The House of Favourite Newspapers

Kenya: Mtanzania Ahukumiwa Maisha Jela Shambulio Garissa

MAHAKAMA ya Kenya imemhukumu Mtanzania Rashid Mberesero kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia ya kutekeleza shambulio la kigaidi mwaka 2015 katika Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya.

 

Amehukumiwa kutumikia adhabu hiyo, akiungana na watu wengine wawili ambao kwa pamoja wamekutwa na hatia ya kuhusika na shambulio la kigaidi lililosababisha vifo vya wanafunzi 148 katika chuo hicho.

 

Wakati akihukumiwa adhabu hiyo, washtakiwa wenzake wawili, Hassan Edin na Mohammed Abdi  kwa jina jingine Mohamned Ali Abikar,  wamehukumiwa miaka 41 kila mmoja gerezani.

Mtanzania huyo  aligundulika katika eneo la tukio akiwa si mwanafunzi wala mfanyakazi wa chuo hicho.

 

Ilielezwa kuwa,  alikuwa akisoma shule ya Sekondari ya Bihawana mjini Dodoma, Tanzania, ambapo alidaiwa kutoroka shule baada ya kukatazwa kuvaa kofia.

 

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati huo, mwanafunzi huyo alijiunga na shule hiyo mwaka 2015 baada ya kutoka shule ya Sekondari ya Bahi-Kagwe.    Licha ya kutoweka shuleni, hakuna aliyefuatilia alikokwenda.

 

Kwa takriban miezi minne wazazi wa kijana huyo walidhani mtoto wao yupo shule lakini haikuwa hivyo. Haijulikani ni nini hasa kilichomfanya kuingia katika ugaidi. Wazazi wa Rashid walishangaa kugundua kwamba mtoto wao alikuwa miongoni mwa watu waliopanga na kutekeleza shambulio la Garissa.

 

Comments are closed.