The House of Favourite Newspapers

Kichanga Chakutwa Kikielea Juu ya Maji

0

KAGERA: Kichanga cha kiume ambacho kilikuwa hakijafikisha umri wa kuzaliwa, kimekutwa kikielea kwenye maji katika Mto Kanoni uliopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Kichanga hicho ambacho mama yake hakufahamika, kilikutwa kikielea kikiwa tayari kimepoteza maisha.

 

Kamanda wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto mkoani Kagera, Shabani Dawa aliliambia Gazeti la IJUMAA kuwa, walipigiwa simu na msamaria mwema akawaambia kuna kiumbe kinaonekana kikielea Mto Kanoni.

“Tulipofika tulikuta kichanga cha kiume kinachokadiriwa kuwa na umri wa miezi saba au nane.

 

“Tulikiopoa na kufuata taratibu zote kwa kushirikiana na Polisi na kwenda kufanya utaratibu wa mazishi.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Buyekera, Justian Kamugisha, aliungana na askari wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto na Jeshi la Polisi ambapo alisema ni vigumu kutambua mwanamke aliyefanya ukatili huo.

 

Kwa upande wake, Anjero John, mkazi wa Buyekera alisema alisikitishwa na kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo ambaye hakujulikana, kwa kujifungua mtoto na kumtupa mtoni.

Alisema wapo wanawake wengi wanatafuta watoto kwa muda mrefu hadi wanalazimika kulipa fedha nyingi kwa waganga au hospitalini ili wasaidiwe kupata watoto.

 

Kufuatia matukio ya ukatili kuongezeka mkoani Kagera, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kagera, Rebecca Ngwambasa alisema vitendo vya ukatili vimeendelea kushika kasi mkoani humo, ambapo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana, mkoa huo ulifikisha matukio 1,160 ya ukatili.

Stori: NYEMO MALECELA, Ijumaa

Leave A Reply