The House of Favourite Newspapers

Kwa Hili Dude… Saida Karoli si wa Nchi Hii!!

0

NA BONIPHACE NGUMIJE | IJUMAA WIKIENDA | Over Ze Weekend

MWAKA 2010 staa wa Muziki wa Soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), marehemu Jean de Dieu Makiese ‘Madilu System’ alitoa sapraizi kwa mashabiki wa muziki huo kwa kutoa Kibao cha Sansa ya Papier akichanganya vionjo kwa kutumia nyimbo mchanganyiko zikiwemo Matata ya Muasi, Azda, Mamou, Mario na Liberte zilizoimbwa na Franco Luambo.

Ikiwa imepita miaka saba tangu Madilu abambe na ngoma hiyo ya Sansa ya Papier, Kibongobongo mkongwe wa Nyimbo za Asili, Saida Karoli baada ya kupotea kwenye gemu ya muziki kwa muda mrefu ameibuka naye akiwa amefanya mchanganyiko wa vionjo kama alivyofanya Madilu katika wimbo aliouita Orugambo (Maneno).

Zaidi inanifanya niamini kile ambacho nimekuwa nikiamini siku zote. Kwamba Saida Karoli ni Mwanamuziki wa Nyimbo za Asili mkali, mwenye kipaji cha kuishi muda wote. Na ikiwa atazidi kukomaa ipo siku atavuna matunda anayostahili kwenye muziki.

Siyo siri, Orugambo ni moja kati ya ngoma kali zilizopokelewa vizuri na wapenzi wa burudani kutokana na uwepo wa kuchanganya nyimbo za wasanii watatu wa Bongo Fleva yaani Diamond, Belle9 na Darassa. Tangu itoke ngoma hiyo kati ya marafiki watano wapenzi wa burudani niliokutana nao, wawili kati yao ni lazima wameniuliza; “Umesikia ngoma mpya ya Saida Karoli?”

Achana na hao marafiki, mitaani kwenye vibanda vya kurushia nyimbo pamoja na mitandaoni nako ni gumzo. Wadau mbalimbali wanamzungumzia mwanamama huyu kwa namna ya pekee huku wakionyeshwa kukoshwa na ufundi wa aina ya pekee wa vionjo na sauti iliyochanganywa kutokana na ngoma za wasanii hao kama Salome (Diamond), Muziki (Darassa) na Give It To Me (Belle9).

Saida mwenyewe akizungumza na Over Ze Weekend anasema amefanya hivyo kama njia ya kutoa fadhila kwa wasanii hao ambao wamemrudisha kwenye ramani ya muziki kwa kutumia vionjo vya wimbo wake Maria Salome (Chambua Kama Karanga) kwenye nyimbo zao.

Hata hivyo, pamoja na kuachia dude hilo linalodhihirisha kuwa mwanamama huyo ‘si wa nchi hii’, nina haya ya kumshauri ambayo ni muhimu kuyazingatia;

Kuwa makini na Menejimenti

Binafsi ni miongoni mwa waandishi waliobahatika kuzungumza mambo mengi na Saida kuhusu maisha yake ya muziki. Nilifanya hivyo mapema mwaka huu nilipokuwa nikimuandikia simulizi ya maisha yake kupitia gazeti namba moja la michezo Tanzania, Championi linalotoka Siku ya Jumatatu!

Alisimulia wazi juu ya kufelishwa kimuziki na watu ambao wamekuwa wakisimamia kazi zake namna ambavyo walijitajirisha kupitia muziki wake na yeye kubaki maskini akiambulia pesa zilizomsaidia kujenga ‘kibanda’ cha kuishi maeneo ya Buswelu jijini Mwanza.

Kwa sasa yupo tena chini ya usimamizi mpya. Ingawa yeye mwenyewe hataki kuweka wazi ni nani hasa anayesimamia kazi zake, lakini suala la kukiri tu yupo chini ya menejimenti linanifanya nimshauri kuwa makini yasimkute yaliyomkuta kipindi cha nyuma na hata ‘kumfukia’ asisikike.

‘Kujibrand’ kwenye mitandao ya kijamii

Nina uhakika, Saida anafahamu kuwa katika zama hizi miongoni mwa njia rahisi itakayomsaidia kufikisha kazi zake kwa haraka kwa mashabiki wake ni pamoja na mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram, WhatsApp na Twitter.

Nasema hivyo kwa sababu namuona akimiliki mitandao hiyo. Hata hivyo, kwa jina lake si wa kumiliki wafuasi 2000 kwenye ukurasa wake Instagram. Saida ana mashabiki wengi ndani na nje ya nchi. Anatakiwa kuzidisha juhudi katika kujibrand kwenye mitandao hiyo jambo ambalo litawasaidia pia mashabiki wake kumfuatilia zaidi na kusapoti anachokifanya.

Kutengeneza mazingira ya kujitegemea

Kilichomtokea baada ya kuachana na menejimenti ya zamani Saida anakifahamu. Ilikuwa ni kupotea kwenye ramani ya muziki na kubaki akipiga shoo zaidi pembeni ya Jiji la Mwanza.

Anatakiwa kuwa mfano wa mtu aliyeng’atwa na nyoka, akiguswa na jani tu anashituka. Kwa hiyo katika kufanya kwake kazi anatakiwa kutengeneza mazingira kwamba atakapoachana na menejimenti hiyo basi awe na uwezo wa kusonga mbele katika muziki wake.

Asikosee kwenye kichupa

Ngoma aliyotoa kiukweli ni kali. Kutokana na hadhi yake hata kichupa chake kinatakiwa kiwe kikali zaidi ili kiisapoti zaidi, lakini mbali na kichupa cha ngoma hiyo ya Orugambo hata ngoma zake zinazofuata ahakikishe zinakuwa kali kama ilivyo kawaida yake.

Saida Karoli-Orugambo(New Song 2017)

Leave A Reply