The House of Favourite Newspapers

Kauli ya Matola na Kapombe kwa Simba

0

KOCHA msaidizi wa Klabu ya Simba, Seleman Matola amewaomba radhi mashabiki na wanachama wa wekundu hao kwa kupoteza mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga akiamini kuwa ni matokeo katika mpira wa miguu lakini sio mwisho wa mpango wao wa kufanya vizuri msimu huu.

 

Matola ameyasema hayo wakati akiweka bayana juu ya matayarisho kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2021/2022 dhidi ya Biashara Mara United utakaocheza leo saa 10 Jioni katika dimba la Karume huko Mkoani Mara.

 

”Kwanza niwaombe radhi mashabiki kwa matokeo yaliyopita kwakuwa yaliwaumiza wengi, hata sisi tumeumia lakini tunawaomba waje watuunge mkono katika mechi yetu dhidi ya Biashara naamini tutapata ushindi kutokana na maandalizi yetu”Kocha msaidizi Seleman Matola.

 

Kwa upande wa Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe naye akasisitiza kuwa licha ya kupoteza dhidi ya Yanga bado wanaendelea kuwekea mkazo malengo yao makuu msimu huu ambayo ni pamoja na kutetea ubingwa wa TPL.

 

”Tumepoteza mchezo muhimu wa kufungua Ligi dhidi ya Yanga, ingawa tuna amini mchezo wa Biashara ni sehemu ya kurejesha hamasa kwa mashabiki wa Simba”Shomari Kapombe nahodha msaidizi wa Simba.

 

Kwa upande wa Biashara Mara United ambao ni wawakilishi wa Tanzania bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wamesema wamejiandaa kikamilifu kuondoka na ushindi dhidi ya Simba.

 

“Wala siyo simba tu, hapa uwanja wa karume patakuwa pagumu kwa wageni msimu huu, tunaanza na hao Simba” – Meneja wa Klabu ya Biashara United Mara, Frank Wabare.

 

Tangu mwaka 2019 timu hizi zimekutana mara 6 katika Ligi Kuu Tanzania bara, ambapo Simba imeshinda mara 5 na sare mara moja , takwimu ambazo zinawapa nafasi kubwa mabingwa watetezi kuibuka na ushindi jioni ya leo.

 

Katika michezo hiyo Simba imefunga mabao 13, imeruhusu mabao 2, huku katika mechi hizo 6, Simba haijaruhusu kuguzwa kwa nyavu zake katika michezo minne kati ya hiyo.

Leave A Reply