The House of Favourite Newspapers

Wameacha Majina Yao ya Asili

0

LIMEKUWA ni jambo la kawaida kwa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, lakini pia wa filamu na tasnia mbalimbali kubadili majina yao ya asili kwa lengo la kuimarisha chapa zao ili kuvutia mashabiki ambao ndiyo wanunuzi wa kazi zao.

 

Lakini wapo wanaotumia majina ya wanyama kama alama kwamba wao ni wakali kama viumbe hao wanaoishi porini. Makala haya yataangazia wasanii 10 wa muziki huo ambao wamebadili majina yao ya asili na sasa yanatumika yale ya kisanii, hao ni hawa wafuatao;

 

LIL SAMA -MR BLUE

Huyu siku hizi anajiita Nyani Mzee akimanisha kuwa amekwepa mishale mingi kimuziki hadi kufikia alipo. Mwanzoni alikuwa anajiita Lil Sama. Baada ya kuachia Ngoma ya Blue na kufanya vizuri ndipo watu wakaanza kumuita Mr Blue.

 

Baadhi ya wasanii wanaojiita majina ya wanyama wakali ni Diamond Platinumz anayejiita Simba, Harmonize (Tembo), Ryvanny (Chui), Dudu Baya (Mamba); jina ambalo msanii Nurdin Bilal au Shetta alilitumia akajikuta anakemewa na Dudu Baya aliyedai kuwa msanii huyo hakidhi vigezo vya kutumia jina hilo.

 

Afande Sele naye alijiita Simba. Hata hivyo, kutokana na majina ya wanyama wakali kuwa machache, wasanii wengine wakajikuta wakinyang’anyana majina kama Simba ambalo alianza Afande Sele, lakini Diamond naye akajipachika.

 

Kama lilivyo jina la Tembo alianza nalo Ali Kiba, lakini sasa analitumia Harmonize. Utamaduni huo unazidi kushamiri kwa wasanii wa Bongo Fleva na sasa wapo wasanii waliotumia majina ya vyeo kama vile Lady Jaydee aliyejiita Komando na Inspector Haroun au Professor Jay ambaye awali alijiita Nigga Jay.

 

Rapa huyu aliyetoka na Kundi la Hard Blasters Crew (HBC) waliofunika zaidi miaka ya 2000 na jina lake la asili ni Joseph Haule albam yao iitwayo Funga Kazi, mwanzoni alikuwa anajiita Nigga Jay, lakini baadaye akaja na Professa Jay.

 

Hata jina la Professa Jay siyo yeye aliyeliunda, bali alipewa na analitumia hadi sasa ingawa limekuwa likipambwa na a.k.a kama Wamitulinga, Mbunge Nje ya Bunge na mengineyo.

Wasanii wengine kwa ufupi ni hawa wafuatao;

 

DOGO BARAKA -BARAKA DA PRINCE

Huyu ni miongoni mwa wasanii waliofanya sana marekebisho kwenye majina yao, alianza kujiita Dogo Baraka. Wakati anatoka kimuziki alijulikana kama Baraka Da Prince na sasa kaliboresha kidogo na kuwa Barakah The Prince.

 

LIL K -YOUNG KILLER

Kabla ya kuanza kutumia jina la Young Killer mwanzoni alikuwa akijita Lil K, hii ni kufuatia umaarufu wa Rapa wa Marekani, Lil Wayne aliokuwa nao wakati ndoto ya Young Killer kimuziki ikiwa imeiva.

Wakati Young Killer akitumia jina Lil K alitoa wimbo uitwao Winner ambao alimshirikisha Barakah The Prince ambaye kipindi hicho alitambulika kama Dogo Baraka.

 

RAPCHA -JOH MAKINI

Rapa huyo kutoka Kundi la Weusi la Arusha kabla ya kusikika akiwa chini ya River Camp Soldiers alikuwa anatumia jina la Rapcha.

Jina la Joh Makini ni chimbuko la jina lake la kuzaliwa, John Simon. Hata hivyo, jina alilolitupa (Rapcha) limekuja kutumiwa tena na msanii mwingine.

 

SARAH -SHAA

Jina la kuzaliwa ni Sarah Kaisi, alipoanza muziki alikuwa akijiita Sarah pekee, jina la Shaa lilitokana na jina la Kundi la Wakilisha ambalo liliundwa na wasanii watatu ambao ni Witness, marehemu Langa Kileo na Shaa mwenyewe, hivyo aliongeza herufi A mwishoni.

 

Hata hivyo, siyo Shaa aliyeunda jina hilo bali ni rapa Albert Mangwea aliyefariki mwaka 2013. Shaa siyo msanii wa kwanza kupewa jina, kuna wasanii wengine kama Young Dee aliyepewa jina hilo na Dully Sykes.

 

JOH MAKINI -NIKKI WA PILI

Kutokana na kaka yake Joh Makini kuwa tayari ameshatoka kimuziki, Nikki alishawishika kutembelea gia hiyo kama alivyofanya Abdu Kiba baada ya kaka yake, Ali Kiba kutoka kimuziki.

Hata alipokuja kujiita Nikki wa Pili kitu hicho kilikosolEwa na Nikki Mbishi kupitia Mgoma ya Puch Line aliyomshirikisha Grace Matata. Mbishi alisema; “Kivipi Nikki wa Pili na wa kwanza hajulikani, wakili unakosa dili kwa stanza hatulingani…”

 

2 PROUD -SUGU

Ni Joseph Mbilinyi. Rafiki yake mzungu ambaye alikuwa akimkubali kimuziki ndiye aliyempa jina hilo, ni kufuatia kauli zake za kila mara ‘Iam too proud of you’ (najivunia wewe), katika kufupisha, yule mzungu ndiyo akaja na jina hilo, 2 Proud kisha likafuata Mr Two.

 

Miaka ya 2000 baada ya kutoa albam kadhaa na misimamo yake katika muziki katika kudai maslahi yake na kwa wasanii wote kwa jumla ambayo yalikuwa akiporwa na wauzaji wa albam (kanda) ndipo likaibuka jina la Sugu.

 

NEY -NAY WA MITEGO

Rapa huyo ambaye ni C.E.O wa Lebo ya Free Nation kabla ya mwaka 2005 alikuwa hatumii jina hilo, bali alikuwa anaitwa Ney; jina alilopewa na mpenzi wake ambaye ndiye aliyemlipia pesa ya kurekodi wimbo wake wa kwanza ndani ya Bongo Records.

 

Mwaka 2005 alitoa wimbo uitwao Wamitego ambao ulifanya vizuri kwa kiasi chake, ndipo mashabiki wengi wakampa jina la Nay wa Mitego ambalo Nikki Mbishi aliwahi kuliponda kupitia wimbo wake (diss track) uitwao Ney wa Mitego.

 

Wasanii wengine walioacha majina yao ya asili na kuibuka na ya kisanii (kwenye mabano ni hawa wafuatao; Nikki Ray (Nikki Mbishi), Maromboso (Mbosso), Darasa (Darassa), Q Chief (Q Chillah) na wengineo.

Hata hivyo, wasanii wengi waliozungumza na safu hii wamesema majina hayo ni mbwembwe tu kwani brandi ya msanii inakuzwa na wimbo wake anaotunga na kukubalika kwa jamii.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Leave A Reply