The House of Favourite Newspapers

Kassim Kayira: Aanza kazi ya uandishi wa habari

kassim kayiraKUPATA fursa ya kusikia historia za watu maarufu duniani, kujua walikopita hadi kufikia utukufu walionao, hakika siku zote imebaki kuwa somo kubwa kwa watu wenye uchu na nia ya kufikia vilele mbalimbali vya mafanikio maishani.

Kama kawaida, katika safu hii tunaye Kassim Kayira, anasimulia historia ya maisha yake. Ni miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji mashuhuri ulimwenguni, aliyefanya kazi katika vituo mbalimbali ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Wiki iliyopita, tuliishia kwenye kipengele cha jinsi nilivyolamizika kusitisha mahojiano na Kayira, baada ya yeye kupata safari ya dharura mjini Dodoma, kwa ajili ya kazi.

Je, nini kilifuata?

KANYAGA TWENDE…

Wiki moja baadaye…

Hakika nilikuwa nimeshaanza kuingiwa na wasiwasi kama nitamalizia mahojiano yangu na Kayira. Hata hivyo, siku moja  nikiwa ofisini, simu yangu ya mkononi iliita, lakini namba ilikuwa ngeni kabisa. Naamua kuipokea huku nikisikilizia sauti ya mpigaji.

“Eeh, halo, ni mimi Kayira aise, hii ni namba yangu mpya ya Tanzania, niko njiani kutokea Dodoma, tukutane kesho ofisini kwetu tumalizie mahojiano, sawa, sawa basi haya, naona hata mtandao si mzuri sana,” inasikika sauti hiyo na baadaye simu inakatwa.

Hatimaye siku ikawadia, majira ya saa tano asubuhi, naamua kwenda makao makuu ya Azam TV, Ilala. Nafika mapokezi nikiwa na shauku kubwa kabisa ya kukutana tena na Kayira. Dada wa mapokezi ananipokea nami harakaharaka namueleza lengo la uwepo wangu eneo hilo.

“Ok, sasa kaa hapo nikuitie, si anajua kuwa uko hapa?,” anauliza dada huyo kwa sauti nyembamba na yenye utulivu.

“Yeah, anajua kuwa niko hapa,” namjibu huku nikijitahidi kuonesha uchangamfu fulani hivi.

Hata hivyo, wakati nikimalizia maneno hayo kwa dada wa mapokezi, ghafla inasikika miguu ya mtu akija mahali tulipokuwa tumesimama, hapohapo najikuta nikilazimika kugeuka nyuma kutaka kuona ni nani aliyekuwa akitembea kwa haraka namna hiyo.

Bila kutarajia, macho yangu yanagongana na macho ya Kayira. Kama kawaida yake, miwani ya jua ikiwa kichwani, begi dogo mkononi na baadhi ya vitabu.

“Ooh, Brighton, karibu sana, dada huyu ni mgeni wangu, umefika zamani?,” anasema Kayira huku akinishika mkono na kunionesha mahali pa kukaa.

“Hapana, sina muda mrefu tangu nifike,” namjibu na kumkazia macho.

“Aisee, karibu sana ndugu yangu, karibu na samahani kwa usumbufu si unajua mambo ya kazi,” anasema Kayira huku akiachia tabasamu pana kama kawaida yake.

“Ooh, ningoje kwanza nije,” anasema na kisha kunyanyuka na kuelekea mahali ambako kwa haraka sikujua ni wapi, ila ndani ya ofisi hiyohiyo.

Dakika mbili baadaye, anakuja na kunichukua hadi ndani ya chumba maalum cha mazungumzo.

“Dah, utanivumilia, tutakuwa tunahama kwenda maeneo mbalimbali, kuna mambo natakiwa niyakamilishe, maana kesho natakiwa kusafiri kwenda Uganda,” anasema Kayira na kulivua begi lake.

“Tulikomea wapi vile?,” anauliza lakini akiwa makini sana kwa kunitazama usoni.

“Tuliishia uliposoma ualimu lakini hukufanya kazi ya ufundishaji,” namkumbusha na hapohapo nasimama ili kumpa kifaa cha kurekodia sauti, mahojiano yanaendelea.

“Basi bwana, mwaka 1997 nilienda nchini Rwanda na kuanza kazi ya kutafuta habari (reporter) katika television ya taifa ya TVR,” anasema Kayira.

“Ilikuwaje kupata kazi huko, ilikuwa rahisi kiasi hicho?,” namuuliza kwa haraka.

“Unajua, kwa wakati huo Rwanda ilikuwa imetoka kwenye yale mauaji ya Kimbari (Genocide), hivyo hapakuwa na watangazaji wa kutosha, kwa kuwa nilikuwa na cheti kizuri, walinipa na kuanza kazi mara moja,” anasema Kayira huku akichomeka simu yake chaji kupitia kifaa cha kuhifadhia umeme (power bank).

“Kazi ikaendelea, nikafanya kwa kujituma mno, kiasi kwamba nilikaa miezi kama mitatu tu nikaanza kupanda vyeo kwa harakaharaka,” anasema Kayira.

“Nini ilikuwa siri ya kupanda vyeo?,” namuuliza.

“Unajua katika maisha ya kazi, hakuna kitu chenye thamani kama kufanya kazi kwa nguvu, nidhamu kwa watu na kazi yako, ndiyo misingi mikubwa sana kwa kazi,” anasema Kayira na kuendelea.

“Tena hapa nataka niweke wazi kitu kimoja, sisi Waafrika ni tofauti sana na wenzetu Wazungu, wao kazi ndiyo kila kitu lakini huku kwetu mtu anakuwa na kiu ya kazi kama hana, lakini akipata  kazi, mambo yanabadilika kabisa.

“Hakuna tena kuheshimu kazi, dharau za wazi kabisa kwa wakubwa na mambo mengi ya kufanana na hayo, ni jambo baya sana, mimi sikuwa hivyo, nilipanda hadi kufikia cheo cha mhariri mkuu wa habari (Chief News Editor),” anasema Kayira na kukohoa kidogo.

Wakati mazungumzo yanaendelea, ghafla namuona akiinuka na kunikazia macho, hapohapo ananiambia jambo ambalo linanifanya niishiwe raha ghafla.

 

Je, nini kitafuata? Usikose wiki ijayo.

Comments are closed.