The House of Favourite Newspapers

KILI MARATHON 2020 YAZINDULIWA MOSHI

0

Mashindano ya mbio za nyika za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2020, ambayo ni toleo la 18 la mbio hizo, yamezinduliwa rasmi katika hoteli ya Kibo Palace iliyoko Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, takribani mwezi mmoja na nusu kabla ya kufanyika kwake mjini Moshi mwanzoni mwa mwezi Machi, mwaka huu.

Akizindua mashindano, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ameapongeza wadhamini, wafadhili na waandaaji wa mashindano hayo maarufu wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager-42 km, Tigo-21km, Grand Malt-5km Fun Run kwa kufadhili mbio hizo ambazo amesema zinazidi kuupa Mkoa wa Kilimanjaro umaarufu ndani na nje ya nchi.

Aidha aliwapongeza wadhamini wakuu wa mbio hizo Kilimanjaro Premium Lager kwa kudhamini mbio hizo kwa mwaka wa 18 sasa ambao amesema pamoja na kuwa wafadhili wakuu, pia wametoa motisha kwa washiriki wa kitanzania ambao watashinda mashindano hiyo. Alisema motisha hizo ni pamoja na shilingi milioni 1.5 kwa kila Mtanzania wa kike na wa kiume atakaeshika nafasi ya kwanza.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa ushauri kwa uongozi wa wizara ya maliasili na utalii kushirikiana na waandaji wa mbio hizo pamoja na wadau wengine ili kukuza mashindano hayo ambayo yanaongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania kila mwaka.

“Kuna ushahidi unaodhibitishwa na idadi ya washiriki kutoka nje ya nchi ya kuwa mashindano haya yanaongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania kupitia ushiriki wao katika mbio hizi, hivyo ushiriki wa wizara ya utalii utaongeza uhamasishaji wake”, alisema. Aidha alitoa rai kwa wafanyabiashara kutumia vizuri fursa inayotokana na uandaaji wa mbio hizo mkoani Kilimanjaro kutokana na ukweli kuwa zitawavutia watu wengi hivyo kuwepo na biashara nyingi.

“Wamiliki wa mahoteli wanaweza kuanza kufikiria kuja na vifurushi tofauti vitakavyoweza kuwavutia washiriki na wale watakaokuja mkoani hapa kwa ajili mbio hizi maarufu; mbio hizi pia zitawavutia watalii wengi ambao watapenda kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, hivyo wafanyabiashara hawana budi kutangaza bidhaa zinazohusiana na bidhaa walizo nazo huku wakizingatia ubora wa bidhaa zao na huduma watakazotoa”, alisema.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, ambao ndiyo wadhamini mbio za kilomita 42 ameelezea matarajio yake ya kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa na mafanikio makubwa kutokana na msisimko mkubwa ambao umeanza kuonekana miongoni mwa watu wengi.

“Nitoe ushauri wangu kwa Watanzania watakaoshiriki kwenye mbio za kilometa 42 kuhakikisha wanafanya mazoezi ya hali ya juu ili zawadi ziweze kubaki nyumbani”, alitoa ushauri wake.

Pamela aliendelea kusema kuwa zawadi zitakuwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 23, ambapo mshindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watapata shilingi milioni 4 kila mmoja na kwamba kutakuwa na zawadi za motisha zenye thamani ya shilingi miilioni 3 kwa ajili ya kuwahamasisha washiriki wa Kitanzania ili wafanye vizuri.

“Mshiriki wa Kitanzania wa kike na wa kiume atakayemaliza wa kwanza katika mbio za kilometa 42 atapata zawadi ya ziada ya shilingi milioni 1.5 kila mmoja.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini na ambao ndiyo wadhamini wa mbio za kilometa 21 maarufu kama Tigo Half Marathon, Aidan Komba amesema taasisi hiyo inajivunia kuwa sehemu ya wadhamini wa mbio hizo maarufu Barani Afrika ambapo alisema ufadhili wao wa mwaka huu wa 2020 utakuwa ni watano mfululizo.

“Tigo tunajivunia kuwa sehemu ya mashindano haya maarufu kwa mara nyingine tena, ambayo huwashirikisha wanariadha maarufu, kutoka maeneo na kada mbalimbali za kimaisha wenye weledi wa hali ya juu katika riadha na ambao wanatoka mataifa mbalimbali duniani”, alisema.

“Nitoe rai kwa washiriki wa kilometa 21 kusajili kupitia huduma ya Tigo Pesa kwa kupiga * 149 * 20 # ili kushiriki mbio za kilometa 21 maarufu kama Tigo Half Marathon”, alisema Komba na kuongeza kuwa Tigo inashirikiana na wadhamini wengine katika kufanikisha mbio hizo maarufu ambazo ni maarufu na muhimu katika kukuza utalii wa Tanzania na wakati huo huo ikileta muungano wa kifamilia miongoni mwa wananchi wa mataifa tofauti tofauti duniani.

Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, David Tarimo, amesema kuwa wanatarajia mbio za kilometa 5 zinazodhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt, zitavutia watu wengi zaidi mwaka huu, ambapo alitoa rai kwa wale wenye nia ya kushiriki mbio hizo kujisajili mapema, ambapo alisema zitahamasishwa na uzinduzi wa Grand Malt zenye ujazo mpya wa 330 ml, ambayo alisema zinaptikana nchi nzima kwa bei ya shilingi 2,000. “Grand Malt ni kinywaji ambacho ni chaguo bora kwa wakimbiaji wakiwemo na watoto pia,” alisema.

Wadhamini wengine wa mbio hizo ni pamoja na Kilimanjaro water, Benki ya Barclays, Simba cement, TPC sugar, Precision Air, Unilever, Kibo Palace Hotels, kampuni ya ulinzi ya GardaWorld, Keys Hotels na CMC Automobiles.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mbio za Kilimanjaro Marathon, John Bayo, amesema usajili unaendelea kupitia mtandao wa www.kilimanjaromarathon.com na pia kupitia huduma za kifedha za Tigo Pesa kwa kupiga * 149 * 20 # na kwamba zoezi hili linatarajiwa kumalizika katiak muda wa mwezi mmoja ujao mnamo au kabla ya Februari 16, 2020.

“Awali kulikuwa na punguzo wa asilimia 20 wakati wa usajili, ambalo lilifanyika kati ya Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020”, alisema na kuongeza pfa hiyo imekwisha na kwamba wale wanaoendelea kujisajili kwa sasa watawajibika kulipia viwango kamili vilivyowekwa.

Kwa upande wao uongozi wa mamlaka ya mapato nchi (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro wameelezea nia yao ya kushirikiana na wandaajiwa mbio hizo kutokana na ukweli unachangia mapato kupitia washiriki wa mbio hizo kila mwaka.

“Nia yetu ni kuhakikisha tunashirikiana na wandaajiw wa mbio hizi ili kuhakikisha zinafanyika vyema na katika kuhakikisha hili, baadhi ya wafanyakazi wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro wameshajiandikisha kuwa washiriki wa mbio za mwaka huu”, alisema Kahleed Mchumwa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wamiliki wa mahoteli Mkoa wa Kilimanjaro Jacob Tarimo, amewapongeza wandaaji wa mbio hizo ambazo alisema uwepo kwake umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha biashara za mahoteli pamoja uchumi wa Mkoa kwa ujumla.

“Nitoe rai kwa uongozi wa Mkoa kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha kunakuwepo na matukio mengine ya ziada ambayo yatalenga kuboresha uchumi wa Mkoa”, alisema.

 

Leave A Reply