The House of Favourite Newspapers

Kubaki Ligi Kuu Bara Hesabu Kali

1
Kikosi cha Tanzania Prisons

Omary Mdose

TAYARI timu ya JKT Ruvu yenye maskani yake Mlalakuwa jijini Dar es Salaam, imeaga Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupoteza mchezo wake wa wikiendi iliyopita dhidi ya Toto Africans ya Mwanza kwa mabao 2-1.

Baada ya timu hiyo ya jeshi kushuka daraja, kitendawili kimebaki timu gani mbili zitaungana nao kutimiza idadi ya timu tatu zinazotakiwa kushuka msimu huu na kutoa nafasi kwa Singida United, Njombe Mji na Lipuli FC ambazo tayari zina tiketi ya kushiriki ligi kuu msimu ujao.
Katika hesabu zilizopigwa na Championi, zinazihukumu timu za Ndanda na Majimaji kitu ambacho kinadhihirisha timu hizo zitaunga na JKT Ruvu kushuka daraja.

Majimaji
Ikiwa imebakiwa na michezo miwili dhidi ya JKT Ruvu na Mbeya City, Majimaji inahukumiwa na hesabu za Championi ambazo zinaonyesha kwamba, katika pointi sita inazozihitaji, ni ngumu kuzipata zote, wakijituma sana wataambulia nne kwa maana kwamba, wanaweza kushinda dhidi ya JKT Ruvu, halafu wakaambulia sare mbele ya Mbeya City. Wakiongeza pointi hizo nne, zitawafanya kumaliza ligi wakiwa nazo 33.
Katika mechi zao za mzunguko wa kwanza, Majimaji ikiwa nyumbani iliifunga JKT Ruvu bao 1-0, na ilipoenda ugenini kupambana na Mbeya City, iliambulia kichapo cha mabao 3-2.

Ndanda
Hii inashika nafasi ya nne kutoka mkiani ikiwa na pointi 30 huku ikibakiwa na michezo miwili. Katika mechi hizo mbili, itaenda ugenini kupambana na Prisons ambayo kwenye mchezo wa kwanza, Ndanda ilishinda 1-0. Kisha itarudi nyumbani kumalizana na JKT Ruvu. Katika mchezo wa kwanza, JKT Ruvu ilishinda 1-0.
Ukiangalia mchezo ujao kwao ndiyo mgumu sana kutokana na timu inayokutana nayo. Prisons nao wanahitaji alama tatu tu katika michezo yao miwili iliyosalia. Hivyo ni lazima wausake ushindi wakiwa nyumbani kwao watakapopambana na Ndanda hali inayosababisha mchezo huo kuwa mgumu zaidi kwa Ndanda. Prisons ikishinda, Ndanda itabaki na pointi zake 30, ikishinda mchezo wa mwisho itamaliza ligi ikiwa na pointi 33 sawa na Majimaji kwa mujibu wa hesabu za Championi.

Toto Africans
Kwa hesabu za harakaharaka, Toto ina asilimia kubwa ya kubaki ligi kuu kwa msimu ujao kuliko Ndanda na Majimaji. Toto inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani, lakini ina faida ya kuwa na michezo mitatu tofauti na wenzake wenye miwili.
Japo inaonekana kuwa michezo hiyo dhidi ya Azam, Yanga na Mtibwa ni migumu, lakini inaweza kukusanya pointi kuanzia nne katika michezo hiyo ambazo zitawafanya kufikisha 33 ikiwa sawa na Ndanda na Majimaji. Toto ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo itakuwa juu yao.
Kwa sasa ina pointi 29, takwimu zinaonyesha kwamba, katika mechi za mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam, ilifungwa 1-0, ikafungwa tena 2-0 na Yanga, kisha ikaifunga Mtibwa 3-2. Mechi hizo zote zilipigwa nyumbani kwake.
Azam na Mtibwa hazina cha kupoteza, tofauti na Yanga inayousaka ubingwa.

Mbao FC
Licha ya kwamba nayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini ratiba yao ina wabeba. Mbao ina pointi 30, imebakiwa na michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar ugenini na Yanga itakayochezwa nyumbani kwao. Katika michezo ya mzunguko wa kwanza dhidi ya timu hizo, yote ilipoteza ambapo ilifungwa 2-0 na Kagera, ikafungwa na Yanga 3-0.
Lakini hivi karibuni ilikwenda ugenini kucheza na Kagera Sugar na kuifunga mabao 2-1, kisha ikaichapa Yanga 1-0 ikiwa nyumbani kwake, mechi hizo zote zilikuwa za Kombe la FA.
Kagera Sugar hawana cha kupoteza, wanaweza kudondosha pointi mbele ya Mbao na kuwafanya kufikisha 33, lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa kupata angalau pointi moja mbele ya Yanga na kuwafanya kuwa nazo 34 zitakazowaweka sehemu salama.

 

Prisons
Fainali yake ipo kwenye mchezo ujao dhidi ya Ndanda watakapokuwa nyumbani kwao katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Prisons ikiwa na pointi 31, inahitaji pointi tatu tu kubaki ligi kuu na pointi hizo wana asilimia kubwa kuzipata mbele ya Ndanda.
Katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza, Ndanda ilishinda 1-0, kutokana na matokeo yao mazuri wakiwa nyumbani, inawafanya kuwa na uhakika wa kupata pointi zote tatu tena. Kitu kizuri ni kwamba, Prisons mechi zake mbili zilizobaki zote itachezea nyumbani kwao, itamaliza ligi kwa kupambana na African Lyon ambayo kwenye mzunguko wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1.
Prisons ikishazipata pointi tatu za Ndanda, haitakuwa na presha tena jambo ambalo litaifanya African Lyon nayo ipumue.

Kikosi cha Yanga SC.

African Lyon
Pointi 31 mkononi huku ikibakiwa na michezo miwili dhidi ya Ruvu Shooting na Prisons, African Lyon ina asilimia kubwa ya kuendelea kucheza ligi kuu kwa msimu ujao.
Ipo hivi; mchezo wao ujao dhidi ya Ruvu Shooting watachezea nyumbani katika Uwanja wa Uhuru, Dar ambao wamekuwa wakipata matokeo mazuri zaidi wakiwa hapo.
African Lyon wanaweza kubebwa na matokeo ya mchezo kati ya Prisons na Ndanda. Ikitokea Ndanda ikafungwa, itawafanya wao kuwa na amani sana hata kama nao wakitoka sare na Ruvu ambayo inahitaji pointi moja tu kubaki ligi kuu.
Kama nilivyoeleza hapo juu, Prisons itakuwa haina cha kupoteza itakapokutana na African Lyon baada ya kuifunga Ndanda.
Ruvu Shooting, Mbeya City, Mwadui na Stand United, ni timu ambazo zinahitaji walau pointi moja kubaki ligi kuu katika michezo yao miwili miwili iliyosalia. Ruvu Shooting kwa sasa ina pointi 33, itacheza na African Lyon na Stand United.
Mbeya City nayo ina pointi 33, itacheza dhidi ya Yanga na Majimaji, huku Mwadui ikiwa na pointi 35, itapambana na Mtibwa na Simba, kisha Stand United ambayo nayo ina pointi 35, itakuwa na kibarua mbele ya Simba na Ruvu Shooting.

1 Comment
  1. […] Ligi Kuu Bara msimu ujao itawakutanisha vigogo Simba na Yanga Oktoba 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini kabla, watani hao watakutana Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja huo, katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao huchezwa wiki moja kabla ya kufunguliwa kwa Ligi Kuu Bara. […]

Leave A Reply