponda kwa maneno mabaya.

Kakolanya ambaye kwa sasa anafanya vizuri na Yanga tangu kuanza kwa msimu huu ameliambia Spoti Xtra kuwa Kindoki ni kipa mzuri lakini amepoteza hali ya kujiamini anapokuwa uwanjani kutokana na maneno ambayo amekuwa akikumbana nayo kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo tangu alipofanya vibaya dhidi ya Stand United.

 

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 4-3 lakini Kindoki hakuwa kwenye ubora wake jambo ambalo liliwaudhi mashabiki wa Yanga na kupoteza uaminifu dhidi yake.

 

Hali hiyo imekuwa ikimtesa vilivyo Kindoki kwani hivi karibuni katika mechi ya ligi kuu dhidi ya Mbao alipata nafasi nyingine baada ya Kakolanya kuumia lakini alionekana kuwa ni mwenye wasiwasi mkubwa alipokuwa na hali ya kutojiamini.

 

“Kindoki ni kipa mzuri na amekuwa akifanya vizuri sana mazoezini ila hivi karibuni amepoteza tu hali ya kujiamini baada ya kufungwa mabao matatu dhidi ya Stand,”alifichua Kakolanya ambaye aliwahi kuidakia Prisons.

 

“Niwaombe tu wapenzi na mashabiki wa Yanga, kumuunga mkono na wasimpatie maneno ya vitisho ili aweze kurudi katika hali ya kujiamini ili tuweze kushirikiana naye vizuri katika kuipambania timu yetu,” alisema Kakolanya.

 

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesisitiza kwamba Kindoki ni mchezaji mzuri na anamuamini kwa vile alimtoa DR Congo akiwa anafanya vizuri dhidi ya timu kubwa za huko.

STORI: SWEETBERT LUKONGE, SPOTI XTRA

Loading...

Toa comment