The House of Favourite Newspapers

Kigwangalla Ataka Karantini kwa Wageni Iondolewe

0

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla amesema kwa kuwa #CoronaVirus tayari imeshaingia Tanzania, haileti maana kuweka masharti magumu kwa wageni kuingia nchini.

 

Kigwangalla amesema kutokana na virusi vya corona vinavyoendelea kuisumbua dunia, mapato katika sekta hiyo yameshuka kutoka Sh trilioni 2.6 zilizotarajiwa kukusanywa. Pia taasisi zilizokadiriwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 132.1 zinatarajiwa kukusanya Sh bilioni 33.5 ikiwa ni anguko la asilimia 75.

Kigwangalla alikuwa  akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21.

 

“Tunadhani mkakati wa lazima wa kukaa karantini kwa siku 14 kwa gharama zako uondolewe, na badala yake uimarishwe uratibu wa lazima kuvaa barakoa kwa kila mtu huku usafi pamoja na umbali baina ya watu ukizingatiwa,” alisema.

 

Aliongeza kwamba wizara imeanza kujipanga kuishawishi serikali kukubali namna ya kufungua biashara za utalii mwezi  Juni mwaka huu. Amedai kwa mujibu wa utafiti na tathmini waliyofanya, ajira 477,000 zipo hatarini kupotea.

 

Vilevile, serikali imesema kama hali haitatulia hadi Oktoba, ajira za moja kwa moja katika sekta ya utalii zitashuka kutoka 623,000 hadi kufikia 146,000 na watalii watashuka kutoka 1,867,000 waliotarajiwa hadi 437,000.

 

Alisema wizara ilifanya tathmini ya awali (rapid assessment) iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi Aprili 6, mwaka huu.

 

Alisisitiza kwamba tathmini hiyo ilibaini kuwa madhara makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana mwanzoni mwa Machi, tofauti na Februari na Januari, mwaka huu ambapo hali ilikuwa shwari.

 

Alisema tathmini ilibaini mashirika 13 ya ndege yalisitisha safari za kuja nchini tangu Machi 25, mwaka huu, hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kupata watalii kutoka nje ya nchi.

 

Pia aliyataja mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja ni Emirates, Swiss, Oman Air, Turkish, Egyptian Air, South African Airways, Rwandair, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na KLM.

 

Alisema NCAA ilikadiria kukusanya Sh bilioni 162.7, kwa sasa itakusanya Sh bilioni 58, TFS ilikadiria Sh bilioni 153.6, sasa ni Sh bilioni 121 na Tawa ilikadiria Sh bilioni 58.1 sasa ni Sh bilioni 22.

Leave A Reply