The House of Favourite Newspapers

Kipigo cha Uchebe, Shilole Afukua Makaburi

0

KELELE nyingi zinasikika kila kona nchini Tanzania juu ya kipigo ‘hevi’ cha staa wa muziki na sinema za Kibongo, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ alichopewa na mumewe, Ashraf Uchebe.

Kipigo hicho kilichosababisha ndoa ya wawili hao kuvunjika, kinatajwa kufukua matukio mengine kama hayo waliyofanyiwa mastaa mbalimbali wa kike Bongo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, listi ya mastaa waliofanyiwa ‘unyambilisi’ kama huo na wapenzi au waume wao ni ndefu na ndiyo wanaongoza mashambulizi ya maneno dhidi ya Uchebe.

Tangu Shilole aanike picha za vipigo kutoka kwa Uchebe Jumatano iliyopita, mastaa hao wamekuwa wakiposti maneno makali na kushinikiza Serikali kuchukua hatua dhidi ya Uchebe na kama sheria haitafuata mkondo wake, basi wako tayari kuandaa maandamano yasiyokuwa na kikomo hadi pale Serikali itakaposikia kilio chao.

Baadhi yao wanadai kwamba, tukio la Shilole ni kielelezo cha wanawake wengi wanaopigwa, kunyanyaswa na kudhalilishwa kimwili na kingono na waume zao kwenye jamii na hawaoni msaada wowote.

“Wengi wanaogopa kusema, lakini sisi ni mfano tu, kuna wanawake wengi mno wananyanyaswa, lakini wanavumilia tu,” anasema Shamsa Ford, mmoja wa waathirika wa vipigo kutoka kwa aliyekuwa mumewe, Rashid almaarufu Chid Mapenzi.

Baadhi ya mastaa waliowahi kuripotiwa kwa vipigo kutoka kwa wanaume wao kwenye Magazeti Pendwa ya Global Publishers, ni hawa wafuatao;

WEMA SEPETU

Staa wa Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu aliwahi kuripotiwa kupokea kipigo kitakatifu kutoka kwa zilipendwa wake ambaye ni kinara wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ enzi za mapenzi yao shatashata kabla ya kutengana.

Wema alidai kwamba, Diamond au Mondi alitekeleza uhalifu huo akimtuhumu kunasa meseji ya kimapenzi kwenye simu yake kutoka kwa mwanaume mwingine.

Kipigo hicho kikali kilimuacha Wema na jeraha usoni, lakini hakuripoti Polisi.

LADY JAYDEE

Wakati akitengana na mumewe wa ndoa ambaye ni mtangazaji maarufu Bongo, Gardner G Habash, mwanamuziki mkongwe; Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ alieleza ni jinsi gani jamaa huyo alivyokuwa akimpa vitasa.

Hata hivyo, kama walivyo wanawake wengi, hakuwahi kuripoti matukio hayo Polisi hadi alipoamua kudai talaka mahakamani kisha akaendelea na maisha yake mengine, japokuwa kuna za chinichini kuwa wamerudiana na sasa ni kitu na boksi.

Juu ya tukio la kipigo cha Shilole, Lady Jaydee anasema; “Huyu Uchebe naye ashikwe apigwe vizuri tu anyooke…”

SHAMSA

Staa mwingine wa sinema za Kibongo ni Shamsa Ford. Naye amekutana na kipigo kutoka kwa mumewe, Chid Mapenzi kabla ya kuamua kutengana naye.

Wakati akitangaza kuachana na Chid Mapenzi, Shamsa alitamka wazi kuwa, jamaa huyo alikuwa akimtesa mno ikiwemo kumpa vipigo.

Juu ya kipigo cha Shilole, Shamsa anasema; “Mtu umvishe, umpendezeshe, umpe heshima halafu unaambulia kipondo? Hapana!”

LULU

Mwigizaji mwingine aliyepitia kashikashi za vipigo ni Elizabeth Michael ‘Lulu’. Yeye aliwahi kukiri kupokea kipondo kutoka kwa aliyekuwa mwandani wake ambaye ametangulia mbele ya haki, marehemu Steven Kanumba.

RUBY

Wakati anaachana na baba mtoto wake aitwaye Kusah, mwanamuziki mkali wa Bongo Fleva, Hellen George ‘Ruby’ alieleza ni kwa jinsi gani jamaa huyo alikuwa akimpa vipigo nusura amtoe uhai.

Lakini kama walivyo mastaa wengine, naye hakwenda kuripoti Polisi.

DAVINA

Kabla ya ndoa yake ya zamani kuvunjika, staa wa filamu za Bongo, Halima Yahya ‘Davina’ aliripotiwa kubondwa mno na mumewe, kisa ujumbe wa mapenzi ulionaswa kwenye simu yake kutoka kwa mwanaume mwingine.

Kuhusu tukio la Shilole, Davina anasema; “Wanawake tukiendelea kukaa kimya na kuvumilia unyama huu, tutakufa na kuwaacha watoto wetu ambao baadaye tunakuja kuzalisha watoto wa mitaani, mimba za utotoni nk.

“Hivi mfano kwa kipigo hiki, bahati mbaya mtu akadondoka na kupoteza maisha, watoto wake anaowahangaikia hivi sasa kuwatafutia maisha wasome, waishi vizuri, nani atawaangalia tena? Nani atawasomesha? “Hili halipo kwa Shishi tu, lakini limeonekana kwa sababu ameamua kuvunja ukimya na kuweka wazi. Je, ni wanawake wangapi wanapitia haya na wako kimya?

“Kuna kesi za wanawake wengi kuuawa kwa kipigo.

“Hili ni darasa, tusikubali na kuficha unyanyasaji kama huu na kiukweli tupo wengi na ni vile wengine tunaamua kunyamaza ila wanawake bado tunanyanyasika…”

GIGY MONEY

Msanii wa filamu na Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’, mara kadhaa aliripotiwa kula vitasa kutoka kwa mzazi mwenzake ambaye ni mtangazaji aitwaye MO J. Kutokana na hali hiyo, wawili hao walishindwana, lakini pia Gigy anaripotiwa kubondwa na mwanaume wake wa sasa ambaye ni Mnigeria.

AUNTY LULU

Mwigizaji na mtangazaji wa kitambo Bongo, Lulu Mathias ‘Aunty Lulu’ aliwahi kuripotiwa kuchezea kipigo kutoka kwa mpenzi wake kiasi cha mimba yake kuchoropoka.

Hata hivyo, suala hilo lilimalizwa kifamilia kabla ya kuachana na mwanaume huyo.

NENO LA UMMY MWALIMU

Kuhusu tukio la shambulio la Shilole, waziri mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliandika ujumbe huu;

“Pole sana Shilole! Hongera kwa ujasiri wa kutokaa kimya dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

“Tuvunje ukimya, ukatili dhidi ya wanawake haukubaliki.”

Leave A Reply